Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mkutano wa kwanza wa Bodi ya Ubunifu wa Kidijitali ya Shirika la Mawasiliano duniani (ITU) umefanyika jijini Geneva, Uswisi huku Tanzania ikitumia fursa hiyo kuelezea uzoefu kwenye masuala ya ubunifu wa kidigiti.

Katika Mkutano huo, Tanzania imewakilishwa kikamilifu na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dk Nkundwe Mwasaga na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta kutoka TCRA Mhandisi Mwesigwa Felician.

Miongoni mwa Manufaa muhimu ya ushiriki wa Tanzania kwenye bodi hiyo na hasa mkutano huo ni pamoja na Tanzania kupata fursa ya kuanzisha kituo cha ubunifu kwa uratibu na ushirikiano kutoka ITU ambapo nchi itapata fursa ya kuendesha kituo kwa utalaamu wa kimkakati ili kuchochea mabadiliko ya ikolojia nzima ya bunifu za TEHAMA ndani ya nchi, kikanda na duniani kwa ujumla.

Akizungumzia Mkutano huo, mjumbe wa Bodi hiyo na mkurugenzi mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kuzindua Bodi pamoja na kujadili kazi zitakazofanywa na chombo hicho pamoja na kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya ubunifu wa kidigiti.

“Hapa tumeangalia njia za kukuza bunifu mbalimbali za TEHAMA, kukuza ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya ubunifu na taasisi zinazojihusisha na ubunifu, tumeangalia namna tunavyoweza kuwa na mfumo utakaowezesha ubadilishanaji wa taarifa za vituo vya ubunifu Duniani,mambo ya haki miliki za ubunifu, ushirikishwaji wa Serikali katika kukuza ubunifu na vipaumbele katika ubunifu hasa bunifu zinazotatua changamoto za jamii,” amefafanua Dk Bakari.

Bodi ya wadau wa Usimamizi wa Bunifu (ITU Innovation Board) inaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mawasiliano ya ITU Dk Cosmas Zavazava ambae ni Mwenyekiti ikiwa na wajumbe 23 ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk Jabiri ni miongoni mwa wajumbe wa bodi hiyo.

Pamoja na wajumbe wa nchi nyingine bara la Afrika linawakilishwa na wajumbe nane kutoka nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Nigeria, Misri, Kenya, Zimbabwe, Gabon na Malawi.

Tanzania imepewa nafasi ya kuanzisha Kituo cha Kitaifa cha Ubunifu wa TEHAMA kitakachosimamiwa na Tume ya TEHAMA ikiwa ni sehemu ya Mtandao wa vituo vya ubunifu (ITU Acceleration Centres) ambavyo vimegawanywa kwenye ngazi ya Kidunia, Kikanda na Kitaifa ukiwa ni mkakati wa ITU kuhakikisha Ubunifu wa TEHAMA unahusika kuchagiza mapinduzi ya kiuchumi katika nchi wanachama ili kuchagiza ukuaji wa uchumi wa kidijiti.

By Jamhuri