ALIZALIWA Oktoba 30, 1960 katika jiji la Buenos Aires, Argentina, kutokana na ndoa ya Diego Maradona na mkewe, Dalma Salvadore ambapo pia naye akaitwa Diego Maradona, kisha akatokea kuwa mwanasoka aliyetamba duniani.

Baada ya kuonyesha cheche tangu akiwa na umri wa miaka minane tu, mtoto huyo alikuja kuwa mwanasoka wa kulipwa kuanzia Oktoba 20, 1976, siku 10 kabla hajatimiza miaka 16 ya kuzaliwa kwake. Timu yake ya kwanza kuichezea soka hilo ilikuwa Argentinos Juniors.

 

 

Miaka mitano baadaye alichukuliwa na Boca Juniors, moja kati ya vigogo wa soka nchini humo. Aliichezea mechi 40 katika misimu miwili, akaondoka na kuvuka bahari na kwenda kucheza soka barani Ulaya mwaka 1982.

Alianzia Barcelona ya Hispania aliyoichezea kwa miaka miwili, akahamia Italia katika timu ya Napoli. Aliporejea tena Hispania mwaka 1992 alijiunga na Sevilla, lakini akadumu nayo kwa msimu mmoja tu na kurudi kwao Argentina.

Huko alijiunga na Newell’s Old Boys, akaichezea hadi mwaka 1994 na kusajiliwa tena na Boca Juniors aliyowahi kuichezea mwaka 1981 – 1982, safari hii akawa nayo kuanzia mwaka 1995 – 1997 alipotundika daluga zake.

Akiwa na timu tano tofauti kwa miaka 21, Maradona alicheza mechi 492 akifunga mabao 258, mengi kati yake akiyafunga akiwa na Argentinos Juniors aliyoichezea mechi 167 na Napoli alikocheza mechi 259, kote akitikisa nyavu mara 115 na hivyo jumla yake kuwa 230.

Ana rekodi ya kutwaa Kombe la Dunia akiwa na vikosi vya aina mbili tofauti vya taifa, kwanza akiwa na timu ya vijana aliyoanza kuichezea Februari 27, 1977 dhidi ya Hungary akiwa na miaka 16 na siku 120.

Alifunga goli lake la kwanza katika timu ya taifa ya wakubwa Juni 2, 1979 wakati Argentina ilipocheza ugenini na Scotland na kushinda kwa mabao 3 – 1 kwenye Uwanja wa Hampden Park.

Akiwa na timu ya taifa ya vijana alishinda Kombe la Dunia mwaka 1979 kabla ya kutwaa taji hilo akichezea timu ya wakubwa miaka saba baadaye.

Alipostaafu mwaka 1994 alikuwa ameichezea mechi 91 na kuifungia mabao 34.

Kama mwanasoka wa kulipwa, Maradona pia ndiye pekee aliyevunja mara mbili rekodi ya uhamisho.

Alianza alipoihama Boca Juniors ya Argentina kwenda Barcelona aliponunuliwa kwa pauni milioni tano (wakati huo), na pale alipotoka timu hiyo kwenda Napoli, aliuzwa kwa pauni milioni 6.9.

Akiwa na Barcelona chini ya kocha César Luis Menotti, Maradona aliiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Mfalme (Copa del Rey) kwa kuwafunga mahasimu wao wakubwa, Real Madrid, kisha ikanyakua Kombe la Hispania kwa kuifunga Athletico de Bilbao.

Wakati alipohamia Napoli, mwanandinga huyo aliifanya timu hiyo kuwa kali zaidi katika historia yake, hatua iliyoongeza mashabiki wake kwa kiwango kikubwa.

Aliiongoza pia kutwaa Kombe la Klabu Bingwa ya Soka ya Italia katika misimu ya mwaka 1986/87 na 1989/90. Ikashika nafasi ya pili mara mbili mwaka 1987/88 na 1988/89.

Mataji mengine aliyoshinda ni Kombe la Italia mwaka 1987, akaiwezesha kushika nafasi ya pili msimu uliofuata na kisha akaiongoza kutwaa Kombe la Chama cha Soka Ulaya (UEFA) mwaka 1989. Aliipatia pia taji la Super Cup mwaka 1990 huku akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu, maarufu kama Serie A mwaka 1987/88.

Akiwa nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Diego Maradona aliiongoza katika kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico kwa kuifunga Ujerumani Magharibi, wakati huo, mabao 3 – 2.

Kwanza alianzia mashambulizi yaliyoing’oa England hatua ya robo fainali kwa kuifunga mabao 2 – 1. Baada ya bao lake la kwanza aliloliita la ‘Mkono wa Mungu’ kulalamikiwa sana, kiungo huyo mshambauliaji aliamua kufunga la pili lililosisimua kuliko yote katika historia ya kabumbu duniani.

Alichukua mpira kutoka umbali wa mita 60 upande wa timu yake, akaanza kuwachambua mabeki mmoja baada ya mwingine hadi wote watano walipokwisha, kisha akahitimisha kwa kipa naye kumlamba chenga na kubaki akiangaliana uso kwa uso na goli lililo wazi.

Aliifungia Argentina mabao matano na kutoa pasi za mwisho zilizozaa mabao matano mengine kati ya 14 iliyofunga timu yake katika fainali hizo.

Katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1990, Ujerumani Magharibi ililipiza kisasi kwa kuichapa Argentina bao 1 – 0 na kutwaa ubingwa.

Alikuwa Andreas Brehme aliyefunga kwa penalti dakika ya 85 baada ya Rudi Völler kufanyiwa madhambi ndani ya kisanduku.

Mwanasoka huyo wa zamani bado anakumbukwa jinsi alivyokuwa akiuchezea mpira anavyopenda, akapiga chenga anavyotaka yeye mwenyewe, akapenya mahali popote, wakati wowote na kuwadhalilisha mabeki kama alivyowafanyia wa timu ya taifa ya England katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986.

Licha ya kimo chake kifupi, lakini umbo lake nene lilikuwa na stamina kuanzia miguuni mpaka kichwani, mshambuliaji aliyekuwa na kila ujuzi anaopaswa awe nao mwanasoka mwenye kipaji kilichopitiliza.

Diego Maradona ambaye jina lake katika lugha ya Kihispaniola inayotumika rasmi hapa Argentina linaandikwa djeɣo maɾaðona, hivi sasa ni kocha wa timu ya Al Wasl ya Dubai.

Ingawa tayari ametundika daluga zake, Maradona ndiye “mwanasoka bora wa muda wote” wa Shirikisho la Kandanda la Dunia (FIFA). Alishinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Karne iliyofanyika kwa uwazi mwaka 1999 na kumtupilia mbali Mfalme wa Kandanda Duniani, Pelé.

Mchuano huo uliendeshwa na mtandao rasmi wa FIFA, jarida la shirikisho hilo na mfumo wa kisheria. Alikusanya asilimia 53.6 akifuatiwa na Pelé aliyepata asilimia 18.53 tu kati ya kura zote zilizopigwa.

Kana kwamba haitoshi, bao la pili aliloifungia Argentina dhidi ya England katika mechi ya robo fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986, liliteuliwa kuwa “bora kuliko yote yaliyowahi kufungwa katika mechi za FIFA”. Aliiwezesha pia timu ya taifa aliyoiongoza huko Mexico kuwa ndiyo “bora zaidi kuwahi kutokea duniani”.

Lakini kwa sababu hakuna kizuri kisichokuwa na kasoro, Maradona pia ana matatizo yake. Alitokea kuwa mtumiaji mkubwa wa mihadarati, akawa teja la kutupwa na kufikia mpaka hatua ya kulazwa mara mbili, tena kwa miezi kadhaa huko Cuba.

Mwaka 1991, wakati huo akiwa na timu ya Napoli ya Italia alifungiwa kucheza kwa miezi 15 alipogundulika kwamba alikuwa anatumia dawa za kulevya aina ya cocaine. Mbali na adhabu hiyo, timu yake ilimpiga faini ya dola 70,000 za Marekani kwa vile angekosekana uwanjani kwa kipindi hicho chote.

Hata hivyo, adhabu hiyo haikuwa lolote wala chochote kwake. Mwaka 1994 alicheza mechi moja tu katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Marekani, akarudishwa nyumbani kwao kutokana na sababu ileile: alipatikana na kosa la kutumia tena mihadarati inayoitwa ephedrine, hatua iliyomfanya kuwa nahodha wa kwanza wa timu ya soka ya taifa kukumbwa na kashfa hiyo.

 Alipokuja kustaafu kucheza kandanda wakati akisherehekea miaka 37 ya kuzaliwa kwake mwaka 1997, Maradona alikuwa tayari amepoteza uzito wake kutokana na kuathirika kwa kiwango kikubwa kabisa na uteja wa mihadarati.

By Jamhuri