Marekani inawezaje kuwa  kiranja wa demokrasia?

Na Nizar K. Visram

Desemba 9 na 10 mwaka huu, Joe Biden, Rais wa Marekani, ameitisha mkutano wa kimataifa kuhusu demokrasia.  

Alizialika nchi 110 katika mkutano wa kilele uliofanyika kwa njia ya mtandao. Licha ya wakuu wa nchi, walialikwa pia wawakilishi wa asasi za kiraia, wafadhili na watendaji wa sekta binafsi. 

Biden alikuwa anatekeleza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni za urais mwaka jana aliposema kuwa atakaposhinda ataitisha mkutano wa kimataifa ili kupambana na udikteta, rushwa na uvunjifu wa haki za binadamu ulimwenguni. 

Hivyo mkutano huu ulilenga kuimarisha misingi ya demokrasia ulimwenguni,  pamoja na kupendekeza mbinu za kupambana na rushwa, kukuza haki za binadamu na uhuru wa habari na kuupiga vita udikteta ulimwenguni.

Inategemewa kuwa baada ya mwaka mmoja utafanyika mkutano mwingine wa ana kwa ana ili kutathmini utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa mwaka huu. Kila mmoja atatakiwa kuelezea hatua zinazochukuliwa katika nchi yake. 

Suala moja limeibuka katika mkutano huu nalo ni kuhusu nchi zilizoalikwa. Wengi wanajiuliza, ni vigezo gani ametumia Biden? Hata hivyo ni dhahiri kuwa mwaliko ulitolewa kwa mujibu wa masilahi ya kimkakati ya Marekani. 

Kwa mfano, Poland ilialikwa licha ya kuwa serikali yake imekuwa dhaifu katika utawala wa sheria na imekuwa ikibana upinzani. Hata hivyo, Biden ameialika nchi hiyo kwa sababu anaitumia kama silaha dhidi ya nchi jirani ya Belarus inayoegemea upande wa Urusi ambayo ni hasimu wa Marekani. 

India na Pakistan nazo zimealikwa lakini si Bangladesh. Ni kwa sababu Marekani inaihitaji Pakistan inayopakana na Afghanistan. 

Hitaji hilo limeongezeka hasa sasa baada ya Marekani kutimuliwa na Taliban nchini Afghanistan. Ingawa inasemekana utawala wa Pakistan unadhibitiwa na majeshi, bado inaalikwa, hata kama nchi hiyo inalaumiwa na Marekani kuwa inawakamata raia na kuwatesa au hata ‘kuwapoteza’ kusikojulikana.

India nayo ni muhimu kwa Marekani kwa sababu inapakana na China, hasimu mwingine wa Marekani. Haidhuru utawala wa India unawagawa raia wake na kuwabagua kwa misingi ya dini, bado inaalikwa katika mkutano wa demokrasia. Bangladesh haina umuhimu huo wa kimkakati.

Singapore haikualikwa ingawa ina uhusiano wa karibu na Marekani. Waziri wa Marekani anayeshughulika na nchi za Asia Mashariki na Pacific, Daniel Kritenbrink, alipoulizwa na wanahabari wa Singapore alijibu: 

“Marafiki zetu wa karibu sana kama Singapore hawakualikwa lakini hiyo haipunguzi hata kidogo ushirikiano wetu na nchi hiyo.” Hata hivyo hakueleza sababu ya kutoalikwa.

Tukigeukia Afrika, tunaona takriban nchi 20 zilialikwa, zikiwamo Angola, Botswana, Namibia, Mauritius, Sao Tome na Principe, Nigeria, Niger, Afrika Kusini, Angola, DR Congo, Ghana, Liberia, Malawi, Zambia, Senegal  na Kenya. 

Hata hivyo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alikataa mwaliko bila kutaja sababu. Waziri wake wa Mambo ya Nje, Naledi Pandor, amesema Ramaphosa alipokea mwaliko siku moja tu kabla ya mkutano!

Nchi kama Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia, Morocco, Misri, Tunisia, Algeria Burundi, Gabon, Equatorial Guinea, Guinea Bissau, Mali, Sierra Leone, Uganda, Tanzania, Msumbiji na Côte d’Ivoire  hazikualikwa. 

Kama nchi hizi hazina sifa za kualikwa inakuwaje Marekani izimiminie misaada ya kijeshi? Ina maana Marekani inazisaidia nchi za kidikteta? 

Nchi nyingine zisizoalikwa ni Hungary, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia na Hungary ambayo ni nchi pekee ya Umoja wa Ulaya (EU) iliyoachwa. 

Kama Saudia na UAE hazina sifa za kualikwa, iweje ziuziwe silaha? Tayari Biden amekubali kuiuzia Saudi Arabia silaha za dola milioni 650.

Wachunguzi wanauliza, iweje Philippines ialikwe na ilhali Serikali ya Marekani imeulaani utawala wake kwa kuwaua raia wasio na hatia?  

Georgia imealikwa bila kujali kuwa asasi ya Marekani iitwayo Freedom House imeripoti kuwa nchini humo serikali na vyombo vya habari vinadhibitiwa na matajiri na mafisadi papa. Halikadhalika Nigeria imealikwa wakati ripoti ya FH inasema nchi hiyo inaruhusu ukamataji na udhalilishaji wa wanahabari. 

Hungary na Uturuki ni nchi wanachama wa NATO lakini hazijaalikwa. Kama nchi hizi hazina sifa ya demokrasia, maana yake hata nchi za kidikteta zinaweza kuwa wanachama wa NATO na zikalindwa na Marekani? 

Ni dhahiri kuwa Urusi na China hazikuwamo katika orodha ya waalikwa kwa sababu lengo kuu lilikuwa ni kuzitenga nchi hizi mbili pamoja na marafiki zao. Wachambuzi wanasema dunia inarudi kwenye enzi za vita baridi. 

Ndiyo maana Biden hakuialika Cuba kwa sababu anaamini kuwa nchi hiyo si ya kidemokrasia. Matokeo yake Cuba imewekewa vikwazo na Marekani kwa zaidi ya miaka 60 – vikwazo haramu visivyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa mujibu wa sheria ya kimataifa. 

Kwa muda wa miaka 30 UN imekuwa ikipitisha azimio kila mwaka likilaani vikwazo dhidi ya Cuba. Mwaka huu nchi 184 zimeunga mkono azimio. Hiyo ni demokrasia ya kimataifa ambayo Marekani inaikataa. 

Huko huko Amerika Kusini nchi nyingine tatu hazikualikwa, nazo ni El Salvador, Guatemala na Honduras. Julai 2020 wakati Biden alipokuwa akigombea urais alitoa mfano wa mafanikio yake makubwa alipokuwa Makamu wa Rais chini ya Barack Obama. 

Alisema akiwa Makamu wa Rais alizisaidia nchi hizo tatu kupambana na rushwa na umaskini. Akafanya jitihada na bunge likaidhinisha dola milioni 750 ili kuzisaidia nchi hizo. 

Biden akajitapa kuwa matokeo yake ni kuziokoa nchi hizo. Biden akashinda urais, lakini katika mkutano wa kilele nchi zote tatu hazikualikwa. Ndipo wengine wakajiuliza, kulikoni?

Tukiachia suala la vigezo vilivyotumiwa katika kuzialika au kutokuzialika nchi, kuna suala la Marekani yenyewe kuitisha mkutano huo. Je, Marekani yenyewe ina sifa gani hata ikajifanya kiranja wa demokrasia ulimwenguni?

Kwa mfano, Januari 6, mwaka huu, makao makuu ya Bunge (Capitol Hill) jijini Washington yalivamiwa na wafuasi wa aliyekuwa Rais Donald Trump, wakipinga Bunge kuidhinisha matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Joe Biden. 

Wakiwa na nondo, mikuki na mashoka walibomoa milango na madirisha na wabunge wakakimbilia mafichoni. Askari mmoja mlinzi akauawa.

Kamati ya bunge inaendesha uchunguzi kuhusu uchochezi wa Trump katika vurugu za Januari 6. Kamati imeagiza kuona nyaraka zake za White House lakini Trump amekwenda mahakamani kuzuia nyaraka hizo zisitolewe.

Wakati huo huo Chama cha Republican kimefaulu katika majimbo 19 kuweka vizuizi kwa wapiga kura, kwa madhumuni ya kuwazuia wapiga kura wa Chama cha Democrats.

Nguvu za kisilaha kutumika katika kuzuia mchakato wa kutangaza matokeo ya uchaguzi ni udhaifu mkubwa uliojitokeza katika demokrasia ya Marekani kama walivyosema waandishi Aaron David Miller na Richard Sokolsky katika Gazeti la Washington Post.

Cliff Albright, mkuu wa asasi iitwayo Black Voters Matter Fund, naye anasema demokrasia ya Marekani ina walakini kutokana na ubaguzi wa rangi na vikwazo kwa wapiga kura. 

Akaongeza: “Hatuwezi kuwa walinzi wa demokrasia ulimwenguni wakati tunashindwa kuilinda nchini mwetu. Huwezi kuzima moto nyumba za jirani wakati nyumba yako inateketea.”

Naye Michael J. Abramowitz, Rais wa FH anasema ni dhahiri kuwa Marekani inayumba wakati huu. Asasi hiyo imetayarisha orodha ya mataifa kuhusu demokrasia na haki za binadamu. Katika orodha hiyo Marekani inashika nafasi ya 50.

Na taasisi ya International Institute for Democracy and Electoral Assistance mjini Stockholm imesema demokrasia ya Marekani imerudi nyuma. Maoni kama haya yametolewa pia na mwandishi Gabriela Bhaskar katika Gazeti la New York Times.

Wanazuoni Martin Gilens na Benjamin walifanya utafiti wakagundua kuwa raia wa kawaida wa Marekani hawana usemi wowote kuhusu jinsi nchi inavyoendeshwa na wanasiasa ambao wanatumiwa na tabaka la matajiri kwa masilahi yao. 

Asilimia 85 ya raia walipoulizwa walisema hawana imani na utawala na wanapendekeza yafanyike mageuzi ya kimfumo. 

[email protected]

0693-555 373