Wiki moja tangu serikali itoe tamko kwamba hakuna ugonjwa wa ebola hapa nchini, Shirika la Afya Duniani (WHO) na kitengo cha kupambana na magonjwa kutoka nchini Marekani (CDC), wamethibitisha kwamba hakuna mlipuko wa ugonjwa huo.

Uthibitisho huo umekuja siku chache baada ya serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuruhusu kuchukua sampuli za wagonjwa waliodhaniwa kuwa na vimelea vya ebola na baada ya kuwapima walithibitisha havikuwa vimelea vya ebola.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi wa CDC, Robert Redfield, aliyewasili nchini kwa ajili ya kuangalia namna Marekani itakavyoweza kushirikiana na Tanzania katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko.

 “Marekani na Tanzania zitaendelea kushirikiana na kusaidiana katika juhudi za kupambana na kudhibiti magonjwa ya mlipuko kupitia Global Health Security,” amesema Redfield.

 Mbali na Tanzania, Redfield atatembelea nchi za Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako kumeripotiwa kuwa na ugonjwa wa ebola.

Mkurugenzi huyo wa CDC amefanya mazungumzo na Dk. Ndugulile ikiwa ni siku chache baada ya serikali kutoa tamko la kutokuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa ebola.

Siku chache zilizopita, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alinukuliwa akisema kwamba tetesi za kuwapo ugonjwa wa ebola hapa nchini si za kweli.

 “Mpaka sasa hakuna mgonjwa aliyethibitika kuwa na ugonjwa huo na kwamba serikali inaendelea kuchukua tahadhari kudhibiti ugonjwa huo,” alinukuliwa Waziri Ummy.

 Tetesi hizo zilichunguzwa zaidi na Shirika la Afya Duniani (WHO) baada ya kusambaa kwa tetesi kwamba kuna ugonjwa usiojulikana na bado wanazidi kufanya uchunguzi wa tetesi hizo.

Tangu Agosti mwaka 2018 DRC ilipobainika kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo, hadi Agosti 12, mwaka jana jumla ya wagonjwa 3,099 walikuwa tayari wamefariki dunia.

Dalili za ugonjwa huo wa ebola ni kuharisha, maumivu ya viungo vya mwili, kuumwa kichwa kutokwa vipele mwili mzima, kutapika damu na ugonjwa wa akili.

Kufuatia hali hiyo, serikali imechukua tahadhari kwa kununua vifaa vya mkononi vya kupimia joto 2,700 na mavazi kinga na kusambaza katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Kigoma, Rukwa, Katavi na Dar es Salaam.

 Serikali imetoa mafunzo kwa watumishi 460, mafunzo hayo yametolewa kwenye kanda mbalimbali zisizopungua 264 wakiwemo waendesha bodaboda.

856 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!