Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umemfurusha Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, katika nyumba ya serikali anayoishi jijini Dodoma, baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umethibitisha.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba mbunge huyo alishindwa kukamilisha kulipa deni la pango linalofikia takriban Sh milioni 7, hata baada ya muda wa notisi ya siku 14 iliyotolewa na TBA kuwa imekwisha.

TBA kupitia mawakala wao wa kuondoa wapangaji, walifanya kazi ya kuondoa vyombo vya Mbunge Ridhiwani Kikwete kabla ya dakika chache baadaye kupigwa simu kutoka ‘juu’ yenye maelekezo kwamba fedha hizo zitalipwa na mmoja wa vigogo serikalini.

“Tulishaanza kutoa vitu katika nyumba hiyo, baadaye tukaambiwa na watu wa serikalini kwamba tusitishe kwanza. Tuliambiwa kwamba fedha hizo zitalipwa na…(jina tumelihifadhi).

 “Nimeshangaa sana kwa kweli kuona kwamba kumbe mambo ya kulindana bado yapo, maana wengine waliondolewa isipokuwa huyu,” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI limemtafuta Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia sekta ya Ujenzi, Arch Elius Mwakalinga, ambaye amesema atafutwe mtendaji mkuu wa TBA.

 “Kuhusu masuala ya wadaiwa sugu wa Wakala wa Majengo Tanzania, naomba uwasiliane na Mtendaji Mkuu, maana wao ndio walikuwa wanatoa invoice na kupokea malipo,” amesema Mwakalinga.

Hata hivyo, chanzo chetu kingine kutoka ndani ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kimeliambia JAMHURI kwamba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ndiye aliyeamua kuingilia kati kumnusuru Ridhiwani na fedheha ya kufungashiwa virago.

“Nilisikia Waziri Mkuu ndiye ameamua kuingilia kati suala hili na kuahidi kwamba fedha hizo atazilipa yeye…bado tunaendelea kusubiri atimize ahadi yake,” kimesema chanzo chetu.

Jitihada za Gazeti la JAMHURI kumtafuta Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pamoja na wasaidizi wake kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo hazikufanikiwa. JAMHURI lilitaka kufahamu kutoka kwa Waziri Mkuu endapo ametekeleza ahadi ya kulipa deni hilo.

Gazeti la JAMHURI limemtafuta Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ajibu tuhuma.

“Naomba unisikilize mimi, maana mimi ndiye mhusika. Ninakwambia kwamba sijanyang’anywa nyumba Dodoma. Suala hilo kama umeambiwa na Meneja wa TBA Dodoma andika, ila kama ni habari za mtaani naomba usiandike.

 “Suala la kwamba nimenusuriwa na Waziri Mkuu, si sahihi tena ninakuomba kaka usimuingize PM (Waziri Mkuu)… Ridhiwani anatafutwa na watu wengi, wewe ni rafiki yangu usiingie kwenye mambo hayo,” Amesema Ridhiwani.

 Alipoulizwa na JAMHURI endapo amelipa deni lake au la, hakukanusha wala kukubali, isipokuwa akasisitiza kwamba mwandishi wa JAMHURI aende kwenye nyumba yake jijini Dodoma na kushuhudia endapo ameondolewa kama inavyodaiwa.

“Kaka mtume mwandishi wako aende nyumbani kwangu Dodoma, atakuta bado ninaendelea kuishi kwenye nyumba hiyo… sijaondolewa kwenye nyumba kama inavyosemwa. Mwambie aende nyumbani kwangu, hakuna shida yoyote,” amesema Ridhiwani alipozungumza na JAMHURI.

Ridhiwani ni mmoja wa wapangaji wa nyumba za Serikali jijini Dodoma, amepangishwa nyumba hiyo kutokana na wadhifa alionao wa Ubunge. Yeye ni mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Chalinze, kupitia tiketi ya CCM.

Julai mwaka huu, TBA ilitoa notisi ya siku 14 kwa wapangaji wote wa nyumba za serikali kulipa madeni yao huku ikiwataka wapangaji wasio na sifa kuishi kwenye nyumba za serikali kuhama mara moja katika muda uliotolewa.

Tangazo hilo lilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki – TBA, Said Mndeme. Alinukuliwa akisema moja ya majukumu ya TBA ni kupangisha nyumba za serikali kwa watumishi wa umma na taasisi za serikali, pia wanapangisha baadhi ya nyumba za serikali kibiashara.

Mndeme alinukuliwa akisema kwamba mpaka sasa wanadai madeni zaidi ya Sh bilioni 10 kutoka kwa wapangaji wao, ikiwa ni malimbikizo ya kodi ya pango.

“Tuliwapa notisi ya siku 30, sasa tumeongeza siku 14. Baada ya muda huo kwisha, TBA tutafanya kazi ya kuwaondoa kwa nguvu wadaiwa wote kwenye nyumba zetu na kwenye maeneo tuliyowapangisha,” amesema Mndeme.

Alinukuliwa akisema TBA imedhamiria kuwafikisha mahakamani wale wote walioondoka au kuondolewa kwenye nyumba kwa sababu mbalimbali na kuondoka wakiwa na madeni ya kodi ya pango.

Mkurugenzi huyo amewataka wapangaji wasio na sifa za kukaa kwenye nyumba za serikali kuhama mara moja. Watu hao wasio na sifa ni pamoja na watumishi wa umma waliohamia vituo vipya, watumishi waliostaafu, watumishi waliofariki dunia na familia zao zikaendelea kuishi kwenye nyumba za TBA na watumishi waliofukuzwa kazi kwa sababu mbalimbali.

Wakati huohuo, Februari mwaka huu, TBA iliwaandikia notisi ya kuwatoa kwenye nyumba watumishi 23 waliouziwa nyumba za serikali, wakashindwa kukamilisha malipo yao kwa wakati, wanaodaiwa takriban Sh milioni 108.4.

Mwaka 2002 Serikali ya Awamu ya Tatu ilitangaza kuuza nyumba zake kwa watumishi wa umma, ambapo ilitoa miaka 10 kwa wanunuzi kukamilisha fedha za ununuzi wa nyumba hizo.

Serikali iliwapatia miaka 25 ya kuishi kwenye nyumba hizo bila ya kubadilisha matumizi. Muda wa miaka 10 wa kukamilisha malipo ya fedha za umiliki wa nyumba ulishapita.

TBA imekuwa ikifuatilia malipo hayo na kwa sasa imewaandikia waraka (notice), wenye kuelezea kusudio la kufuta mikataba ya kuwauzia nyumba hizo.

Alisema watumishi waliouziwa nyumba hizo, kwa awamu ya kwanza hadi ya tano, kwa kipindi cha marejesho ya mkopo cha miaka 10, ni watumishi 7,539.

Wapo watumishi waliobadilisha matumizi ya nyumba hizo kabla hata ya miaka 25 waliyopewa kuisha kwa kuwa miaka hiyo inakwisha mwaka 2027.

Wapo ambao wameshabadilisha matumizi hayo ya nyumba na kujenga nyumba za kisasa za kupangisha (apartments), hasa maeneo yaliyokuwa adhimu, kwa maana ya waliyokuwa wakiishi watumishi wa ngazi za juu serikalini kama vile Oysterbay, Masaki, Upanga na Mikocheni, Dar es Salaam.

Wapo ambao wameingia ubia na kujenga maduka makubwa, ofisi na hata baa au kumbi za burudani.

Kwa kuwa uuzwaji wa nyumba hizo ulifanyika nchi nzima, hivyo ni wazi kuwa kuna maeneo mengine ya mikoani, ambayo pia matumizi ya nyumba hizo yamebadilishwa kabla ya muda huo.

JAMHURI linafahamu kwamba wapo watu waliobadilisha matumizi ya nyumba hizo ilhali bado hawajamaliza kulipia nyumba walizouziwa.

Ifahamike kuwa waliouziwa nyumba hizo waliuziwa bila ya nyongeza ya asilimia yoyote, kwa maana ya fedha ya faida, licha ya kuwa nyingi ya nyumba hizo zilikuwa kwenye maeneo muhimu ya kibiashara.

Hata hivyo, wapo ambao hawajamalizia kuzilipia. Katika mkataba, waliouziwa nyumba hizo hawatakiwi kufanya matengenezo makubwa na kama kuna haja ya kufanya matengenezo makubwa ya nyumba hizo, wanatakiwa kupewa kibali na TBA.

By Jamhuri