Serikali imewaondoa wasiwasi wananchi kuhusu taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa ugonjwa wa Ebola nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ametoa ufafanuzi huo jijini Dar es Salaam kutokana na taarifa zinazozagaa kuhusu uwezekano wa kuwepo virusi vya Ebola.

Waziri Ummy amesema taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na baadhi ya vyombo vya habari si za kweli, huku akisisitiza kuwa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitika kuwa na ugonjwa huo.

Amewasihi wananchi kutokuwa na hofu juu ya ugonjwa huo kwani tangu ulipothibitika kuwepo nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Agosti mwaka jana, serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa usiingie nchini.

Waziri Ummy amesema serikali imeimarisha uratibu na ufuatiliaji wa ugonjwa huo kupitia kwa wataalamu wa afya katika mikoa, wilaya na maeneo ya mipakani, ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi kwa wageni wanaoingia nchini kupitia mipakani.

Ummy amesema serikali imenunua vifaa mbalimbali vikiwemo vipima joto vipya vya kutumia mkono  ambavyo wasafiri wanaotoka nchi jirani zinazohisiwa kuwa na ugonjwa huo wamekuwa wakipima.

“Serikali imenunua na kusambaza takriban seti 2,700 za mavazi  kinga kwenye mikoa yote iliyo katika hatari ya kukumbwa na tishio la ugonjwa wa Ebola ambayo ni Kagera, Kigoma, Mwanza, Rukwa na Katavi, ambayo inapakana na DRC.

 “Ni katika muktadha ule ule wa kujiandaa serikali imenunua vifaa hivi ili itakapohisiwa au kutokea mlipuko wa ugonjwa huo tuwe tayari kukabiliana nao,” amesema Waziri Ummy.

Waziri huyo amesema serikali imeandaa kitini chenye maelezo muhimu ya jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo, nakala za kitini hicho zimetumwa kwa waganga wakuu wa  mikoa yote nchini pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa unavyoenezwa na namna ya kujikinga.

“Tumetoa mafunzo kwa watumishi wa afya zaidi ya 460 na watu 264 kutoka ngazi ya jamii, tumetoa mafunzo kwa viongozi  wa dini, bodaboda pamoja na watendaji wa vijiji katika mikoa iliyo hatarini.

“Pia tumeimarisha utambuzi wa ugonjwa wa Ebola kwa kujenga uwezo katika maabara yetu kuu ya taifa iliyoko Dar es Salaam, hospitali ya rufaa ya kanda iliyoko Mbeya na kituo cha utafiti wa magonjwa na tiba kilichopo KCMC Moshi,” amesema Ummy.

Amesema ugonjwa wa Ebola umeendelea kuripotiwa kuwepo katika nchi jirani na kusisitiza kwamba wizara inawakumbusha wananchi kuchukua hatua stahiki za kujikinga na ugonjwa huo huku akizitaja dalili kuu za ugonjwa huo kuwa ni homa kali, kutapika na kuhalisha, viungo vya mwili kuuma, kuumwa kichwa, kutokwa vipele mwilini pamoja  na kutokwa damu katika matundu ya mwili.

Amewataka wananchi katika mikoa yote ya nchi kujiepusha kugusa damu, mikojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.

Pia amewataka wananchi watoe taarifa mapema kwa viongozi wa serikali na kwa wahudumu wa afya katika vituo vya afya pale anapojitokeza mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa huo ama kuaga dunia kutokana na dalili hizo.

Waziri Ummy amezitaja namba ambazo wananchi wanatakiwa kutoa taarifa za uwepo wa mtu mwenye dalili za ugonjwa huo ambazo amesema ni 0800110124 au 0800110125.

“Utamaduni wetu wa kupeana mikono tunatakiwa tuuzingatie, tunapopeana mikono tunawe mikono mara kwa mara kwa maji yanayotiririka  kwa kutumia sabuni,” amesema Ummy.

Wakati huo huo, Waziri wa Afya ameagiza waganga wakuu wote wa mikoa na wilaya zote nchini kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wizara hususan kuzingatia taratibu za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na waganga hao kutoa maelekezo hayo kwa vituo vyote vya afya vya serikali na watu binafsi

Kuhusu uvumi wa taarifa za kuwepo kwa ugonjwa  huo hapa nchini zimetokana na kuwepo kwa wahisiwa wawili wa ugonjwa Ebola, ambapo tayari serikali imechukua sampuli na kuzifanyia uchunguzi na kuthibitisha wagonjwa hawakuwa na virusi vya Ebola.

Hata hivyo, amesema dhamana ya kutoa taarifa ya magonjwa ya milipuko ikiwemo Ebola ni waziri wa afya kwa mjibu wa sheria, huku akisisitiza kuwa kutoa uvumi wa taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii ni kukiuka Sheria ya Makosa ya Mitandaoni ya mwaka 2015 na Sheria ya Huduma ya Habari namba 12 ya mwaka 2016.

Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuratibu na kudhibiti magonjwa ya milipuko ikiwemo Ebola.

Ikumbukwe kuwa tangu ugonjwa huo kuripotiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Agosti mwaka jana, hadi kufikia Septemba mwaka huu watu 3,099 wamethibitika kuwa na ugonjwa huo wa Ebola.

Ebola ni ugonjwa gani?

Ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi cha Ebola, ambacho kina uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2014, inasema kwa mara ya kwanza ulibainika mwaka 1976 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ( DRC) na Sudan.

Chanzo cha kirusi hiki hadi sasa hakijajulikana, lakini popo aina ya Pteropodidae wanaonekana kuwa wabebaji wa kirusi hicho.

Ugonjwa wa Ebola unaonekana kuzikumba kwa kiasi kikubwa nchi za Afrika Magharibi huku mlipuko mkubwa ukitajwa kusababisha maambukizi ya binadamu kwa binadamu kuliko wanyama.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha kwamba vifo vingi vinavyotokana na kirusi cha Ebola hutokea kwenye mazishi au mila za mazishi, ambapo katika shughuli hizo waombolezaji wanagusana na mwili wa marehemu, hivyo kujiweka haratini.

480 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!