Juliana Philipo, mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam, amedanganya katika Kituo cha Polisi  Kigamboni ili asaidiwe kupata hati ya kifo cha ‘mumewe’.

Aliwaambia polisi kwamba amepoteza kibali kilichotumika kusafirisha mwili wa mzazi mwenzake, Charles Reuben, aliyefariki dunia Julai 28, mwaka huu baada ya kufunikwa na kifusi cha makaa ya mawe akiwa kazini katika Kiwanda cha saruji cha Nyati kilichopo Kimbiji – Kigamboni.

Amewadanganya polisi wa kituo hicho wakampatia barua ili aweze kuomba namba ya kibali kilichotolewa na Kituo cha Afya  Vijibweni wakati wa kusafirisha mwili wa Reuben kwenda kuzikwa Katoro, mkoani Geita.

Gazeti la JAMHURI limeona nakala ya kibali halisi cha kusafirisha mwili huo chenye namba 0744660, kilichotolewa Julai 28, mwaka huu, ambacho yeye anadai kimepotea ilhali kimetunzwa na ndugu wa marehemu anayefahamika kwa jina la James Reuben.

Inadaiwa kwamba baada ya kupata namba hiyo ameitumia kuambatanisha kwenye nyaraka alizopeleka ofisi za Wakala wa Ufilisi, Usajili na Udhamini (Rita) ili aweze kupata hati ya kifo cha Reuben kwa ajili ya kufungua shauri la mirathi mahakamani.

Sambamba na hilo, inadaiwa kuwa ametumia namba hiyo kuweka zuio mahakamani ili ndugu wa marehemu wasiendelee na juhudi za kufuatilia mirathi hiyo, ambapo kiapo cha kushughulikia shauri la mirathi hiyo kimefunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo Katoro, Geita.

Pamoja na juhudi za Juliana kutaka mirathi ya marehemu mume wake (Charles Reuben), ndugu wa marehemu wanakataa kumtambua katika mirathi hiyo, kwani wanadai yeye hakuwa mke wa ndoa wa marehemu na kwamba kabla ya mauti kumkuta walikuwa hawakai pamoja kwa takriban miaka saba.

James Reuben,  kaka wa marehemu amelieleza JAMHURI kuwa ndugu yake ameacha watoto watatu aliowapata kwa Juliana lakini watoto hao hawampi uhalali mwanamke huyo kuwa mrithi wa mali za marehemu, kwani yeye hakuwa mke wake wa ndoa, hivyo wao kama ndugu hawamtambui bali wanawatambua watoto peke yao aliowaacha marehemu.

Kutotambulika kwa Juliana katika familia hiyo, James anakueleza kusababishwa na vitendo vya kikatili ambavyo mwanamke huyo alimfanyia ndugu yao enzi za uhai wake, ambavyo ndivyo vilisababisha kuacha nyumba aliyoijenga Chanika na kuikimbia familia.

 “Kaka yangu alinyanyaswa mno na huyo mwanamke (Juliana), alimfanyia vituko hadi nyumba ya Chanika akaihama, aliishi mitaani kwa kufanya kazi zisizoeleweka, mpaka anakufa alikuwa hana uwezo wa kwenda nyumbani kwake kwani aliwekewa sharti kuwa akitaka kwenda kuonana na watoto wake lazima atoe taarifa na si vinginevyo,” anaeleza James.

Awali Juliana aliliambia Gazeti la JAMHURI kuwa yeye ndiye mke wa ndoa wa marehemu Charles Reuben na kwamba wameoana kihalali huku akisisitiza kuwa na cheti cha ndoa kinachothibitisha uhalali huo.

Amesema ndugu wa marehemu anayefahamika kwa majina ya James Reuben na dada wa marehemu anayeitwa Sara Reuben wanamnyanyasa huku wakiingilia suala la kufuatilia fidia wanayotakiwa kupewa na Kiwanda cha saruji cha Nyati pamoja na mirathi.

“Wakati ajali inatokea mimi sikupewa taarifa, aliyeanza kupewa taarifa ni dada yake anayekaa Kigogo anaitwa Sara. Mimi siku ya tukio nilikuwa kwenye gari muda wa saa mbili nikielekea Kariakoo, nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama mfanyakazi mwenzake na mume wangu akaniuliza wewe ndiye Mama Robin?  Nikamjibu ndiyo! Akaniambia… Charles anaomba aletewe watoto wake.

“Huyo mtu alikata simu halafu baada ya muda akapiga tena na kuniambia…Charles anaumwa sana, akakata simu tena, nilipompigia mimi akanijibu kuwa anaumwa sana hawezi kuongea,” amesema Juliana.

Anakumbuka zilipita kama dakika 20 akapigiwa simu na wifi yake wa Kigogo (Sara Reuben) ambaye alimweleza kuwa Charles Reuben amepata ajali akiwa kazini na kwamba amefariki dunia.

Wakati taarifa hiyo inamfikia ilikuwa saa tatu asubuhi na kuelezwa kuwa anatakiwa kujiandaa afunge nguo na kuwaandaa watoto kwa ajili ya kusafiri kwenda Geita kwenye mazishi.

Mama huyo ameliambia JAMHURI kuwa walikwenda Kituo cha Polisi Kigamboni kwa ajili ya kupata taarifa juu ya tukio hilo na kwamba walielezwa na mpelelezi wa wilaya (OCCID) kuwa kifo cha Charles Reuben kimetokea kwa sababu ya uzembe wake, kwani hakuwa amefunga mkanda.

“Mimi niliomba kabla ya kusafirisha mwili twende kwenye eneo la tukio lakini polisi wakaniambia kwamba haitasaidia chochote kwani hata wao wamekagua wakabaini kuwa marehemu ndiye mwenye makosa, kwani eneo hilo lina usalama wa kutosha,” amesema Juliana.

Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kigamboni, Mrakibu wa Polisi (SP) Thobias Walelo ameulizwa na Gazeti la JAMHURI kuhusu taarifa ya kifo cha Charles na kusema anayepaswa kutoa taarifa za tukio hilo ni Kamanda wa Polisi Temeke.

Hata hivyo amekana kutoa taarifa za kifo cha Charles Reuben kwa ndugu yeyote huku akisema tangu tukio hilo kutokea hakuwahi kumwona ndugu yeyote akija kituoni hapo kulalamika wala kudai taarifa za tukio hilo.

“Nakumbuka siku ya tukio walikuja tukakaa hapa ofisini kwangu, tukaongea vizuri wote wakakubaliana kwa pamoja kusafirisha mwili, huyo mwanamke nakumbuka alikuwepo naye alikubali na tangu kipindi hicho sijamuona tena, hayo ya kusomewa taarifa za kifo kusababishwa na uzembe wake nayasikia kwako, sisi hatujatoa ripoti ya namna hiyo na hata wakitaka kuipata wao kama ndugu watatakiwa kuja kuomba, wataelezwa tu, hakuna tatizo,” amesema Walelo.

Wakati akiwa amechafua hali ya hewa Polisi Kigamboni, Juliana anaulalamikia uongozi wa Kiwanda cha saruji cha Nyati kuegemea upande wa ndugu wa marehemu na kumtenga wakati yeye ndiye aliyetakiwa kupewa kipaumbele, huku akikosoa kitendo cha uongozi huo kutoa mkono wa pole wa Sh milioni tatu kwa ndugu wa marehemu huku yeye akiambulia Sh milioni moja tu.

Ofisa Utumishi wa Kiwanda cha Nyati, Julieth Domel, ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa katika nyaraka zilizowasilishwa na Charles Reuben ofisini kwake wakati wa kusaini mkataba wa ajira hakuonyesha kama ana mwanamke wala watoto, bali walioorodheshwa katika nyaraka za mkataba wake wa ajira ni ndugu wa karibu, akiwemo dada yake (Sara Reuben).

Kuhusu utaratibu wa mirathi amesema hawana tatizo nao, bali kinachotakiwa ndugu wa marehemu wakae pamoja na kumchagua msimamizi atakayeshughulikia shughuli zote na kwamba mahakama itakapowaandikia barua na kutakiwa kulipa watalipa bila kuchelewa.

By Jamhuri