WASHINGTON, MAREKANI

Serikali ya Marekani imewawekea vikwazo viongozi kadhaa wa Cuba wakidaiwa kukiuka haki za binadamu wakati wa maandamano yaliyofanyika mapema mwezi huu.

Kitendo hicho cha utawala wa Rais Joe Biden kimekuja katikati ya shinikizo kutoka kwa raia wa Marekani wenye asili ya Cuba wakimtaka kuingilia kati.

Kwa sasa Marekani inatafuta njia ya kurejesha mtandao wa internet kisiwani humo.

Maandamano ya Julai 11, mwaka huu ndiyo makubwa kuwahi kutokea ndani ya miongo kadhaa. 

Mamia ya watu walikamatwa huku raia mmoja akiuawa.

Cuba inadai kuwa maandamano hayo pamoja na matatizo mengine mengi vimechagizwa na vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na Marekani. Marekani inasema inawaunga mkono raia wa Cuba katika kudai haki zao.

Waandamanaji wanadai kukasirishwa na kuanguka kwa uchumi, uhaba wa chakula na dawa, kupanda kwa bei na namna serikali inavyopambana na Covid-19.

Vikwazo hivyo vilitangazwa wiki iliyopita vikimlenga Waziri wa Ulinzi, Jenerali Alvaro Lopez Miera na vikosi maalumu vya Wizara ya Mambo ya Ndani, vinazuia miamala yote na Marekani.

“Huu ni mwanzo tu. Marekani itaendelea kuweka vikwazo kwa mtu mmoja mmoja aliyehusika na ukandamizaji wa watu wa Cuba,” inasema taarifa ya Rais Biden.

Wakati wa kampeni za urais, Biden aliahidi kubadili sera za aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, dhidi ya uchumi na usafiri.

Mwaka 2015, Rais Barack Obama, alirejesha uhusiano wa kidiplomasia na Havana.

By Jamhuri