Marekani yamnyooshea kidole Mtanzania

*Yamtuhumu kushiriki ugaidi, kusambaza silaha Msumbiji

CAPE TOWN

Afrika Kusini

Peter Charles Mbaga, raia wa Tanzania, anatajwa na Idara ya Fedha ya Marekani kama mmoja wa watu wenye uhusiano na kikundi cha kigaidi cha Msumbiji, ISIS-Mozambique.

Mbaga anayefahamika pia kama Abu Kaidha, anatajwa na idara hiyo nyeti ya Marekani yenye jukumu la kufuatilia mzunguko na mwenendo wa fedha safi na chafu ndani na nje ya taifa hilo, kuwa mtu anayewasaidia magaidi kupata silaha kutoka Afrika Kusini.

Kikundi cha kigaidi cha ISIS-Mozambique kilichokuwa kikipambana na majeshi ya Serikali ya Msumbiji, kwa sasa kinaelekea kusambaratika baada ya mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC) kupeleka majeshi kuzima ugaidi.

Takriban watu 4,000 wanadaiwa kuuawa huku wengine 800,000 sawa na nusu ya wakazi wa Jimbo la Cabo Delgado lililopo kaskazini mwa Msumbiji wakiyahama makazi yao kutokana na mgogoro uliodumu kwa miaka minne sasa.

Askari wa Rwanda na Afrika Kusini wanashirikiana bega kwa bega na wanajeshi wa Msumbiji kupambana na magaidi hao ambao Marekani sasa wanaamini kuwa Mbaga ndiye msaada mkubwa kwao katika kupata silaha.

“Yeye pamoja na watu wengine watatu wanasaidia magaidi kununua silaha kutoka katika masoko ya Afrika Kusini,” inasomeka taarifa ya Idara ya Fedha ya Marekani iliyotolewa wiki iliyopita na kusainiwa na Brian Nelson.
Kitengo cha Udhibiti wa Mali za Nje (OFAC) ndani ya Idara ya Fedha kinasema Mbaga na wenzake watatu ambao wote wanaishi Afrika Kusini, ndio kiungo kati ya magaidi wa Dola ya Kiislamu wa Iraq na Syria (ISIS) na washirika wao wa Msumbiji (ISIS-M). 

“Hawa watu wanne wanashiriki kwa kiwango kikubwa kuwezesha mkondo wa fedha kutoka kwa wanachama wa juu wa ISIS kuvifikia vikundi vya kigaidi vilivyopo maeneo mbalimbali ya Afrika,” anasema Nelson na kuongeza:

“Kwa hiyo idara imeamua kuwaweka hadharani watu hawa wanaotumia mfumo wa kifedha wa Afrika Kusini kusaidia mtandao wa ISIS barani Afrika.” 

Anasema Marekani inafanya kazi kwa kushirikiana na nchi marafiki barani Afrika, ikiwamo Afrika Kusini, kusambaratisha mitandao ya kifedha ya ISIS. 

“Katika siku za karibuni ISIS wamejaribu kupenyeza ushawishi barani Afrika hasa maeneo ambako udhibiti wa serikali ni mdogo. Vyanzo vya mapato kwa ISIS barani Afrika huwa ni kwa njia za wizi, utekaji nyara na kudai ‘kikombozi’, pamoja na fedha kutoka Uarabuni,” inasomeka taarifa hiyo.

Watu wengine ambao idara hiyo inawamulika ni raia wa Afrika Kusini, Farhad Hoomer (au Farhad Omar; Farhaad Umar; Farhad Umar), anayeishi Kwazulu Natal na Siraaj Miller, mkazi wa Cape Town. 

Pia yupo Abdella Hussein Abadigga (au Abdella Asid Abadigga; Abdallah Asid Abadika; Abdallah Usseni; Abu Hamza; Abdi Carlos), mkimbizi kutoka Ethiopia anayeishi Johannesburg. 

Abadigga anamiliki misikiti miwili anayoitumia kukusanya fedha kwa ajili ya ISIS, akitumia jukwaa linalofahamika kama ‘hawala’.
Kiongozi wa ISIS nchini Somalia, Bilal al-Sudani, anamchukulia Abadigga kama mtu muhimu na wa kutegemewa, mwenye uwezo wa kuwaunganisha waungaji mkono wa ISIS wa Afrika Kusini kujiimarisha na kuingiza wanachama wapya.
JAMHURI limezungumza na maofisa kadhaa wa Interpol-Tanzania kutaka kufahamu iwapo kuna taarifa za Mbaga katika kumbukumbu zilizopo nchini.

Mmoja wa maofisa hao (jina linahifadhiwa), ameliambia JAMHURI kuwa upo mchakato katika kutafuta na kufahamu taarifa za mtu yeyote anayetuhumiwa kimataifa kwenye kanzidata za idara hiyo.

“Tusifanye haraka. Hizi ni taarifa nyeti. Zinahitaji kuwa na namba ya kumbukumbu ili baadaye taarifa zisije kuleta matatizo,” amesema ofisa huyo akiahidi kutoa taarifa kamili wiki hii.