Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Ruvuma

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma kuwakamata wafugaji wanaoingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kuwachukulia hatua za kisheria. 

Amesema haridhishwa na kasi ya jeshi hilo katika kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji Mkoani humo ambapo matukio ya wafugaji yakuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima yanaongezeka na kusababisha uharibifu wa mazao kutokana na askari kutofanya wajibu wao ipasavyo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akisalimiana na Viongozi wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma wakati alipokuwa anawasili Kituo Kikuu cha Polisi Tunduru Wilayani humo,

Masauni ametoa kauli wakati akizungumza na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wa Wizara yake, Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma, leo wakati alipofanya ziara ya siku moja kutatua mgogoro wa wakulima na Wafugaji mkoani humo.

“Kazi yenu Polisi ni kulinda raia na mali zao, lakini bado hamnifurahishi katika kushughulika na migogoro ya wakulima na wafugaji, wananchi wametumia muda mrefu kuandaa mazao yao kwa ajili ya chakula na pia biashara ambapo watakapouza mazao hayo nchi itafaidika kwa kupata kodi, lakini wanatokea baadhi ya wafugaji wanaingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kufanya uharibifu mkubwa, hii haiwezekani katika Serikali ya awamu ya sita ambayo inataka haki,” amesema Masauni. 

Amesema Serikali ta Rais Samia Suluhu Hassan inawajali askari na imewatendea mambo mengi ikiwemo kukamilisha mahitaji yao ikiwemo kupandishwa vyeo kwa askari, kushughulikiwa kwa stahiki za askari, kutoa mafunzo, kutatua changamoto ya ofisi pamoja na kutoa ajira.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akisalimiana na Viongozi wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma wakati alipokuwa anawasili Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kwa ziara ya kikazi,

“Mheshimiwa Rais nampongeza kwa kujali askari, amewajali sana na mnalijua hilo, fanyeni kazi ni wajibu wenu, mambo mengi ameyafanya mama kwa majesho yote ikiwemo Wizara hii, amewapandisha vyeo askari, ameshughulikia stahiki za askari, kupitia Bajeti ya Bunge ameongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya stahiki za askari polisi pamoja na vitendea kazi kutoka Bilion 900 mpaka Trilion 1.12 na kuwapo kwa mpango wa kununua magari mapya kwa Polisi wilaya zote Tanzania,” amesema Masauni.

Hata hivyo, Masauni amewapongeza askari kwa utendaji kazi wao wanaoufanya na kuwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kuhakikisha wanawatumikia wananchi kwani kodi zao ndio zinazofanya kulipwa mishahara na posho mbalimbali.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Alfred Hussein amemshukuru Waziri Masauni kwa kufika Mkoani humo na kuahidi kuyatendea kazi maelekezo yoye aliyoyatoa katika ziara yake hiyo

By Jamhuri