“Kila mwananchi anataka maendeleo, lakini si kila mwananchi anaelewa masharti ya maendeleo, sharti moja kubwa ni juhudi. Sharti la pili la maendeleo ni maarifa. Juhudi bila maarifa haiwezi kutoa matunda bora kama juhudi na maarifa.”

Nimenukuu maneno haya kutoka katika Azimio la Arusha lililotokana na mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU, iliyokutana katika Community Centre ya Arusha kuanzia Januari 26 hadi 29, 1967 na kutangazwa rasmi Februari 5, 1967 na aliyekuwa Rais wa TANU, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Nimekumbuka kifungu hicho cha maneno kutokana na kilio cha muda mrefu cha wananchi kutaka maendeleo, lakini bado kufanikiwa hadi sasa. Zipo sababu, ikiwemo kuliweka kando Azimio la Arusha.

Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), maendeleo maana yake ni upigaji wa hatua kutoka hali duni kwenda bora zaidi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Ukweli nakusudia kuzungumzia mafanikio ya mtu binafsi, jumuiya na taifa. Naangalia ufanisi kwa maana ya utekelezaji wa mambo na ustawi kwa maana ya mtu kuwa na mali nyingi kwa njia ya halali na maisha mazuri.

Je, wananchi tangu tupate uhuru mwaka 1961 na kuwa na Azimio la Arusha mwaka 1967, maendeleo tuliyoyataka tumeyapata? Jibu ni wazi, hapana. Zipo sababu za kukosa mafanikio, yakiwemo masharti ya maendeleo, kuanzia kwa mtu binafsi, jumuiya hadi taifa.

Juhudi ni kufanya jambo kwa kutumia akili, maarifa, ujuzi, weledi na nguvu alizonazo mtu ili kujiletea maendeleo. Ni kufanya bidii na kuweka dhamira ya kufanya kazi na nia moyoni.

Maarifa ni ujuzi aghalabu wa kuzaliwa nao, anaotumia mtu kupambana na maisha yake ya kila siku. Kutumia mbinu, hekima, busara pamoja na elimu aipatayo kutokana na kusoma, kusikia na kutenda. Ni uzoefu kwa maana ya ustadi na tajiriba.

Ni dhahiri juhudi bila maarifa haiwezi kutoa matunda bora. Ni dhahiri shahiri maarifa bila juhudi haiwezi kuleta maendeleo. Ni dhahiri shahiri kupata matunda bora na maendeleo, kila mtu aelewe masharti ya maendeleo, afikiri kupata maarifa yatakayo mwezesha kutumia nguvu zake na za wenzake kujiletea maendeleo yao.

Serikali ya Awamu ya Tano nchini imeonyesha wazi kurejea tamko la Azimio la Arusha kuhusu maana na masharti ya maendeleo. Tafsiri yake kila mtu binafsi, jumuiya na taifa kufanya kazi kwa bidii na kutumia kaulimbiu ‘Hapa Kazi Tu.’

Azimio la Arusha lilibeba kaulimbiu ‘Uhuru na Kazi’ baadaye ‘Uhuru ni Kazi.’ Hii ina maana uhuru wetu hauna maana iwapo hatufanyi kazi. Ubora, uungwana na ustaarabu wa mtu, jumuiya au taifa ni kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Nchi zinazopewa sifa kuwa zimeendelea maana yake wananchi wanafanya kazi. Wanatumia uwezo walionao, elimu ya maarifa na kubuni mambo mapya, kujenga miundombinu ya uchumi, kutoa elimu bora na kuzingatia kanuni za afya bora.

Serikali inayoongozwa na Rais, Dk. John Magufuli tangu iingie madarakani imeonyesha dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo ya watu kuanzia vijijini hadi taifa kwa kujenga miundombinu ya nishati, maji, tiba, elimu, usafiri na usafirishaji na ujenzi wa viwanda, bila kusahau kilimo, uvuvi na ufugaji.

Wananchi lazima tufanye mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa na kufanya kazi. Kazi ni maendeleo. Kutofanya kazi, kuzembea na kupuuza wajibu, kutozingatia misingi ya elimu bora, kuzurura na kubwabwaja vijiweni na mitaani ni kutoa shahada kuzuia mtu asiwe na mali na maisha mazuri.

Nakumbusha na kuomba kila nafsi ya mwananchi ifanye mabadiliko ya kuacha uvivu na hiyana, na kuanza kuzungumza ukweli. Kutaka maendeleo na kupenda kufanya kazi. Mabadiliko yatakayoondoa shari, ufisadi na usaliti katika kuzuia maendeleo.

Please follow and like us:
Pin Share