Kujua ni mtihani. Majuto ni mjukuu kwa sababu kuna kutokujua. “Ningejua” huja baadaye. Ukijua huu, ule huujui, ukijua hiki, kile hukijui. Haitoshi kujua, lazima kujali. “Hakuna anayejali kiasi unachokijua, mpaka ajue kiasi unachojali,” alisema Theodore Roosevelt. Kujua ni mtihani. “Kujua unachokijua na ambacho hukijui, hiyo ndiyo elimu ya kweli,” alisema Conficius.

Kuna ambao wako katika ndoa wanasema: “Ndoa yangu ningejua.” Kuna ambao wapo katika wito fulani wanajiambia: “Ningejua.” Mungu anasema: “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.” (Hosea 4:6).  Unapojilinganisha na wengine bila kujua yaliyoko nyuma ya pazia unaweza kujuta bure.

Nimepokea ujumbe huu wa kwenye whatsApp: Mtu mmoja alikutana na mmoja wa wanadarasa wake baada ya miaka mingi na hakuamini macho yake. Alikuwa akiendesha toleo jipya la Mercedes Benz. Alirudi nyumbani akijisikia vibaya. Alifikiria kuwa alikuwa ameshindwa katika maisha. Jambo ambalo hakulijua ni kuwa mwanadarasa huyo alikuwa ni dereva na alikuwa ametumwa na bosi wake kwenye shughuli fulani. Alinyong’onyea kwa sababu ya kutokujua.

Ukweli huu unanikumbusha kisa ambacho nilikisia kwenye kanisa fulani ambapo mwanaume baada ya kuegesha gari kwenye maegesho ya kanisa alitoka na kwenda kumfungulia mlango wa gari mke wake upande wa kushoto. Wanandoa majirani wao waliona kila kilichotendeka. Mwanamke alianza kumgombeza mume wake kwa kutoiga walichokiona. Jambo ambalo hawakujua ni kuwa mlango wa gari ulikuwa umeharibika, ulikuwa unafunguliwa kwa nje. “Ukweli ni kuwa sote tunayakabili magumu ya namna fulani, na huwezi kujua magumu mtu anayoyapitia. Nyuma ya kila tabasamu kuna hadithi ya jitihada za mtu binafsi,” alisema Adrienne C. Moore.

Acha kujilinganisha na wengine, hujui yote. Ujumbe niliopokea unasema: “Acha kujiuliza kwa nini mimi? Rika langu wanaolewa. Rika langu wana watoto. Rika langu wana kazi nzuri. Rika langu wamefanikiwa. Rika langu wanaishi karibu na ufukwe. Rika langu wananunua magari mazuri ya starehe. Rika langu ni waheshimiwa kwenye jamii. Rika langu wamejenga nyumba za kifahari…Ni kweli lakini ni aibu, unasahau kuna rika lako wamezikwa. Kuna rika lako wako kwenye ‘koma’. Kuna rika lako wana matatizo ya figo damu inasafishwa na mashini. Kuna wanarika lako wako kwenye vituo vya walemavu wa akili. Kuna wanarika wako wanaolala barabarani. Kuna wanarika wako ambao ni yatima. Kuna wanarika wako ambao hawajaajiriwa.” Kujua ni kinga ya majuto. Ungejua ukweli huo usingejuta.

Kuna methali ya Afrika isemayo: “Wajuanao hawagombani”. Mtu anayekujua vizuri ukigombana naye ataanika mambo yako yote hadharani. Ni msamaha na uelewa vinaweza kuanua yaliyoanikwa. Ukimjua utampenda. “Watu wengi wanaamini kuwa ni upendo unaokua, lakini ni kujua kunakokua na upendo unapanuka kuweza kubeba kujua huko,” alisema Paul Young. Ukimjua jirani utampenda. Ukimjua mwenzi wa ndoa utampenda.

Jua unalolitaka. Jua wito unaoutaka. “Karama zako na mahitaji ya dunia vinapokutana ndipo ulipo wito wako,” alisema mwanafalsafa Aristotle.  Ni muhimu kujua vipaji vyako. Moyo ulipolalia ndipo miguu huelekea. Pale moyo wako unapolalia ndicho kipaji chako.  “Kumbuka ndoto zako na zipiganie. Lazima ujue unalolitaka katika maisha. Kuna jambo moja ambalo linafanya ndoto zisiwezekane, nalo ni hofu ya kushindwa,” alisema Paulo Coelho. Furaha ya kushinda inazidi hofu ya kushindwa.

Kujua kunahitaji kujifunza. “Ambaye anajifunza lakini hafikiri, amepotea! Ambaye anafikiri lakini hajifunzi yupo katika hatari kubwa,” alisema Confucius. Fikiria na tenda. “Kama unafikiri kwa msingi wa mwaka mmoja panda mbegu; kwa msingi wa miaka kumi panda miti; kwa misingi ya miaka 100 wafundishe watu,” alisema Conficius. Ili watu wasiangamizwe kwa kukosa maarifa, watu wanahitaji kufundishwa. “Kuna mbinu tatu za kuwa na hekima. Ya kwanza ni kutafakari, ambayo ni mbinu ya juu sana. Ya pili ni mbinu ya kuiga ambayo ni rahisi. Ya tatu ni uzoefu ambayo ni kali sana (chungu sana),” alisema Conficius. Kusema kweli kujua ni kinga ya majuto.

Please follow and like us:
Pin Share