Mwandishi T. L. Osbon anasema: “Ukiacha kujifunza unaanza kufa.” Tafuta wazo jipya kila siku. Kumbuka usipotumia nguvu nyingi kuwaza mawazo yatakayoibadili dunia ni lazima utaajiriwa na watu waliotumia nguvu nyingi kuwaza mawazo yaliyoibadili dunia. Mwandishi wa vitabu vya kiroho, Tony  Evans anasema: “Watu wengi wanatumia muda wao mwingi kuishi maisha ya watu wengine.’’

Simamia ndoto yako. Huko Marekani msichana wa Kiprotestanti aligeuka na  kuwa Mkatoliki na kujiunga na shirika la watawa kinyume cha matarajio ya familia yake. Baba yake mzazi alimwandikia, na sehemu ya barua yake ilisomeka: “Nitakuachia dola milioni 12 kwa sharti kwamba utauacha utawa na kutoka konventini.” Msichana huyu aliyekuwa amekubali kumfuata Yesu Kristo kwa mtindo wa maisha ya wakfu alimjibu baba yake kupitia barua, sehemu ya  barua ya  msichana huyu kwenda kwa baba yake ilisomeka: “Baba nilijiandaa kuwa mtawa. Utajiri ulionao naomba uwasaidie watu wasiojiweza. Baba yangu wa mbinguni ni tajiri zaidi ya baba yangu wa duniani.” Msichana huyu alibaki konventini na kuwa mtawa. Maisha ya msichana huyu yanatufundisha umuhimu wa kusimamia ndoto zetu.

Mafanikio ni nchi ya juhudi. Kibali cha kuishi katika nchi hii ya ‘juhudi’ ni kukubali kuwa mwana-juhudi. Vaa sura juhudi. Vaa viatu vya juhudi. Tembea kwa juhudi. Ona kwa juhudi. Ota kwa juhudi. Fikiria kwa juhudi. Samehe kwa juhudi. Penda kwa juhudi. Sali kwa juhudi. Mwanaharakati wa haki za binadamu wa Marekani, Malcom X anasema: “Kila unapomuona mtu mwenye mafanikio kuliko wewe, ujue anafanya vitu ambavyo wewe hufanyi.” Siri ya utajiri ni mawazo ya mtu. Maisha unayoishi uliyataka mwenyewe. Amka uishi. Hii ndiyo siri kubwa ya utajiri kuliko zote ulimwenguni. Ukifikiria chanya maisha yako yatakuwa chanya, ukifikiria hasi maisha yako yatakuwa hasi. Unachofikiria ndicho kitakachokuwa. Siri ya mafanikio yako ni jumla ya mambo unayoyawaza. Leo anza kuwaza vizuri.

Aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Wiston Churchill, alipata kutoa nasaha hii: “Mafanikio siyo ajali. Ni kujifunza, kujituma, kujitoa mhanga na kikubwa kuliko vyote ni kupenda unachokifanya.”  Mafanikio yapo. Hayawabagui watu. Wakati mwingine watu hujibagua wenyewe wasifanikiwe. Wanafanya hivyo kwa kujua au kwa kutokujua. Aliye na nia ya dhati ya kufanikiwa na anajua kuwa ana nia ya kufanikiwa atafanikiwa. Mwenyezi Mungu anataka tufanikiwe. Hataki tuwe maskini na ombaomba. Tazama shauku ya Mungu juu ya mafanikio yetu. “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.’’ [3Yoh 1:2]. Mungu anataka tufanikiwe katika mambo yote yaliyo ya halali. Anataka tufanikiwe katika mipango yetu yote iliyo ya halali.

Amka uishi. Amka ufanikiwe. Kuna mtu mmoja alisema hivi: “Kufika hapa nilipofika leo nilijitolea vitu vingi na mambo mengi katika maisha yangu. Niliishi katika uhamisho wa kijamii kwa ajili ya mafanikio. Nilijitolea muda. Nilijitolea usingizi. Nilijitolea starehe. Wakati wengine wakienda baa mimi nilikuwa kazini. Wakati wengine wamelala, mimi nilikuwa macho nikifanya kazi. Wakati wengine wakiangalia vipindi pendwa vya televisheni, mimi nilikuwa nikiangalia vipindi visivyopendeka vya televisheni. Wakati wengine wana muda wa kuchezea, mimi nilikuwa nikiyaendesha maisha yangu kwa ratiba maalumu.”

Usishibe mafanikio ya mtu mwingine. Usiwe mpambe wa mafanikio ya watu wengine. Tafuta mafanikio yako. Hakuna mtu anayeweza kula na kushiba kwa niaba ya mtu mwingine bali mtu anaweza kuandaa chakula kwa nia ya kumsaidia mwingine. Mwandishi Enock Maregesi anasema: “Mafanikio unapaswa kuyataka kama unavyotaka hewa. Hewa ni kitu cha muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote kile ulimwenguni. Ukipewa hewa au shilingi bilioni kumi, chagua hewa.”

Jiandae kuzaliwa mbinguni.

Please follow and like us:
Pin Share