Mgogoro umeibuka kuhusiana na kiwanja kwenye Kitalu Na. 52, Block 27 katika Mtaa wa Somali, Kariakoo, ambako jengo lenye zaidi ya ghorofa 10 linajengwa. Inadaiwa kuwa mmiliki wa sasa anayejenga jengo hilo alinunua nyumba ambayo ilidhulumiwa kutoka kwa ndugu wa mjane aliyeachiwa kiwanja hicho na mume wake.

Jengo lenye zaidi ya ghorofa kumi linalojengwa katika kiwanja ambacho baadhi ya watu wanadai kudhulumiwa katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Jitihada za ndugu hao kufuatilia suala hilo katika sehemu mbalimbali ikiwemo mahakamani zimegonga mwamba.

Taarifa zilizolifikia JAMHURI zinabainisha kuwa ingawa eneo hilo limeshauzwa mara mbili baada ya wamiliki halali kupokwa umiliki kwa njia za hila, hakuna kodi yoyote iliyolipwa kwa mamlaka za serikali kutokana na mauzo hayo.

Chanzo cha mgogoro huo kinatajwa kuwa watu walioshirikiana na baadhi ya watumishi wa serikali wasio waaminifu kupindisha sheria na kutoa vibali feki ili kuhalalisha nyumba ya urithi iliyokuwa katika kiwanja hicho kuuzwa.

Nyumba hiyo Na. 47 ilijengwa na Abdallah Makawa, mume wa Fatuma Selemani Kombo, ambaye aliirithi baada ya mume wake huyo aliyekuwa mfanyabiashara kufariki dunia. Lakini mama huyo naye alifariki dunia Februari 19, mwaka 2005 na kuiacha nyumba hiyo mikononi mwa mdogo wake, Amina Kalimanzira, mkazi wa Temeke, Dar es Salaam kama msimamizi halali wa mirathi aliyethibitishwa kwa vikao vya ukoo pamoja na mahakama.

Hata hivyo, tangu mwaka 1991 nyumba hiyo imekuwa kwenye mgogoro wa mirathi baina ya ndugu na watu waliojipachika undugu bandia na familia ya aliyekuwa mume wa Fatuma, Abdallah Makawa, aliyefariki dunia Mei 13, 1989.

Fatuma alipofariki dunia nyumba hiyo iliachwa chini ya mdogo wake kwa sababu wenza wawili hao hawakujaliwa kupata mtoto.

Akizungumzia sakata la kutapeliwa nyumba hiyo, Amina Kalimanzira anasema baada ya kifo cha Abdalla Makawa alijitokeza mtu aliyefahamika kwa jina la Yahaya Juma na kufungua shauri la mirathi ya nyumba hiyo.

Shauri hilo Na. 84/1991 lilifunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo ambapo Yahaya aliomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi.

Kwa mujibu wa Amina, taarifa hizo zilimfikia mke wa marehemu Abdalla Makawa, Fatuma, hali iliyolazimu naye kukata rufaa Na. 19/1992 katika Mahakama ya Wilaya Ilala, akipinga shauri hilo.

Amina anaeleza kuwa mahakama ya Wilaya ya Ilala ilijiridhisha na ushahidi wa Fatuma Kombo wa kupinga ombi la mirathi la Yahaya Juma hivyo kumpa ushindi.

“Tangu kipindi hicho marehemu dada yangu (Fatuma Kombo) alikuwa mmiliki halali wa nyumba Na. 47, aliendelea kuishi humo mpaka alipofariki dunia mwaka 2005,” anasema Amina.

Anasema enzi za uhai wake, Abdalla Makawa alikuwa mwalimu wa madrasa na kwamba wahusika wa utapeli huo ni kati ya watu waliowahi kufundishwa naye.

“Mzee Makawa aliacha wosia, aliandika kwamba mke wake ndiye mrithi wa nyumba,” anasema na kuongeza kuwa wosia huo ulitumika kama kielelezo mahakamani na kumpa ushindi Fatuma Kombo dhidi ya mipango ya kitapeli iliyokuwa imepangwa.

Aidha, anasimulia kuwa mwaka 2003 alijitokeza mtu mwingine akifahamika kwa jina la Bakari Kauchimbe na kufungua  shauri la mirathi Na. 112/2003 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kauchimbe alifungua shauri hilo akieleza kuwa anaomba mahakama imruhusu kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu kaka yake, Abdalla Makawa.

Anadai Kauchimbe aliidanganya mahakama kwa kuwasilisha nakala ya cheti kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kikionyesha kwamba Abdalla Makawa alifariki dunia mwaka 1987 wakati si kweli.

Anabainisha kuwa wakati shauri hilo linafunguliwa Fatuma Kombo alikuwa mgonjwa wa kulala kitandani hali iliyomlazimu kutoa nguvu ya kisheria (Power of Attorney) kwa Amina.

Aidha, Amina anasema baada ya kupewa nguvu hiyo alianza kufanya hatua za kufungua kesi ya kupinga shauri Na. 112/2003 lakini akiwa katika hatua hizo alipata taarifa ya kufunguliwa kwa kesi nyingine ya mirathi Na. 50/2005 katika Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo.

Anaeleza kwa mujibu wa nyaraka za mahakamani, mirathi Na. 50/2005 ilifunguliwa na mtu aliyejitaja kama Abbas Manyasi, wakati mtu huyo huyo anatambulika kwa jina la Afaki Juma.

Anasema Abbas Manyasi alijitambulisha kuwa ni ndugu wa Yahaya Juma aliyekuwa amefungua mirathi ya kwanza Na. 84/1991 katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo.

 “Baada ya kuona hali hiyo, nilifungua jalada Na. 14/2005 katika Mahakama ya Wilaya Ilala nikiomba uamuzi wa hukumu ya Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo iliyokuwa imemteua Abbas Manyasi itenguliwe. Tumeifuatilia kesi hiyo lakini tunaambiwa kuwa faili lake halionekani,” anaeleza Amina.

Aidha, anasema mwaka 2006 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitoa amri majalada yote kuhusiana na mirathi hiyo yafikishwe mahakamani hapo na yaliunganishwa na kuifanya nyumba hiyo kuwa na watu watatu wanaodai kuteuliwa kuwa wasimamizi wake.

“Baada ya shauri letu kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hakimu aliagiza majalada yote yaunganishwe, yaani jalada la mirathi Na. 19/1992, namba 112/2003 na namba 50/2005,” anaeleza.

Hata hivyo, anasema tangu majalada hayo yameunganishwa wameyafuatilia bila kupata majibu na badala yake mwaka 2009 hakimu aliwaeleza kupeleka shauri lao katika Ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

“Ingawa tulifuata ushauri wa hakimu na kulifikisha suala letu huko tume, lakini hadi leo hatujapatiwa majibu yoyote ya malalamiko yetu,” anasema.

Amina anaongeza kuwa mwaka 2011 alijitokeza mtu mwingine akijitambulisha kwa majina ya Rajabu Bakari Mnhonya, naye akidai apewe usimamizi wa mirathi wa nyumba hiyo.

Anadai Rajabu Mnhonya alikwenda Mahakama ya Mwanzo Kariakoo ambako alipatiwa usimamizi wa mirathi kupitia kesi namba 50/2005 iliyokuwa imefunguliwa awali na msimamizi wa awali, Abbas Manyasi.

Amina anaeleza kuwa Rajabu Mnhonya aliieleza Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kwamba Abbas Manyasi amefariki dunia.

“Lakini hakuwa na hati ya kifo cha Abbas Manyasi wala muhtasari wa kikao cha familia uliompendekeza yeye kuwa msimamizi wa mirathi,” anasimulia.

Amina anasema baada ya Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kumkubalia Mnhonya asimamie mirathi ya Abbas Manyasi, Mnhonya alishirikiana na watumishi wa Wizara ya Ardhi kupata hati ya Kitalu Na. 52 na kuiuza nyumba hiyo kwa Sh milioni 400 kwa Yusufu Matimbwa, ambaye mara baada ya kuinunua aliamua kuivunja bila kibali cha mamlaka yoyote wala kutoa notisi ya kuwaondoa waliokuwamo.

“Walituvunjia nyumba wakaacha vyumba viwili tu, mimi nilikuwa naishi humo mvua ikawa inaninyeshea.

Kipindi hicho tulikuwa na ndugu yetu mgonjwa alifariki dunia kwa mshituko wa moyo baada ya nyumba kuvunjwa,” anasema Amina.

Anasema amewahi kuwekwa rumande kwa siku tatu kwa tuhuma za kutunga kwamba anatishia kumdhuru Matimbwa.

Pia, anabainisha kuwa kwa takriban wiki mbili baada ya nyumba kuuzwa, Matimbwa akishirikiana na Mnhonya walimteka na kumfikisha eneo la Posta jijini Dar es Salaam kwenye jengo la Shirika la Nyumba (NHC), plot. Na. 717/11 Mtaa wa Jamhuri ambako walimwingiza kwenye ofisi ya uwakili iliyoko ghorofa ya pili katika jengo hilo.

Anasimulia kuwa akiwa ndani ya ofisi ya JURIS CONSULTANT Law Chambers walimlazimisha kuweka saini kwenye mkataba ambao hakusoma huku wakimpiga picha.

Akiwa humo anasema kulikuwa na wanaume zaidi ya watano na baadhi yao walikuwa wameshikilia bastola ambavyo baada ya kumsainisha walimkabidhi hundi ya Sh milioni 50.

“Walinisainisha mkataba ambao sikuutambua, wakanipiga picha wakati nasaini, baada ya hapo wakanipeleka Manispaa ya Temeke kwa gari lao hadi kwenye Benki ya NMB Tawi la Temeke. Tulivyofika kwenye benki hiyo walinifungulia akaunti Na. 2071624151 kwa jina la Amina Bakari, zikaingizwa hela hizo, walivyomaliza tu, Matimbwa akaniambia amenipiga bao la kisigino akaondoka,” anasimulia Amina.

Hata hivyo, anaeleza kuwa mara baada ya michakato hiyo ya utapeli kumalizika Matimbwa aliiuza nyumba hiyo tena kwa Sh milioni 200 kwa mfanyabiashara Christopher Letson Mgalla.

JAMHURI limefika katika ofisi hizo za uwakili na kuelezwa kuwa mwanasheria aliyeshuhudia wakati Amina anasainishwa makubalino hayo anaitwa Mbuga Jonathan, ambaye kwa sasa hayupo tena chini ya ofisi hiyo.

Aidha, JAMHURI limefanikiwa kuonana na Mbuga akiwa ofisini kwake ghorofa ya nne katika Hoteli ya Golden Tulip na akakiri kuwa saini iliyopo kwenye makubaliano hayo ni yake.

Hata hivyo, amegoma kutoa ufafanuzi wa upungufu kwenye makubalino hayo akitaka aonyeshwe hati halali ya makubaliano.

“Siwezi kuongea chochote, hii sahihi ndiyo ni yangu, lakini siwezi kusaini bila kuandika maneno ya kisheria. Nakumbuka kuna mahali niliandika neno, ‘certicified by’, hilo neno kwenye hizi nakala halipo, ukija na orijino mimi nitazungumza na wewe bila shida,” anasema Mbuga.

Hussein Likalama, mjukuu wa Amina, anaeleza kuwa mauziano yote yaliyofanywa katika eneo hilo yamefanyika kihuni na kwamba shughuli za ujenzi zinazoendelea katika eneo hilo zimejaa udanganyifu kwani hakuna kibali halali cha ujenzi.

JAMHURI limefika kwenye ofisi za wahandisi wa Jiji wanaohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi na ukaguzi uliofanywa na Mhandisi Mkuu Idara ya Ukaguzi na Vibali, Jastine Magoda, umebaini kuwa kibali kilichotolewa katika kiwanja hicho ni cha jengo lenye ghorofa sita.

Lakini hivi sasa jengo hilo linaloendelea kujengwa lina urefu wa zaidi ya ghorofa kumi na Magoda alieleza kuwa Januari mwaka jana Mgalla aliomba kibali kingine cha kuongezea jengo.

Gazeti la JAMHURI limeomba kuona nakala ya kibali kipya kinachomruhusu Mgalla kuendeleza ujenzi kutoka kwenye ofisi hizo lakini halikufanikiwa.

“Kama mnataka kupata nakala ya kibali alichoomba mwaka jana andikeni barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa, mimi nitawapa sina shida,” anaeleza Magoda.

JAMHURI limewatafuta Yusufu Matimbwa, Christopher Mgalla na Rajab Mnhonya bila mafanikio.

Matimbwa amepigiwa simu mara kadhaa bila simu yake kupokewa. JAMHURI lilifika ofisini kwake Mtaa wa Sudan, Manispaa ya Temeke lakini halikufanikiwa kuonana naye. Kila mara mwandishi alipofika aliambiwa yupo nje ya ofisi.

JAMHURI pia lilimfuata Christopher Mgalla hadi eneo linapojengwa ghorofa lake na kuelezwa kuwa yuko nje ya nchi. Hata hivyo, mtu mmoja alilidokeza gazeti hili kuwa Mgalla yuko Tunduma, mkoani Songwe.

By Jamhuri