Wafanya-biashara 370 katika Soko la Machinga Complex jijini Dar es Salaam wamebaki katika hali ya sintofahamu baada ya mamilioni ya fedha waliyochanga na kufungua akaunti katika Benki ya Equity Tawi la Kariakoo ili waweze kupata mikopo kushindwa kuwasaidia.

Wafanyabiashara hao walijiunga katika mfuko ujulikanao kama Gulio Expo Machinga Guarantee Fund, baada ya kushauriwa kufanya hivyo na benki hiyo. Walifanikiwa kcuhangishana Sh milioni 16 na kufungua akaunti kwa ahadi kuwa hiyo itakuwa dhamana ya wao kupata mikopo.

Lakini kwa takriban miaka minane sasa, wengi wa wafanyabiashara hao hawajapata mikopo hiyo huku benki ikiwakana kila wanapokwenda kuulizia.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa wafanyabiashara hao wamezungukwa na wenzao wachache waliowachagua kama viongozi wao na waweka saini katika akaunti hiyo.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa benki na baadhi ya viongozi hao zinaonyesha kuwa wakati kundi kubwa la wafanyabiashara wakiwa hawajui kinachoendela, baadhi yao, hasa wale viongozi, wamekuwa wakipata mikopo kutoka benki hiyo na kuendesha shughuli zao.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, katibu wa kamati ya ufuatiliaji wa mfuko huo, Gasper Charles, amedai kuwa awali kabla ya kujiunga kama kikundi walikuwa wakifanya biashara kiholela ndipo walipokuja maofisa wa Benki ya Equity Tawi la Kariakoo na kuwashauri kuunda kikundi ili wapate mikopo kwa urahisi.

Charles anasema walianzisha kikundi hicho mwaka 2012 na kuwachagua baadhi yao kuwa viongozi na waweka saini kwenye akaunti yao, huku kila mwanachama akitakiwa kuchanga Sh 50,000.

“Nilishiriki kuwashawishi wenzangu tuunde mfuko huu na kufungua akaunti kwa sababu wakati ule wengi wetu tulikuwa hatuna uwezo wa kimtaji kuendesha shughuli zetu kwa ufanisi, hivyo hii ilikuwa njia ya kupata mitaji mikubwa,” anasema katika mahojiano na JAMHURI.

Hata hivyo, anasema tangu wakati huo wanachama wengi hawajapatiwa mikopo kama walivyoahidiwa na jitihada zao za kufuatilia fedha zao zimegonga mwamba.

“Tulipoiandikia benki kuomba kurudishiwa fedha zetu, ikatukana ikisema haitufahamu. Sasa tunaiomba serikali itusaidie tupate fedha zetu ili zitusaidie katika biashara zetu,” analalamika Charles na kuongeza:

“Tumechoka kusumbuliwa na kupewa majibu yasiyoridhisha na uongozi wa benki hiyo.”

Akisimulia hatua nyingine walizochukua anasema Januari 31, mwaka huu walimwandikia Katibu Mkuu Wizara ya Afya, ambako ndiko walisajili mfuko wao, wakiiomba ofisi hiyo iwasaidie kutatua tatizo lao.

Lakini alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake, Meneja wa Equity Tawi la Kariakoo, Alex Ndondole, alikiri wafanyabiashara hao kufungua akaunti katika benki hiyo chini ya umoja wao.

Hata hivyo, anasema akaunti hiyo inaonyesha kuwa inamilikiwa na kikundi cha watu wanne tu; Dimo Dibwe, Fred Kimiti, Kisa Mwakyusa na Brian Kikoti ambao kwa pamoja ndio watia saini wa akaunti hiyo.

“Hawa ndio watu tunaowafahamu kupitia akaunti hiyo na ndiyo maana hao wafanyabiashara wengine hatuwezi kuwapatia taarifa kuhusu akaunti ambayo haiwahusu, sheria zinatukataza kutoa taarifa za akaunti kwa mtu asiyehusika,” anafafanua.

Anasema taarifa kwamba benki hiyo imechukua pesa hizo, si kweli kabisa, kwa sababu wanakikundi ambao wamekidhi vigezo wamekuwa wakipatiwa mikopo na kurejesha.

“Mkataba baina ya benki na kikundi hicho ulikamilika mwaka 2015 na hadi wakati huo tayari tulishatoa mikopo kwa kukindi hicho na wote waliokuwa wamekopa walisharejesha mikopo yao,” anasema na kuongeza:

“Ni kweli baadhi ya wafanyabiashara wanatuandikia barua kutaka kujua taarifa za akunti hiyo lakini kama nilivyoeleza hatuwezi kuwapatia kwa sababu wao haiwahusu.”

Amewashauri wafanyabiashara hao kwenda kuzungumza na hao watu wanne ambao ndio benki inawatambua kama wamiliki wa akaunti hiyo.

Alipozungumza na JAMHURI, Dimo Dibwe, amekiri kuwa yeye ni mmoja wa watu wanne wanaomiliki akaunti hiyo.

Anasema wao ndio waliokuja na wazo jipya la kuanzisha kikundi baada ya kuona wamefeli katika kazi walizopewa na serikali za kuboresha soko hilo kwa njia ya matangazo.

“Chini ya mpango huu sisi wanne tulikuwa kama wadhamini tu. Tulipowahamasisha wenzetu wengi walikubali kwa hiari yao na kujiunga. Sisi tukawasiliana na benki na kuingia nayo mkataba ili itupatie mikopo,” anasema.

Dibwe anadai kuwa benki hiyo iliweka masharti ambayo wale walioweza kuyatimiza walipatiwa mikopo kama walivyoahidiwa lakini kuna baadhi yao ambao walitoa taarifa za uongo, hivyo benki ikasita kuwapatia mikopo.

“Bado tunaendelea vizuri na wale waliokidhi vigezo, watu wanaendelea kupata mikopo,” anasema.

1422 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!