Na Georgina Misama, Maelezo

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi amesema Bwawa la Umeme Julius Nyerere (JNHPP) halikusababisha mafuriko yanayoendela katika wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani na badala yake bwawa hilo limesaidia kupunguza muda ambao mafuriko hayo yangetokea kwa kukusanya maji.

Matinyi amesema hayo leo Aprili 12, 2024 wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo alieleza kwamba mafuriko hayo yamesababishwa na mvua za El Nino ambazo zilianza mwezi Oktoba mwaka jana 2023 na kuungana na mvua za msimu wa masika mwaka huu 2024, hivyo kusababisha maji kuwa mengi kuliko msimu wa masika wa kawaida na kwamba hali hii ilitabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na taarifa hizo zilitolewa kwa wananchi ili wachukue tahadhari.

“Kwa kuzingatia kuwa bwawa hili lilijengwa ili lipunguze mafuriko, mara baada ya kuanza kukusanya maji mnamo Desemba 2022, uwezekano wa mafuriko ulipungua hadi hivi sasa wakati wa mvua za El Nino ambapo kiasi cha maji kimekuwa kikubwa mno. Licha ya kwamba kulikuwa na hatua ya lazima ya kuyafungulia maji ili kuzuia bwawa lisiharibike, lakini ni hakika kwamba maafa ya mafuriko yalikuwa yamezuiwa yasiwe makubwa zaidi ya ilivyo sasa,” alisema Bw. Matinyi.

Alisema kwamba maji yanayopita katika mto Rufiji yalifikia wingi wa mita za ujazo 8 ,445 kwa sekunde mwezi Februari 2024, na kuendelea kwa wastani wa mita za ujazo zaidi ya 6500 kwa sekunde, lakini Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekuwa likiachia kiwango cha chini kati ya mita za ujazo 3,000 na mara chache hadi 6 ,OOO kwa sekunde kwa siku tofauti za mwezi Machi na Aprili 2024.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia kamati ya maafa katika kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo Bw. Matinyi alisema viongozi mbalimbali walitembelea maeneo yaliyoathirika ikiwemo wilaya za Rufiji na Kibiti mkoa wa Pwani pamoja na Mlimba wilaya Kilombero mkoa wa Morogoro ambapo walijionea hali halisi na kutoa maelekezo katika huduma muhimu na tayari dawa za tiba kwa binadamu na za tiba ya maji, huduma za afya, chakula, malazi, uokozi, usalama na ushauri nasaha vimeanza kuwafikia wananchi. Aidha, askari wa wanyama pori wamepelekwa kwenye maeneo yote ili kudhibiti wanyama aina ya mamba.

“Kwa maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, timu ya mawaziri na manaibu mawaziri kumi na makatibu wakuu wao, ilifanya ziara kwenye maeneo yalioathirika mnamo tarehe 10 na 11 Aprili ikiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama ambao mbali ya kutoa salamu za pole za Mhe, Rais viongozi hao pia walitoa ahadi za misaada ya serikali na kuagiza miundombinu iliyoharibika ifanyiwe kazi,” alisema Bw. Matinyi.

Kwa upande wa madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo, Bw. Matinyi alisema mpaka sasa mkoani Pwani kuna vifo vitano (Rufiji 2, Kibiti 2 na Kisarawe 1) majeruhi 2 Kibiti na 3 Kisaware lakini pia kuna uharibifu wa mashamba ya mazao yakiwemo mahindi, mpunga, ndizi, ufuta, mihogo, matama na pamba vilevile makaazi, miundombinu ya barabara, madaraja, nguzo za umeme, shule, kituo cha afya cha Muhoro kusombwa na maji, jumla watu 126,831 wameathirika mkoani Pwani: 88,768 (Rufiji), 36,900 (Kibiti) na 1,163 (Kisarawe). Hekta za mashamba zilizoathirika ni 33930.24 (Rufiji), 71,366 (Kibiti) na 167 (Kisarawe), hadi sasa Watu 1,014 wameokolewa wilayani Rufiji.

“Mkoani Morogoro zimesababisha vifo 28 katika halmashauri 8 na kubomoa nyumba 1 ,035 zingine 6,874 kuzingirwa na maji. Vifo hivi ni tofauti na vile vilivyoripotiwa na Polisi, vilevile ekari 34,970 za mazao mbalimbali yakijumuisha mahindi, mpunga, ufuta, pamba na mazao mchanganyiko zimeathirika ikiwa ni pamoja na mifugo 1 ,466 imeathirika. Miundombinu ya reli, barabara, makalvati na madaraja imeharibika katika halmashauri za Malinyi, Mlimba, Ifaraka Mji, Ulanga na manispaa ya Morogoro imeharibika.

Please follow and like us:
Pin Share