Mauaji ya koromeo tishio Kagera

Kwa muda wa mwezi mmoja sasa nipo hapa mkoani Kagera. Nazunguka katika wilaya mbalimbali kuangalia maendeleo ya Mkoa wa Kagera.
 Nimepata fursa ya kufika Kayanga Karagwe, nimeishia kupata mshangao. Nimeshangaa kwani Kayanga niliyoiacha ikiwa na majengo mawili mwaka 2001; Tindamanyile na KDCU, leo ina mpaka vituo vya mafuta na hoteli za kisasa.


Kabla sijaendelea na makala hii, nitoe salamu za pole kwa wanahabari wenzangu, familia na Watanzania kwa ujumla kwa kumpoteza mwanahabari mahiri aliyekuwa akiibukia kwa kasi, ndugu yangu, kijana wangu; Edison Kamukara. Nimepokea msiba huu kwa masikitiko makubwa. Nimeshtuka na nimezidi kupata ushuhuda kuwa wanadamu tuko sawa na maua. Tunaweza kunyauka muda na wakati wowote. Nimeumia kuona Kamukara anatutoka katika umri mdogo hivi. Mungu amweke Mahala Pema Peponi.
Nikirejea katika makala yangu, wakazi wa Mkoa wa Kagera wamejikomboa. Ukiacha  ya ‘koromeo’ nitakayoeleza hapa chini, maisha yamezidi kuwa bora. Nyumba za nyasi katika vijiji vingi ni historia. Wapo watoto waliozaliwa hawazifahamu kabisa nyumba za kitamaduni za msonge, ambazo hadi mwaka 2000 zilikuwa kwenye kila kijiji. Leo hata nyumba zilizoezekwa kwa nyasi zinahesabika. Familia nyingi zimesakafia nyumba zao na maeneo mengi umeme umefika.


Barabara nazo si haba. Zamani ilikuwa kama una safari ya kwenda Ngara, Karagwe au Biharamulo, unajiandaa wiki nzima. Mkifika eneo la Kasindaga kama mnakwenda Biharamulo, bila kujali kuwa umelipa nauli, mkikwama mnatolewa nje ya gari kusukuma, huku simba na mbung’o wakiwapumulia pembeni. Sitaki kukumbuka enzi hizo za miaka ya 1978, ambapo wakati mwingine ilituchukua hadi siku mbili safari ya Bukoba Biharamulo.
Sitanii, leo ninachozungumza hali ni tofauti. Safari ya Biharamulo-Bukoba baada ya kutengenezwa lami ni saa 2 tu. Karagwe kulikuwa na mlima unaoitwa Gakorongo, huu ndiyo ilibidi kama unakwenda Karagwe uandike wosia kwanza. Hakuna gari lilokuwa na uhakika wa kuupandisha. Leo mlima ule umekatwa na kama halitaharibika jambo, barabara ile nilivyoishuhudia itageuka kivutio cha utalii badala ya hatari dhahiri kwa maisha ya binadamu ilivyokuwa.


Kwa mshangao, hivi sasa nakwenda Karagwe na kurudi Bukoba siku hiyo hiyo. Wiki iliyopita nilikuwa Kayanga Karagwe hadi saa 3:00 usiku, nikapata hofu kuwa huenda sitapata usafiri, wenyeji wangu wakaniambia hadi saa 5:00 usiku usafiri upo. Na kweli, nilipata usafiri saa 3:15 ilipofika saa 4:30 niliishafika Bukoba. Hakika katika eneo la miundombinu Kagera imepata ukombozi wa kweli chini ya uongozi wa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kwa Mkoa wa Kagera, zao kuu la biashara ni kahawa. Kahawa imepoteza mwelekeo. Katika soko la dunia, bei inapanda lakini si kwa kulingana na uhalisia, na kiukweli mtu atakuwa sahihi kusema enzi ambazo kilo moja ya kahawa ilikuwa inauzwa Sh 20, fedha hii ilikuwa na thamani kuliko sasa inapouzwa Sh 1,300. Hapa miaka ya 1990 hadi 2000 familia nyingi zilikata tamaa ya kuishi.


Ukiacha kahawa, uchumi wa Mkoa wa Kagera kwa kiasi kikubwa ulitegemea uvuvi. Uvuvi nao kitumbua kikaingia mchanga. Baada ya minofu ya samaki kuanza kuuzwa Ulaya wakazi wa Kagera wakaishia kula mapanki, ikawapo hatari ya wazi kuwa watoto wangeweza kupata utapiamlo. Samaki waliokuwa kitoweo cha uhakika wakageuka bidhaa adhimu.
Chakula cha msingi – ndizi, nazo zikakumbwa na dhoruba. Mnyauko ukachukua nafasi, familia nyingi zikakumbwa na janga la njaa. Hapa lilikuwapo tishio la wazi katika miaka hiyo niliyoitaja kuwa Mkoa wa Kagera ungeweza kudidimia zaidi na kutopea kwenye umaskini. Hata hivyo, Mungu si Athumani na wala hanywi chai ya rangi.


Sitanii, kidogo mambo yakabadilika. Upande wa chakula ikaletwa mbegu ya migomba iitwayo Mtwishe na nyingine kwa jina la Fia. Hakika mbegu hizi zimewafuta machozi wakazi wa Kagera. Ingawa ladha ya ndizi zake huwezi kuilinganisha na ‘nshansha, nshakala, njubo, entobe, enyoya au enkonjwa ya gani,’ lakini hakuna anayeweza kufa njaa.
 Familia nyingi kwa sasa hawali mihogo. Fia moja hawakati kutoka kwenye mgomba. Wanatumia ngazi kukwanyua ndizi, vinginevyo kwa ukubwa wa mkungu wake ukiikata na kuiweka chini zitageuka mbivu kabla hujala hata nusu ya mkungu. Kwa upande wa chakula naweza kusema kuwa Kagera sasa kuna nafuu kuliko ilivyokuwa miaka hiyo niliyoitaja.


  Kiuchumi, nako si haba. Ukiangalia wakazi wa mkoa huu wameamua kuwaiga wenzao wa Iringa. Wameamua kupanda miti aina ya pine na mikalatusi (ekinyaibabi). Maeneo mengi ya milima yaliyokuwa wazi enzi hizo, kwa sasa yamefunikwa na miti. Miti imekuwa mkombozi kwa wakazi wa mkoa huu. Wanakata mbao, wanauza na kujipatia pato la uhakika.
 Yapo mazao mengine kama maharage, mahindi na pamba kwa baadhi ya maeneo, na mazao mengine ya chakula ambayo nayo yanawaingizia pato wenyeji wa mkoa huu. Pia tusilionee aibu, badala yake tutafute jinsi ya kuliendeleza zao la ‘konyagi’ kwa mikoa mingine inaitwa gongo, lakini wakubwa wengi wa nchi hii wamesomeshwa na gongo nikiwamo mimi.
Kama Uganda wamefika mahala wakaiendeleza gongo yao kwa kuifunga kwenye chupa na viroba ikawa na viwango na sasa inaitwa Waragi, inakuwaje sisi tushindwe kuweka utaratibu kama Serikali kuangalia jinsi ya kuendeleza gongo hii ikatusaidia kama Scotland ambapo karibu kila familia inatengeneza whisky? Kwao nao hiyo ndiyo gongo yao, ila Serikali imetunga sheria inayoweka viwango na kila Mskochi anaitengeneza kwa kufuata viwango. Hata sisi tukiamua tunaweza gongo ikapata heshima.


Sitanii, nimelazimika kugusia maendeleo ya Mkoa wa Kagera kwa nia ya kukuleta kwenye picha wewe msomaji ukapata mwanga juu ya maisha ya mkoa huu. Watu hawa waliopigwa na Vita ya Kagera 1978/79, kisha baada ya vita likaja janga la Ukimwi ambalo wamepambana nalo kwa ujasiri mkubwa na kulififisha kwa sasa, si mkoa unaoongoza kwa Ukimwi kwani Iringa ndiyo kinara, leo wamekumbwa na mauaji ya koromeo.
Hivi ninavyoandika makala hii, mimi nikiwamo, wakazi wengi wa Mkoa wa Kagera wanalala saa 1:00 jioni. Wanalala muda huo kutokana na hofu iliyotawala. Kwamba kuna kundi la watu wanaotafuta utajiri wa haraka, wanavizia watu wanaotoka kwenye vilabu vya pombe na kuwakata koromeo. Mwanzo ilidhaniwa kuwa wahusika wanatafuta koromeo, lakini sasa tatizo ni zaidi.


Tangu tatizo hili lilipoanza maeneo ya Kibeta, watu zaidi ya 10 wameuawa kwa utaratibu huu mkoani Kagera. Inaelezwa kuwa wauaji wana mtambo, ambapo mtu akiwa amelewa ndiye wanayemtafuta kwani damu inakuwa imechemka inafyonzwa haraka. Wanatembea na mapanga na ndoo ya plastiki. Wanapita kwenye baa kuangalia nani yupo na anatumia kinywaji.
Kisha baada ya hapo wanamvizia njiani, wanamkata shingo, wanaweka mtambo wa kuvuta damu, unavuta damu inatoka yote mwilini wanaiweka kwenye ndoo ya plastiki na kuondoka nayo, maiti wanaitelekeza. Haya yametokea kata za Gera, Igombe, Kibeta na maeneo mengine. Wamekwenda mbali zaidi, sasa wanawinda hata mtu anayeishi peke yake ndani.


Wiki iliyopita walikwenda eneo la Kyamyosi, wakachimba nyumba ya mtu anayeishi peke yake, wakatoboa tundu, mmoja akaingia ndani. Bahati nzuri inadaiwa mtu waliyepanga kumchinja alikuwa na simu akatuma ujumbe kwa marafiki, marafiki wakatoa taarifa polisi, kisha polisi wakawahi katika eneo la tukio. Waliokuwa nje wakakimbia, aliyekwishaingia ndani akiwa na mtambo wa kuvutia damu na ndoo akakamatwa.
 Huko eneo la Kiziba, wananchi inasemekana wiki iliyopita pia waliwakamata watu wengine watatu, wakiwa na mtambo huo wa kuvutia damu, ndoo na mapanga. Walipowakamata wakasema walikuwa wanatafuta nguruwe wa kununua. Wamewapeleka polisi Kyaka na nasikia wamehamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi Bukoba.
Sitanii, baa nyingi sasa zinakufa. Wanywaji wameacha kwenda kwenye baa, na hata wasio wanywaji wana hofu ya kufuatwa majumbani. Polisi mkoani Kagera wanasema wanafanya kazi. Kamanda wa Polisi aliyekuwapo amehamishwa, ameletwa mwingine na inaaminiwa kuwa huyu aliyeondolewa pamoja na kupewa taarifa za kina alikuwa hazifanyii kazi kwa usahihi.


Baadhi wanalalamika kuwa kuna watendaji wachache wanaohujumu juhudi za polisi. Polisi wanafanya doria usiku kucha, lakini wanasema taarifa walizokuwa wanapofikisha kwa wakubwa ndani ya jeshi hilo ilikuwa zinapuuzwa. Kwa sasa polisi wanafurahi baada ya ujio wa Kamanda Olomi. Wanaona angalau hatua zimeanza kuchukuliwa kwa hao wachache waliokamatwa.
Nimejaribu kudodosa damu au koromeo ikichukuliwa inafanyiwa nini, nikapata majibu yanayochang’anya. Baadhi wanasema kuna wanasiasa wanaoitumia damu kushinda uchaguzi. Baadhi wakasema kwa asilimia zaidi ya 70 inaaminika inapelekwa kwa wavuvi wakubwa wanaopeleka samaki viwandani. Inadaiwa kuwa wavuvi wanatumia damu kuvutia samaki, hivyo wanavua samaki wengi na kupata utajiri wa haraka. Taarifa hizi zimenishtua. Naamini uongozi shupavu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela, kwa kushirikiana na Kamanda Olomi ambaye utendaji wake hautiliwi shaka, kuna kila uwezekano wa kumaliza kadhia hii.


Kwa jinsi tatizo lilivyo kubwa, naamini hata Usalama wa Taifa wanao wajibu wa kuongeza nguvu angalau kwa miezi mitatu kuchunguza na kuja na taarifa za kina tuweze kuwatia nguvuni hawa wanaotishia amani mkoani hapa. Serikali ya Mkoa na Serikali Kuu zinapaswa kushirikiana kwa dhati kuhakikisha tatizo hili linadhibitiwa, vinginevyo wakazi wa Mkoa wa Kagera watageuka wakimbizi ndani ya nchi yao.
Sitanii, nahitimisha makala hii kwa kusema utajiri wa kuua binadamu mwenzako kamwe hauwezi kuwa na tija. Nchi yetu isimame sasa iseme ushirikina hapana. Tulichokiona kwenye mauaji ya albino, ndicho kinachoshuhudiwa Bukoba kwenye mauaji yaliyopewa jina la koromeo. Hali hii haikubaliki. Mongela, chukua hatua na najua unaweza. Mungu ibariki Tanzania.