Na Samwel Mtuwa – Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Madini itaanza rasmi uchimbaji wa Madini Adimu yaani Rare Earth Element (REE) kupitia kampuni ya uchimbaji madini ya Mamba ijulikanayo kama Mamba Minerals Corporation Limited (MMCL) yenye ubia kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Ngualla Group UK Limited ambayo ina umiliki kwa asilimia 100 na kampuni ya Peak Rare Earth ya nchini Australia.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu uendelezaji wa leseni za madini na hatua za uchimbaji nchini.

Waziri Mavunde alieleza kuwa mradi huu wa uchimbaji wa madini adimu (REE) upo katika eneo la Ngualla Wilaya ya Songwe mkoani Songwe katika leseni namba SML 693/2023 ambao utachimbwa kwa kipindi cha miaka 30, unatarajiwa kuanza mapema mwaka 2025.

Akielezea kuhusu hali ya ulipaji fidia kwa wananchi Waziri Mavunde alisema kuwa sehemu kubwa ya leseni ya uchimbaji ipo kwenye hifadhi ya mlima wa kijiji cha Ngualla ambapo taratibu za uthamini zinaendelea pindi utakapokamilika fidia itatolewa kwa wananchi husika.

Kwa upande wa mradi wa uchimbaji wa madini ya heavy minerals sand uliopo eneo la Fungoni wilaya ya Kigamboni, Waziri Mavunde alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina umiliki wa asilimia 16 na kampuni ya Strandline Resources inamiliki hisa asilimia 84.

Waziri Mavunde alifafanua kuwa katika mradi huo Serikali ina hisa huru zisizopungua au kushuka thamani ambapo leseni namba ML 678/2022 itadumu kwa kipindi cha miaka kumi na ukomo wake utakuwa Oktoba 2, 2032.

Aidha, Kampuni ya Nyati Minerals Sand inaendelea na taratibu za kukamilisha ulipaji wa fidia ambapo mpaka sasa kiasi cha shilingi bilioni 18.4 kimelipwa kwa wananchi 1,112 kati ya 1224 wanaostahili kulipwa fidia.

April 17, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiani saini ya mkataba wa msingi (Framework agreement) baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Ngualla Rare Earth kuhusu uchimbaji Madini Adimu aina ya Neodymium na Praseodymium (NdPr)

By Jamhuri