Mwanasheria na mmoja wa wafanyabiashara Watanzania vijana, Nyaga Mawalla (pichani chini), amefariki dunia. Amefariki dunia akiwa bado kijana mwenye umri mdogo, lakini mwenye mafanikio makubwa kibiashara.

Nyaga amemaliza safari ya hapa duniani. Hakuna shaka yoyote kwamba baada ya yeye, wengine tunaomjadili sasa tutamfuata, maana hata maandiko matakatifu yamesema kila nafsi itaonja mauti (kulla nafsin dhaaikatil maut).

 

Kwenye makala hii naomba wasomaji waniwie radhi kwa haya nitakayoyasema. Kabla sijaendelea, niseme wazi kwamba nimesikitishwa mno kwa kifo cha kijana huyu.

 

Ndugu zangu, tumekuwa na kawaida ya kuwamwagia sifa njema wenzetu waliotangulia mbele ya haki. Mara zote sifa hizo zimetolewa hata kama waliofariki dunia walikuwa majambazi, wauaji, wezi au watu wenye roho mbaya. Nyaga hakuwa na sifa hizo zote, lakini nashawishika kusema hakuwa mzalendo wa kweli. Alijipendelea kiasi cha kupoteza sifa ya uzalendo.

 

Amefariki dunia akiwa na deni kubwa la uadilifu kwa Tanzania na Watanzania. Ameshiriki vilivyo kuwapoka ardhi wananchi kadhaa wanaoishi kando ya hifadhi mbalimbali, na kuhakikisha wawekezaji wa kigeni wanapata maeneo hayo. Nyaga, kwa imani yake katika utajiri, na kwa kutumia mbinu zake za kisheria, amewafanya wakazi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Serengeti waingie mikataba ya aibu na wawekezaji. Aligeuka na kuwa nabii wa mabepari na ubepari.


Nyaga ameiyumbisha mno Wizara ya Maliasili na Utalii. Amefariki dunia akiwa anahaha katika jaribio lake la pili la kuhakikisha ugawaji vitalu vya uwindaji wa kitalii unarejewa upya, baada ya kukwama kwenye jaribio la awali la kuibadili Sheria namba 5 Wanyamapori ya mwaka 2009 na Kanuni zake za mwaka 2010. Kamwe hakuwa na hoja za kunishawishi niamini kuwa anachotaka kibadilishwe kwenye sheria hiyo kina masilahi kwa Watanzania.


Katika utetezi wake wa kuipinga sheria niliyoitaja, alitumia vitisho kadhaa kuwatia hofu wananchi, na kwa kweli ni kama alitaka viongozi wa Serikali na hata wabunge waogope. Akasema Tanzania ikitekeleza sheria hiyo, basi ijiandae kushitakiwa!


Akadiriki kusema Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 inakinzana na Sheria ya Uwekezaji nchini na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ina vimelea vya ubaguzi! Ndiyo, kama inakinzana, hilo si jambo la kutusumbua. Busara hapa kwenye mkinzano ni kuamua turekebishe sheria ipi kati ya hizo mbili. Tubadilishe ili tuwabane wawekezaji, au tulegeze ili waendelee kuchota rasilimali zetu.


Alijua fika kuwa Katiba yetu inazuia ubaguzi, lakini haisemi kwamba kwa kuwa Tanzania inapinga ubaguzi, basi tuwaache wageni wachote tu rasilimali zetu kwa sababu kuwazuia ni ubaguzi! Hakuna.


Ibara ya 9 (c) inasomeka, “Kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine”


Shughuli za Taifa kwa tafsiri nyepesi kabisa hapa bila shaka ni pamoja na sheria zinazotungwa kwa ajili ya rasilimali za nchi. Ibara inasema utajiri wa nchi utumiwe kwa manufaa ya wananchi wote. Wananchi hapa ni Watanzania, na wala si wageni ambao Nyaga amewatetea hadi anafariki dunia. Mtu kumnyonya mwingine inamaanisha mtu katika nchi – bila kujali kama ni Mtanzania au mgeni. Lakini kwa utajiri kuwanufaisha wananchi, ina maana walengwa ni Watanzania – wenye nchi. Mtu si lazima awe Mtanzania, anaweza kuwa katoka Marekani au Afrika Kusini kama wengi waliotetewa na kubebwa na Nyaga.


Ubaguzi katika suala la maendeleo, hasa kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika ni ubaguzi halali! Tuangalie mifano michache. Uingereza, Marekani, Afrika Kusini na kote alikoenda Nyaga, wenye nchi hizo wameweka sera za “ubaguzi”. Sheria zao wanazitunga kwa misingi ya kuhakikisha kuwa wanaonufaika na rasilimali za nchi ni wana wa nchi hizo kwanza.


Nyaga alikuwa rafiki wa wageni aina ya kina Harpreet Singh Brar ambaye alikuwa na pasipoti ya Uingereza namba 761039340 na sasa ana pasipoti ya Tanzania yenye namba AB342102. Ni Mkurugenzi wa kampuni kadhaa zilizopata vitalu vinono vya uwindaji kama Mtanzania! Fikiria, mtu kazaliwa Uingereza anaukana uraia wa nchi hiyo na kuwa tayari kuwa raia wa nchi yenye “matatizo” kama Tanzania. Mwenye akili hahangaiki kujua kilichomfanya aukane uraia wake wa asili.


Nyaga alifikia hatua ya kuwatisha wananchi kwamba kampuni za kigeni zikiondoka, watu 5,200 watapoteza ajira. Alitunga takwimu hizo ili kuwatisha watoa uamuzi. Hakuna idadi hiyo ya waajiriwa kwenye kampuni hizo.


Alijua kuwa hata Afrika Kusini kuna “Black Empowerment”.

Hapa kwetu kuwataka Watanzania wamiliki uchumi wao, na wageni wawe wa kununua sehemu ya hisa au kuwawekea ukomo, si ubaguzi. Ni jambo la kiungwana. Duniani kote watu wenye mapenzi mema na nchi na wananchi wao, ndivyo wanavyofanya.


Nyaga alitumia kila mbinu kuhakikisha anakuwa wakala wa wageni katika kupata vitalu. Akajitahidi kuandaa hadi semina za kuwarubuni wabunge. Moja ya semina aliziendesha katika hoteli ya St. Gasper mjini Dodoma. Akawahadaa wabunge kwamba ugawaji vitalu uliofanywa unahatarisha rasilimali ya wanyamapori.


Akiwa wakala wa Wazungu, akakomaa kuhakikisha ugawaji vitalu vilivyopo Ziwa Natron unafutwa. Akataka la Pori la Akiba la Ugala aachiwe yeye. Akaapa kuyapata kwa udi na uvumba maeneo mengine kama Maswa ambako wanaoyataka wako tayari kutumia fedha kiasi chochote kuyapata. Ameshiriki kuwakwaza wafanyabiashara Watanzania katika tasnia ya uwindaji wa kitalii.


Amefariki dunia akiwa na deni kubwa la kuhakikisha anapata vitalu – si chini ya vinne – ambavyo Wazungu hadi leo wanavitaka kwa gharama yoyote. Naamini aliyekufa ni Nyaga, lakini dhamira ya wageni hao bado ipo pale pale. Amefariki dunia akiwa anahaha kwa mbinu zote anazozijua, kuhakikisha wazalendo, tena waliopata alama nyingi kwenye uthamini, wananyang’anywa vitalu walivyokabidhiwa kisheria licha ya kupata alama nyingi hata kuwashinda wageni.


Baadhi ya maofisa katika Wizara ya Maliasili na Utalii walielekea kulegea na kutaka ugawaji vitalu urejewe. Lakini wapo Watanzania makini na shupavu ndani ya Wizara hiyo na katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliotoa hadhari ya kurejewa ugawaji upya vitalu kwa kigezo tu cha kuwafurahisha na kuwaneemesha Wazungu.


Nyaga ameaga dunia wakati waliopewa vitalu kisheria wakitakiwa kuwa wamelipia ada zao ifikapo Machi 30, mwaka huu. Amefariki dunia akitambua kuwa mpango wake wa kupoka vitalu wazalendo na kuwapa Wazungu umegonga mwamba licha ya kutumia ushawishi wa hali na mali. Nani anaweza kubisha kuwa hilo linaweza kuwa moja ya mambo yaliyompa mshituko?


Nihitimishe makala hii kwa kusema wazi kwamba ndugu yangu Nyaga, pamoja na kujitahidi kuonekana muungwana, hakuwa mzalendo.


Alijali zaidi masilahi yake na jamaa zake Wazungu kuliko Watanzania. Alikuwa wakala mahiri aliyehakikisha anatumia taaluma na haiba yake kuwabana wanyonge na kuwatetea wageni. Kifo chake kinapaswa kufungua ukurasa mpya wa utendaji kazi ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, hasa kwenye Idara ya Wanyamapori ambako imezoeleka kuona wenye fedha na kujuana na viongozi wakuu, ndiyo wanaoifaidi tasnia ya uwindaji wa kitalii.


Namlilia Nyaga kama rafiki yangu, lakini naendelea kumtambua kama mmoja wa Watanzania walioamua, ama kwa tamaa au kwa kutojua, kuwa mawakala wa Wazungu walioapa kuitafuna Tanzania kwa nguvu za fedha zao.  AMEN.


Please follow and like us:
Pin Share