Ulimi mzuri mali, mbaya hatari

Sitafuti mashahidi wa haya nitakayosema, kwani kauli nitakayotoa ni yumkini na yanayotokea hapa Tanzania – ya watu kusema na kutenda mambo bila hadhari.

Kabla ya kusema hayo, nanukuu baadhi ya maneno yaliyomo kwenye wimbo wa ‘Ulimi’ ulioimbwa na bendi ya muziki wa mahadhi ya taarab – Black Star miaka 40 iliyopita ikiwa na maskani yake kati ya barabara ya 13 na 14 kwenye barabara kubwa ya Makoko (Msikiti wa Ijumaa) wa jijini Tanga:

 

“Ulimi wa pilipili, haufai kutumia, hutenga watu wawili, hadhari nakwambia, ulimi mzuri mali, hupendeza wasikizi, huvuta walio mbali, hufuata maongezi, sikia yangu kauli, hilo ni jambo azizi.”


Nimeunukuu ushauri huo kutaka kuonesha mambo mawili makubwa. Kwanza thamani na matumizi mazuri ya ulimi, na pili faraka na matumizi mabaya ya ulimi.

 

Ulimi unapotumika vizuri hujenga utu, upendo na heshima na kuweka umoja, amani na utulivu. Unapotumika vibaya hutoa maneno ya kejeli, dharau na matusi, na kujenga chuki na vurugu ambazo huzaa mfarakano ndani ya jamii husika. Kwa muda mrefu viongozi na wananchi wa Tanzania wametumia vizuri ndimi zao kujenga umoja, upendo na mshikamano katika shughuli mbalimbali zikiwamo za ulinzi, uchumi, siasa, utamaduni na michezo.

 

Matumizi mema hayo yamevuta mataifa mbalimbali kutoka Afrika, Asia, Ulaya, Marekani na Australia kujenga urafiki, udugu na kusaidia kutoa huduma za kijamii katika sekta za elimu, afya, maji, barabara, kilimo na michezo.

 

Ni dhahiri, matendo mema yote hayo yasingestawi kama ulinzi na usalama wa raia ungekuwa mgogoro. Ni wazi, ndimi njema za Watanzania zimesikika na mataifa duniani hata kuyafanya kuipa nchi yetu sifa ya KISIWA CHA AMANI.

 

Sifa njema hiyo haina budi kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa kwa faida yetu na vizazi vyetu vijavyo. Tusizipe nafasi semi zisemazo “Ngoma ikilia sana mwisho hupasuka, na mgema akisifiwa tembo hulitia maji.” Ya Rabii tuepushe na semi hizo.


Leo nchini mwetu wapo wananchi wanaohusudu kutaka kutumia ndimi zao kutia mwasho masikioni mwetu na kupeleka mshawasha katika bongo zetu ili tujenge uhasidi, chuki na mfarakano kwa lengo la kuvunja utaifa. Baadhi ya viongozi wa siasa wanathubutu kurefusha ndimi zao, mishipa ya shingo kusimama na macho pima, kuhamasisha wananchi kuvunja sheria na kanuni za nchi kwa mtaji wa demokrasia. Si busara wala maadili ya uongozi bora.

 

Wanaharakati wanatumia kigingi cha Haki za Binadamu na Utawala Bora, kushawishi vikundi vya taaluma fulani kuitia jakamoyo Serikali iwape maslahi bora zaidi; hata kama Serikali haina uwezo wa kutoa. Vitendo hivyo vinakoleza na kujenga chuki kati ya Serikali na vikundi hivyo.


Viongozi wa madhehebu ya dini wanabariki ndimi za waumini wao kuvunja taratibu zilizopo za Serikali na kuzuia haki za waumini wengine, kwa madai ya uongozi umetoka kwa Mungu. Kauli hizo zinachochea utengano na kujenga sintofahamu kati ya Serikali na taasisi za dini.

 

Wananchi wanashabikia kauli hasi kutoka kwa viongozi wao huku wakirindima kwa mayowe, “Hatukubali hadi kieleweke” na kutenda uovu. Kabla kuanza kupima majawabu ya matendo yao hujikuta wamekwishazama ndani ya maangamizi.

 

Nayo Serikali inatoa majibu yasiyokidhi hoja za raia wake. Inatoa vitisho kwa wadai haki, na kutumia mabavu na sulubu kuwaadhibu wapinga dhuluma. Vitendo hivyo vinaondoa mapenzi kati yake na raia wake. Huo si uadilifu na utawala bora, isipokuwa kujenga vyanzo vya uasi.

 

Makundi makuu yote hayo yameshaleta madhara. Nchi hivi sasa inayumba na inayo harufu mbaya ya uovu na kupoteza sifa nzuri ya amani na utulivu, kutokana na kauli zinazotolewa na baadhi ya watu katika makundi hayo.

 

Kejeli, dharau na matusi vimekuwa ni sera. Chuki, vitisho na vurugu ndiyo miongozo. Nchi tunaipeleka wapi? Ni kweli macho hayaoni, masikio hayasikii wala pua hazivuti harufu ya damu? Tuzinduke na tujisahihishe Watanzania. Wakati ni huu.

 

Rai yangu kwa makundi yote hayo; watu wawe waungwana katika kauli na vitendo vyao. Wachague maneno murua ya kusema na vitendo maridhawa vya kutenda. Waache kauli za uchochezi na kushabikia vurugu.

 

Wananchi turudi kwenye uzalendo wetu. Nchi haijengwi na kustawishwa na miundombinu ya maisha tu. Inajengwa na kudumishwa pia na ndimi fasaha, vikao makini na yakinifu, na matendo kuntu ya wazalendo.

 

Rais wangu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete iangalie Tanzania. Barafu ya umoja inayeyuka na utaifa unameguka. Nyasi za kijani za amani zinakauka na nyasi kavu nyikani zinashika moto. Uzalendo unadidimizwa ndani ya bahari ya utandawazi. Angaza.


Please follow and like us:
Pin Share