Na Jumanne Magazi

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema ameridhishwa na ujenzi na majaribio ya safari ya treni ya mwendokasi maarufu SGR, kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Ameyasema hayo leo Machi 18, 2024, wakati wa muendelezo wa safari za majaribio za treni hiyo ambapo amesema kuanzia mwezi Julai mwaka huu wanataraji kuanza safari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Amesema kwa majaribio hayo wanayofuraha kuwatangazia Watanzania kuwa ujenzi wa reli hiyo umefikia zaidi ya asilimia 94 kwa kipande Cha Dar es Salaam hadi Dodoma.

Aidha Prof. Mbarawa ametoa rai kwa Watanzania kupuuza taarifa za uzushi kuhusu kwamba ujenzi huo hauna tija, badala yake watu wamejionea wenyewe kasi na mabadiliko ya utendaji na matengenezo ya reli hiyo.

Amesema awali walifanya majaribio ya vichwa ambayo ilichukuwa miezi miwili ambapo amesema vichwa viliweza kufanya kazi kwa ufanisi.

Prof. Mbarawa amesema baada ya majaribio hayo wamejiridhisha, na sasa wameanza kuunga vichwa vya umeme ukiwa sambamba na kuunga mabehewa 12 kutoka 4 vya awali.

Aidha Mbarawa amesema kwa sasa wapo kwenye majaribio ya kiusalama hivyo treni hiyo haliwezi kukimbia mwendo mkali kwakuwa Bado kilometa zinazopaswa kukimbia sio sahihi kulingana na vichwa husika.

Amesema kuanzia mwezi Julai mwaka huu wanataraji kuanza operesheni hivyo wataongeza vichwa vyenye kasi kubwa kulingana na umbali wa safari,ikiwa ni agizo Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amelitaka Shirika la Reli nchini kuanza kutoa huduma haraka kabla ya kufika Julai mwaka huu

Prof Mbarawa amesema mara reli hiyo itakapo kamilika baada ya majaribio yote kukamilika itakuwa na uwezo kutoka Dar es Salaam kwa muda wa dakika 90, na saa moja na nusu, ikiwa ni tofauti na usafiri wa kawaida

Awali mkuu wa Morogoro Adam Malima ambaye alikuwa sehemu ya mapokezi ya treni hiyo amesema huu ni muda muwafaka kwa wananchi wa Morogoro kutumia reli hiyo kwa ajili ya fursa za kiuchumi, kwa wafanyabiashara na wakulima kufanya biashara.

Aidha mkuu huyo wa mkoa amemuomba waziri Mbarawa kuongeza mikakati kama wizara kutanua miundombinu ya reli mbali ya SGR ikiweno reli ya kati na Ile ya TAZARA.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema kwa sasa wapo kwenye uhakiki wa miundombinu ya treni ya mwendokasi SGR ikiweno vichwa na mabehewa.

Akizungumza wakati wa safari ya majaribio ya treni hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo amesema wao kama shirika wamejipanga vyema na hivi karibuni wataanza safari za masafa mafupi.

Kadogosa amesema majaribio hayo ni endelevu na kuwa hadi sasa ujenzi huo umekalika kwa asilimia 98.9 kutoka Dar es Salaam hadi mlMorogoro.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi TRC, Ali Aman Kalavila, amesema kwao ni mafanikio makubwa kibiashara.

Amesema wananchi walikuwa na haki ya kulalamika kutokana na kuchelewa kuanza kwa huduma hiyo lakini kilio hicho kinakwenda kukamilika hivi karibuni.

Kavila amesema wao wanakwenda kubadirisha mfumo mzima wa kibiashara katika sekta ya kibiashara kwani wemepanga kupanua wigo kiutendaji kwa kufika maeneo mengi ya nchi pamoja na nchi za nje.

Kwa upande wake Yahya Rashidi Abdallah mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar amesema amefurahi kuwa sehemu ya safari hii ya majaribio ya SGR.

Amesema anamshukuru mheshimiwa Rais Samia kwa maono yake ya kuendeleza miradi hii ya kimkakati, hivyo amewataka wananchi kuwaunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Samia kwa utekelezaji miradi hiyo.

By Jamhuri