Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro  linamshikilia mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la  Mohamedi Omari, mkazi wa kijiji cha Kimamba A, wilayani  Kilosa  kwa tuhuma za  kumuua mkewe  na kumzika ndani ya chumba wanacholala.

Tukio hilo la kuhuzunisha  ambapo kabla ya kifo chake inadaiwa  marehemu baada ya kipigo kikali  kutoka kwa mumewe alilia kwa uchungu akimsisitiza  kutunza watoto wake ambao hakuzaa nae.

Akizungumza tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa baada ya kufanya mahojiano na watoto wa mama huyo aliyetambulika kwa jina la Beatrice Haiyasi wameeleza jinsi walivyopitia unyanyasaji mpaka kupelekea kukosa huduma muhimu za kielimu kutokana na kufungiwa ndani.

Pia ameeleza kuwa tukio hilo limebainika mara baada ya mtuhumiwa huyo kudaiwa kuuza mabati ya mkewe ambaye amekuwa akiishi naye baada ya kumuua mwanamke mwingine.

Amesema kuwa kutokana na kitendo hicho kilisababisha ugomvi ambapo watoto wa marehemu walimkanya marehemu asigombane na mtuhumiwa kwani atamuua kama alivyomuua mama yao.

“Tulipata taarifa za mama huyu kuuawa na mume wake kutoka kwa wasamaria wema hii ni baada ya kutokea ugomvi kati ya mtuhumiwa na mke wake ndipo watoto wa marehemu wakaanza kumkanya mama huyo kuwa asigombane na mtuhumiwa huyo kwani atauawa kama alivyouawa mama yao ndipo mama huyo akatoa taarifa kwa mamlaka husika” amesema Shaka.

Kwa upande wa majirani wameeleza kuwa familia hiyo ilikuwa ni ngeni katika eneo hilo hawakuwa wanachangamana na wakazi wa eneo hilo kwani walikuwa ni watu wa kujifungua ndani.

Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema wanamshikilia mtuhumiwa huyo na uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.