Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imesema mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeendelea kuimarika na kukua kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021, asilimia 9.1 mwaka 2023 na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde ameeleza hayo leo Mei 15,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya na utekelezaji wa Serikali ya awamu ya sita.

Waziri huyo ameeleza kuwa Sekta ya Madini imefanikiwa kuvuka lengo la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa mwaka mmoja kabla ya muda ulioainishwa katika Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026 na kufikia mchango wa asilimia 10.1 mwaka 2024.
“Kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021, asilimia 10.8 mwaka 2022 na kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023”amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan, maduhuli ya Serikali yamepanda kutoka Shilingi bilioni 623.24 Mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.18 Mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 20.8 ya makusanyo kwa miaka mitatu.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara ilipewa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni Moja na kwamba hadi kufikia tarehe 14 Mei 2025, Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 902.78 sawa na asilimia 90.28 ya lengo la mwaka 2024/2025.

“Mchango wa Sekta ya Madini katika fedha za kigeni kwa mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi umeendelea kuimarika kutoka Dola za Marekani bilioni 3.1 sawa na asilimia 45.9 mwaka 2021 hadi Dola za Marekani bilioni 3.55 sawa na asilimia 46.1 mwaka 2023,” amesema.
Kwa upande wa mauzo ya bidhaa zisizo asilia (non-traditional goods), amesema mchango wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 53.8 mwaka 2021 hadi asilimia 56.2 mwaka 2023.
Amesema tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini mwaka 2019, Masoko na Vituo vya Ununuzi vimeongezeka kutoka 42 na 100 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 43 na 109 mwaka 2024/2025 mtawalia.

