Mchango wa mlemavu wamng’oa mwenyekiti

MOROGORO

Na Mwandishi Wetu

Wakazi wa Lukwenzi, Mvomero mkoani Morogoro wamemwondoa madarakani Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Zakaria Benjamin, wakimtuhumu kupoteza fedha za umma, zikiwamo Sh 350,000 zilizotolewa na Maria Costa ambaye ni mlemavu.

Benjamin amekuwa akilalamikiwa mara kwa mara kwenye Kamati ya Siasa ya Kata ya Mziha, akidaiwa kutumia vibaya fedha za ujenzi wa daraja, shule na kutotoa taarifa ya mapato na matumizi kwa muda mrefu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 14, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kata hiyo, Shadrack Mahoma, amemtaka Benjamin kuachia uongozi ili kupisha uchunguzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU).

Benjamin pia anatuhumiwa kupokea rushwa ya Sh 200,000 kutoka kwa mfugaji mmoja aliyelisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima pamoja na kumiliki pingu bila kibali.

Katika mkutano huo, wajumbe watano miongoni mwa sita wa Halmashauri ya Kijiji cha Njeura, waliitwa mbele ya wananchi ili mmoja wao achaguliwe kukaimu nafasi iliyoachwa wazi hadi uchunguzi utakapokamilika, na Bakari Ramadhan akachaguliwa.