KATAVI

Na Daniel Kimario

Mwaka 2020 Tanzania iliingia katika uchumi wa kati. Uwanda huu unatafsiriwa na wataalamu mbalimbali, Benki ya Dunia na vyombo vyake kuwa ni uwanda wa mataifa ambayo uchumi wake unawezesha pato la mtu mmoja mmoja kuwa kati ya dola za Marekani 1,026 na 12,475 kwa mwaka. 

Tanzania imefikia hatua hiyo baada ya kufikia pato la dola za Marekani 1,080 kwa mwaka 2019. 

Vigezo vya uchumi huu ni pamoja na kiwango cha umaskini kupungua, urahisi wa upatikanaji wa huduma za kijamii kama afya, elimu, maji, usafiri, ubora wa sheria na mifumo yake, ubora wa taasisi na huduma bora, ubora wa miundombinu na kasi ya ukuaji wa uchumi.

Utekelezaji wa majukumu na utendaji kazi katika taifa lolote hugawanyika katika sekta mbalimbali ili kupata motokeo chanya. 

Hatua iliyofikia Tanzania imechagizwa na sekta zote kwa ujumla wake; yaani siasa, utawala, uchumi, kijamii, utamaduni, sanaa na sekta ya fedha na mipango.

Kila sekta ina wake; uwe mkubwa au mdogo, unaopimika na usiopimika ambapo bila mchango huo kuingia uchumi wa kati ingekuwa bado nadharia. 

Lakini kupitia vigezo mbalimbali, Benki ya Dunia (WB) imetupima na sasa tumehitimu.

Kupata maendeleo hufananishwa na kazi za wadudu kama mchwa na nyuki wanavyofanya kazi. 

Mchwa, pamoja na udogo wao, hujenga kichuguu kikubwa huku nyuki nao ‘hujenga; nyumba zao na kutengeneza masega ya asali huku wakiendeleza koloni lao. 

Mgawanyo mzuri wa kazi, uwajibikaji, bidii na umoja ndiyo sifa kubwa ya wadudu hawa. 

Dira ya Maendeleo inatutaka kuwa na tabia kama ya wadudu hawa. 

Kaulimbiu au mwitikio mpya wa salamu usemeo; ‘kazi iendelee’, inabeba ujumbe huo kwa uzito stahiki.

Sekta ndogo ya sheria na utoaji haki imo ndani ya sekta ya utawala. Kwa hakika hii ni sekta mtambuka inayogusa karibu sekta zote, kwa kupitia Katiba ya nchi.

Kila taifa katiba na sheria huwa na nafasi muhimu katika usimamizi wa masuala yote iwe ya kisiasa, kiuchumi, kijamii au kitamaduni. 

Kwa maana hiyo katiba na sheria haviwezi kutenganishwa na maendeleo na ustawi wa nchi na watu wake.

Hata hivyo, uhusiano wa katiba, sheria na maendeleo au ustawi wa taifa na watu wake huwa si rahisi kueleweka kwa wananchi na hata wataalamu wa fani nyingine. 

Lakini ni muhimu kuhusianisha na fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali, hasa baada ya kuingia uchumi wa kati, hasa kwa wawekezaji, wabunifu na wengine wanaoangalia na kutafiti mambo na mwenendo wa shughuli mbalimbali ili nao waingie kwenye mfumo.

Tanzania kuingia uchumi wa kati, maana yake ni kujitathmini na kuendelea kuweka sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayoendana na uchumi huo. 

Hivyo ukiwa na taasisi imara ambazo zimefungamana na kujifungamanisha katika utendaji wake, unakuwa na uhakika wa kupiga hatua katika ustawi wa taifa na wa jamii. 

Ushirikiano huu pia hujenga uchumi imara wenye ushindani na uwezo wa kuhimili mikikimikiki ya mataifa mengine.

Ni muhimu kukumbuka kuwa wanasheria na taasisi zao wanachangia kila siku, iwe shughuli za maendeleo, biashara, uwekezaji, ustawi wa jamii na mambo mengine kadhaa ya maendeleo. 

Mchango wa wanasheria katika kufanikisha maendeleo utaugundua kwenye mikataba, biashara, uwekezaji, fedha na utatuzi wa migogoro. 

Wanasheria na taasisi zao pia husaidia kuelekeza uchumi, yaani kuleta mgawanyiko bora wa kipato cha mtu mmoja mmoja ili isitokee uchumi kuwa mikononi mwa wachache; wengi wakibaki maskini. 

Hebu tuangalie mifano michache inayoonyesha mchango wa sheria katika uchumi.

Viwanda. Wengi hutazama viwanda kama mitambo na majengo, bila kuhusisha sheria ambazo huleta muunganiko wa uzalishaji vitu vilivyokusudiwa, vyenye ubora na kwa wingi kuendana na mahitaji ya soko. 

Katika kulifanikisha hili lazima pande zote kupeana taarifa; wanasheria kujua kwa undani mwelekeo wa sekta ya viwanda, hali kadhalika wenye viwanda kujua mwelekeo wa sheria.

Muunganiko huo huleta faida kila upande hasa kipindi tukiwa katika uchumi wa kati wenye tabia, utamaduni, kasi na matarajio yake tofauti na awali. 

Sheria husimamia maendeleo ya haraka ya viwanda huku zikihakikisha walaji wanapata bidhaa bora kwa afya na usalama wao. 

Kwa hiyo ni muhimu sekta ya viwanda na sheria kuendelea na mshikamano uliopo na kubeba matarajio chanya yaliyomo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo na Mpango wa Tatu wa Maendelo ya Taifa; 2021/22 hadi 2025/26.

Kubadilishana taarifa kwa sekta hizi mbili kunasaidia kubadilika na hatimaye kukua kwake; kunawawezesha wasimamiaji wa mifumo kubuni na kutoa miongozo ya ukuaji wa viwanda.

Kushikamana vizuri kwa sekta hizi kunasababisha utendaji usiokuwa na mvutano kati ya wawekezaji hivyo kutekeleza dhamira yetu ya ‘Kazi Iendelee’. 

Utaalamu wa wanasheria, maaarifa ujuzi na weledi wao katika kushauri kinachoruhusiwa au kinachokatazwa, huchangia katika ubora wa huduma ya sheria unaohitajika kusukuma mbele uchumi wa viwanda. 

Hali hii itaharakisha mchakato wa taifa kuingia katika uchumi wa kati wa juu. 

Katika kujenga ubora imara, hatuna budi pia kuingia katika matumizi ya teknolojia ambayo nayo inakuwa kwa haraka. 

Teknolojia ni mkombozi katika maeneo mengi na kiungo muhimu katika maendeleo ya viwanda, hivyo inabidi iwe mkombozi kwa sekta ya sheria.

Ndiyo maana Tanzania imeamua kuwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kuimarisha matumizi ya teknolojia katika nyanja zote.

Vyombo vya kutoa haki. Kujenga uchumi imara si kazi ya wanasiasa au serikali tu, bali pia ni kazi ya Mahakama inayotakiwa kuongozwa na misingi inayohakikisha katika kukuza uchumi na maeneo mengine. 

Kama hakuna uhakika katika sheria, watu hukimbilia mahakamani. Mahakama haitoi uamuzi kwa kumsikiliza mlalamikaji tu, bali pia mlalamikiwa na kuangalia mambo mengine kadhaa.

Mahakama ina mchango katika utekelezaji wa sheria zilizopo au zilizobadilishwa na kuangalia zilizopitwa na wakati na kuishauri serikali kuzirekebisha. 

Haya yote huchangia katika safari kuelekea uchumi wa juu huku mifumo na miundo iliyopo ikifanyiwa tathmini ili ikibidi kurekebisha penye upungufu kulingana na mahitaji ya uchumi wa kati.

Kama ilivyo maeneo mengine, ubora ndiyo nguzo muhimu katika kuleta ufanisi, hivyo hilo halikwepeki katika mfumo mzima wa utoaji haki. 

Ni lazima mifumo ya utoaji haki iimarishwe na kukua huku maarifa, ujuzi, weledi na ubora wa watoa haki nao wakiimarishwa na kuwezeshwa kwa kiwango stahiki.

Tunapozungumzia ubora tunamaanisha taaluma na utaalamu wa kiwango cha juu katika maarifa, weledi, ujuzi, uwajibikaji utekelezaji wa sheria na uamuzi usio na shaka. 

Kiwango cha ubora chini ya hapo kinaturudisha kwenye umaskini ambapo huko tumeshatoka na kuhitimu kuingia kwenye uchumi wa kati. 

By Jamhuri