Wahitimu zaidi ya 10,000 walioitwa katika usaili Idara ya Uhamiaji katika Uwanja wa Taifa mwaka 2013. Vijana zaidi ya 30,000 walipeleka maombi.
Wahitimu zaidi ya 10,000 walioitwa katika usaili Idara ya Uhamiaji katika Uwanja wa Taifa mwaka 2013. Vijana zaidi ya 30,000 walipeleka maombi.

Serikali imetenga Sh bilioni 40 kwa mwaka huu wa fedha wa 2019/2020 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya 25 nchini.

VETA wanasema maombi ya vijana wanaotaka kujiunga kwenye vyuo vyake yamefikia 800,000 kwa mwaka ilhali uwezo ilionao ni wanafunzi 200,000 pekee! Hii ina maana robo tatu ya vijana wanakosa nafasi! Makisio ya VETA ni kuhakikisha inapokea vijana 700,000 ifikapo mwaka 2023.

Hii ni habari njema kwa maelfu ya vijana nchini. Hii ni aina fulani ya ukombozi inayofifishwa na nadharia potofu ya kuamini kuwa elimu ni ya vyuo vikuu tu, na kwamba hii ya vyuo vya ufundi ni kama haina umuhimu. Tunajidanganya.

Mataifa yote yaliyopiga hatua ya maendeleo duniani yamefikia hatua hiyo kubwa kwa kuwekeza kwenye ‘VETA’ zao. Huko ndiko kuliko na ‘vichwa’ ambavyo vikiendelezwa huleta mapinduzi makubwa na ya haraka kwa jamii, taifa na ulimwengu. Wakati huu ambao mapinduzi makubwa ya sayansi na teknolojia yanazidi kunyonga nafasi za ajira kwa vijana, njia sahihi ya kukabiliana na hali hii ni kuwekeza zaidi kwenye ‘VETA’.

Mimi ni miongoni mwa wanaoamini kuwa huwezi kuwa na idadi kubwa ya wahandisi inayozidi ile ya mafundi mchundo. Hatuwezi kuendelea kwa kuamini katika kuwa na idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu, na wakati huo huo tukapuuza mamilioni kwa mamilioni ya vijana wanaohitimu shule za msingi na sekondari kila mwaka.

Pamoja na kuipongeza serikali kwa kutenga Sh bilioni 40 kwa ajili ya VETA, ukweli ni kuwa kiasi hiki bado ni kidogo mno. VETA inahitaji fedha nyingi zaidi. Kuwepo utaratibu wa wazi wa kuwakopesha wasomi wa VETA na vyuo vingine vya ufundi. Huko ndiko kwenye nuru ya Tanzania mpya ya kesho na keshokutwa.

Kwenye mtandao wa kijamii kuna andiko zuri linalohusu aina ya elimu tunayopaswa kuwapa vijana wa taifa letu. Sina hakika na aliyeliandika, lakini itoshe tu kusema maudhui yaliyomo ni hazina na mwongozo mwema kwa watunga sera na wazazi wote wenye nia ya kuona tunakuwa na Tanzania yenye vijana waliojaa fikra mpya za ukombozi wa kiuchumi.

Mwandishi wa waraka huu ametajwa kuwa ni Profesa Kamuzora. Nalileta kwenu tulisome sote ili tufaidi ushauri huu muhimu. Mambo mazuri kama haya hatuna budi kuyapata – tukilenga kubadili mtazamo, kwa kuachana na elimu iliyozoeleka kwa miaka yote.

Anasema: “…Falsafa ya elimu yetu ni kuwa watu wanasomea taifa na si kusomea maisha yao. Hivyo, wote mnaingizwa kwenye behewa kuelekea kwenye combinations ambazo taifa limechagua, yaani PCM, PCB, PGM, CBG, CBN, ECA, EGM, HGL, HGE, HGK. Ukikosa nafasi kwenye behewa sasa ndiyo ukatafute hizo fursa zingine za NACTE na VETA.

“Falsafa hii na mfumo huu una athari za kisaikolojia. Kwanza unafanya watu wakikosa nafasi kwenye behewa la form five wajione kuwa ni watu waliofeli na waliopoteza ndoto za maisha.

“Pili, inafanya elimu ya NACTE na VETA kuonekana kama ni sitara na hifadhi kwa waliokosa nafasi behewani. Matokeo yake, tunapeleka huko kwenye NACTE na VETA waliopoteza matumaini. Yaani tumegeuza NACTE na VETA kuwa ni elimu mbadala na si chaguo tu kama kwenda form 5.

“Katika hili nitapenda kutoa mfano wa jamii ya Watanzania wenye asili ya Asia. Hivi hawa wanaishiaga wapi? Mbona wengi hawaendi form 5 na hata wanaokwenda hawasomi HGL, HGK na HGE bali utawakuta aidha kwenye PCB, PCM na ECA na EGM? Na je, mbona huko chuoni hawaonekani kwenye vitivo vya Sheria, Sayansi ya Siasa, Sosiolojia, Historia na Archaeology?  Mbona ni kama hawapo kabisa kwenye Masters degree zinazotolewa na Chuo Kikuu kipendwa cha UDSM, pia hawapatikani kule kwenye Masters za jioni za Mzumbe wala zile za Open University? Lakini mbona pamoja na kutowaona huko kote hatuwaoni mtaani wakipita na bahasha za khaki zenye photocopy za vyeti na barua za kuomba ajira? 

“Wenzetu hawa walishajinasua siku nyingi katika mtego wa fikra tuliouingia wa kusomeshea watoto kwenda kujaza nafasi za wanaostaafu na kufa katika sekta ya umma. Wenzetu wanajifunza stadi zaidi. Anayetaka uhasibu, akifika form four anajisajili kwenye mitihani ya Bodi za Uhasibu (NBAA na ACCA) anaendelea huko. Wengine watakwenda kujifunza masuala ya kukatisha tiketi za ndege IATA system, wengine watakwenda kujifunza stadi za Hardware na Software Engineering na stadi nyingine nyingine. Wengine watasomea u-pilot, wengine insurances nk. Leo nenda kwenye nursery schools walimu  wengi ni Watanzania Waasia kwa kuwa wanakwenda kusomea fani hiyo. Kwao behewa la form 5 ni moja tu kati ya mabehewa mengine na si behewa takatifu au la wateule.

Wenzangu na sisi tunakwenda na behewa, tunaingia chuo tunapigwa sumu ya DS 101 tunakuwa wanamapinduzi na wachukia mabeberu huku tukisoma archaeology, sociology, political science na Kiswahili mwisho wa siku [mwishowe] tunasubiri Sekretariati ya Ajira itangaze kazi, tunajikuta inaajiri asilimia 10 tu ya waliomaliza chuo. Mwishowe hao hao wasomi wanarudi kuajiriwa na mabepari waliokuwa wanawachukia wakiwa chuoni.” Mwisho wa kunukuu.

Maono ya Profesa Kamuzora yanaashiria kuwapo kwa tatizo kubwa kwenye mfumo wetu wa elimu na namna tunavyowaandaa vijana kuyakabili maisha na kulijenga taifa letu.

Mwalimu Nyerere alishaliona hilo, na akatuasa tuache “kutafuta wachawi” wa maendeleo yetu, badala yake tutumie akili kutatua matatizo yanayotukabili.

Katika kijitabu chake cha TUJISAHIHISHE alichokiandika Mei, 1962; Mwalimu Nyerere anasema maneno haya:“Sababu moja ambayo ilituzuia sisi Waafrika kuendelea ni majibu ya urahisi kwa matatizo makubwa. Shamba letu kama halikutoa mavuno ya kutosha, jibu lilikuwa wazi; au limelogwa au ni amri ya Mungu. Watoto wetu walipokuwa wagonjwa daima, jibu lilikuwa rahisi; au walilogwa au ni amri ya Mungu. Nyumba yetu ilipopigwa radi ikaanguka, jibu lilikuwa rahisi; au ni uchawi au ni amri ya Mungu. Majibu ya namna hii huzuia binadamu kupata sababu za kweli za matatizo yao, kwa hiyo yanazuia akili kutafuta njia za kweli za kuondoa matatizo hayo.

“Siku hizi, tumeanza kutumia majibu mengine rahisi, mambo yakienda mrama, badala ya kutumia akili zetu na kutafuta sababu za kweli, tunalaumu Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n.k. Yawezekana kweli kwamba kosa ni la Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n. k.-lakini yafaa akili ifikie jibu hilo baada ya uchaguzi wa kweli, si sababu ya uvivu wa kutumia akili! Uvivu wa kutumia akili unaweza kufanya tutumie dawa kuondoa matatizo ambayo si ya dawa hata kidogo.” Mwisho wa kunukuu.

Naam! Matatizo yetu, hasa ya ajira kwa vijana tunapaswa kutumia akili zetu kuyatambua na kuyapatia suluhu. Hatuwezi kuondoa lawama za ajira kama mfumo wetu wa elimu utaendelea kuwa huu huu aliousema Kamuzora; na wala hatuwezi kupata majawabu ya matatizo yetu kama tutaendeleza visingizio. Mwalimu ametuasa tutumie akili zetu kuyatambua matatizo yetu na kuyapatia majawabu. Tusitafute mchawi. Kwa kuwekeza katika VETA tutakuwa tumetambua ugonjwa wetu; na kwa kuutambua tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kukabiliana nao. VETA ndiyo jawabu la kweli la utatuzi wa ajira kwa Watanzania wa leo na wa miaka mingi ijayo.

By Jamhuri