Nia ni kusudio, yaani dhamiri ya kutaka kukamilisha jambo au haja. Binadamu hafanyi jambo bila ya kuwa na nia katika nafsi yake. Nafsi humsukuma kutaka jambo lake lifanikiwe katika umbo la uzuri au ubaya.

Nia nzuri au mbaya huonekana binadamu anapoonyesha dhamiri yake kwa binadamu wenzake. Nia njema hupokewa kwa shangwe na nia mbaya hupokewa kwa masikitiko.  Ndipo Waswahili tunaposema, ‘nia njema tabibu, nia mbaya harabu.’ Hili ni jambo la kulizingatia kila mara.

Nia njema ni kutaka utulivu, amani, umoja na mshikamano. Nia mbaya ni kutaka ghasia, chuki, uhasama na uadui wa milele. Hizi ni sifa mbili tofauti katika matumizi. Waswahili tunasema,  nia mbili hazienziani. Ni funzo jingine Watanzania tulielewe na kulizingatia.

Watanganyika na Wazanzibari tulipodai uhuru wa nchi zetu na utu wetu, tulitumia nia nzuri. Tukajikomboa kutoka katika mikono ya watawala wa kikoloni (Wazungu na Waarabu) na kujitawala wenyewe kwa kuondoa unyonge na uonevu uliokithiri.

Tuliweka nia njema na tukaunda muungano na kuimarisha umoja na mshikamano wetu. Leo tunajivuna tunalo taifa moja lililo imara na asili ya historia na utamaduni mmoja. Huku tukiamini umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

Hakika nia hii njema imetuwezesha kuwa na nchi na taifa moja la Tanzania, ambalo tunalifurahia. Furaha yetu inatujengea majivuno yenye thamani kama lulu, utu wetu unaheshimika kama yakuti na Tanzania yetu inapendwa kama feruzi. Je, ni taifa lipi halipendi kuwa na sifa kama hizi?

Wapo wananchi wa mataifa mengine duniani wanapenda wawe na thamani, heshima na upendo kama huu tulionao Watanzania. Lakini wanakosa sifa nzuri hizi kwa sababu baadhi yao katika nchi zao wanahusudu kufanya chuki, hiyana na dhuluma. Wananchi wa aina hii wana nia mbaya.

Wapo radhi kukebehi mafanikio waliyonayo, kupuuza kauli za viongozi wao, kudharau mamlaka za nchi zao na kuharibu miundombinu inayofanikisha kupata maendeleo yao. Kisa, wana nia mbaya. Ama kweli watu wanasema, ubaya hatima yake mbaya. Hili ni funzo jingine tena kwa kila Mtanzania.

Watanzania tukumbuke tangu tuwe taifa moja lenye lugha moja kuu ya mawasiliano, yaani Kiswahili, tumeweza kujijengea ngome madhubuti yenye misingi ya kihistoria, umoja na undugu unaotufanya tuwe na amani na kuishi kwa usalama. Je, hatuoni mataifa ambayo hayana misingi kama hii yanavyotapatapa?

Tusikubali umoja na mshikamano wetu kuvunjwa au kubomolewa na baadhi ya Watanzania wenzetu, waliojaa kiburi, wivu na hiyana zilizotawaliwa na nia mbaya. Kwani wao wamejizatiti kuiangamiza nchi yetu katika kina kirefu cha ufukara. Tukumbuke, ‘penye nia pana njia’.

Watanzania wapenda amani na wenye kuthamini utu wetu, umoja na mafanikio yetu, hatuna budi kuelekeza macho yetu kwao na kuchukua hatua ya kukabiliana nao. Tuweke nia njema akilini na mioyoni katika vita hii, na tukijua, ‘macho yaliyopanda mlima hayaogopi mabonde.’

Na wala tusipuuze maneno machafu kama choo tunayoambiwa na kuyasikia yakitoka vinywani mwao. Tudhibiti matendo yao na mbwembwe za kutweka tanga. Nina amini Watanzania tunafahamu, ‘chombo cha mwenye kiburi hakifiki bandarini.’ Umakini unatakiwa katika jambo hili.

Ni matarajio yangu Watanzania werevu na wasikivu siku zote wako imara na hawakubali kuyumbishwa na mtu au taifa lolote. Ni fahari kupambana kuondoa nia mbaya na kuzidisha mapambano kwa kutumia nia njema.

By Jamhuri