Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, amefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akidai Gazeti la Citizen limlipe fidia ya Sh bilioni 3.

Analilalamikia gazeti hilo akidai liliandika habari zisizo za kweli na kumsababishia adha kubwa kwa jamii.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Leila Mgonya ilianza kitambo kutokana na habari iliyoandikwa na gazeti hilo Machi 23, 2018.

Mchechu anaiomba mahakama iliamuru gazeti hilo limlipe fidia na kumuomba radhi kutokana na habari anayodai kwamba ilimchafua na kumshushia hadhi yake.

Akitoa ushahidi wake mwishoni mwa wiki, akiongozwa na Wakili Vitalis Peter, Mchechu aliiambia mahakama hiyo kwamba habari hiyo ilimshushia heshima kwa jamii.

Kwa mujibu wa Mchechu, habari hiyo ilieleza kwamba alifukuzwa kazi na Rais John Magufuli kwa matumizi mabaya ya ofisi; jambo alilolisema kuwa halikuwa na ukweli wowote.

“Mheshimiwa Jaji kama itakupendeza naomba maelezo yangu yakubaliwe ili gazeti hilo liniombe radhi kwa uzito ule ule na kwa msisitizo ule ule katika ukurasa wa mbele.

“Kwa kuwa habari hiyo iliniumiza, kwa kadiri Mahakama itakavyoona inafaa, naomba nifidiwe hasara za kiuchumi kama nilivyoumizwa na jinsi ninavyoendelea kuumizwa, kwani gazeti hilo limo mtandaoni na linaendelea kusomwa na watu.

“Gazeti la Citizen linasomwa na watu mbalimbali duniani. Kwa hiyo kitendo cha kuandika habari ambayo haikuwa ya kweli dhidi yangu kilinichafua, kilinipa msongo wa mawazo, kiliharibu biashara zangu nilizokuwa nikifanya na wabia baada ya wenzangu kuniona sina uadilifu. Pia habari hiyo ilinifanya nijiuzulu baadhi ya nyadhifa nilizokuwa nazo.

 “Mheshimiwa jaji, nimetumia nguvu na muda mrefu kuijenga familia yangu, baada ya gazeti hilo kuandika habari mbaya dhidi yangu nilivuliwa heshima yangu katika familia.

“Pia mimi ni kiongozi wa kanisa katika ngazi ya usharika, jimbo na ngazi ya dayosisi. Kwa hiyo, habari hiyo ilileta taharuki na sintofahamu kanisani, kwa sababu mimi ni msimamizi mkuu wa fedha za kanisa katika ngazi ya dayosisi.

“Kimataifa, habari hiyo ilinifanya nijiuzulu katika baadhi ya majukumu, ikiwamo kwenye Bodi ya East Africa Breweries. Pia nilijiondoa katika kugombea nafasi ya kutafuta Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha na Nyumba linalohusisha nchi 44 za Afrika ambako nilikuwa na nafasi nzuri ya kupata nafasi ile, kwani sifa zote nilikuwa nazo,” amedai Mchechu.

Amesema kwa kipindi chote alichokuwa mtumishi wa NHC hakuwahi kuchunguzwa wala kuhojiwa na chombo chochote ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kwamba NHC hawajawahi kununua ekari 500 Arusha kama ilivyoripotiwa na gazeti hilo.

Akizungumzia kuondoka kwake NHC, amesema hakufukuzwa kama gazeti hilo lilivyoripoti, bali aliondoka kwa barua nzuri iliyompongeza kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote cha utumishi wake.

“Kwa bahati nzuri, Mungu kaniongoza kurudi tena katika ofisi ile ile, lakini hata kuondoka kwangu NHC kipindi kile, niliondoka kwa barua, walinishukuru kwa kazi nzuri niliyofanya na ieleweke kwamba, mtu aliyefukuzwa hawezi kushukuriwa wala kupongezwa,” amedai Mchechu.

Pamoja na Wakili Vitalis, Mchechu anatetewa pia na mawakili Aliko Mwamanenge na Joyce Mwakapila. Gazeti la The Citizen linawakilishwa na mawakili Ambrose Nkwera na Laban Rugina. Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea Mei 20, 2022.

Kwa sasa Mchechu ni Mwenyekiti wa Benki ya BOA, Mwenyekiti wa Kundi la Kampuni za Amboni, Amboni Beach Properties, Amboni Sisal Ltd, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Kampuni ya Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC), Kampuni ya Watumishi Housing (WHC), Mjumbe wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Dar es Salaam (TUDARCO), Katibu wa Usharika wa Kanisa la KKKT – Mbezi Beach na  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Fedha na Mipango wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP).

Wakati akiandikwa Mchechu alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Mwenyekiti wa Serengeti Breweries Limited, Mwenyekiti wa Benki ya NBC, Makamu Mwenyekiti wa TMRC, Mwenyekiti wa Kampuni za Amboni Sisal Properties Limited na Amboni Beach Limited, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shule za Rightway Schools; Mwenyekiti wa Kampuni ya NHC/PPF Investment Company Limited; Mkurugenzi na Mwanzilishi wa CEO Roundtable (CEOrt), Mkurugenzi wa Bodi ya WHC, Mwenyekiti wa Kikosi Kabambe cha Wataalamu kwa ajili ya Mji wa Makao Makuu ya Serikali Dodoma (Chairman of the Government Special Task Force responsible for the Master-Plan of the Dodoma New Capital City and fundraising strategy and private sector engagement initiatives).

Kimataifa alikuwa Mjumbe wa Bodi ya East Africa Breweries Limited (EABL GROUP) na Mwenyekiti wa Board Audit and Risk Committee.