OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameelekeza Uongozi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuongeza watoa huduma ili kuboresha huduma ya usafiri wa haraka kwa wananchi wa Dar es salaam.

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo Oktoba 24, 2023 kwenye ziara yake kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ili kupata taarifa ya utendaji kazi wa Wakala huo.

Amesema huduma ya mabasi yaendayo haraka ni muhimu sana kwa maisha ya wakazi wa Dar es salaam na inatakiwa kusaidia kupunguza adha ya usafiri, hivyo uwapo wa mtoa huduma mmoja anazidiwa na kusababisha changamoto kwenye baadhi ya maeneo.

Amesisitiza kuwa suala la kuongeza watoa huduma kwa sasa haliepukiki na linatakiwa kuwa kipaumbele kwanza kwa kuwa kuna njia mpya zitakazoanza hivi karibuni.

“Mtoa huduma mliyenaye kwa sasa ni UDART pekee muda umefika sasa kuwa na mtoa huduma zaidi ya mmoja ili kuleta ushindani kwenye kutoa huduma za usafiri kwa ili wananchi wapate huduma bora,” amesema Mchengerwa.

Pia Waziri Mchengerwa amewataka uongozi wa DART kuimarisha mifumo ya kutoa taarifa mara tu panapotokea changamoto yeyote ya usafiri.

“Sijapenda kuendelea kuona vurugu kwenye vituo vya kusubiria mabasi, ni vyema panapotokea hitilafu kuwe na mifumo ya kutoa taarifa ili kupunguza manung’uniko kwa wananchi ambao huenda wamekaa pale muda mrefu kusubiria basi,”amesema.

Awali, akitoa taarifa za utendaji kazi wa Wakala huo, Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Edwin Mhede amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya sita, uwezo wa kusafirisha abiria kwa siku umeongezeka kutoka abiria 90,000 mpaka 210,000 na umetokana na maboresho makubwa yaliyofanyika kwa Wakala huo.