*Aapa kuilinda NHIF kwa nguvu zote dhidi ya wajanja

*Kicheko matibabu saratani, safari za India kubaki historia

*Malawi kuanza kuleta wagonjwa 1,900 Ocean Road

Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameapa kupambana na magenge ya watu ambao wamekuwa vinara wa kutaka kuhujumu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), huku akisisitiza  kwamba hatakubali kuhujumiwa.

Amesema mfuko huo umebeba uhai na ulinzi wa afya za Watanzania, hivyo unapaswa kusimama imara ili utoe huduma zake kwa ufanisi wakati huu ambao serikali imezindua mkakati wa bima ya afya kwa wote, ambapo kila kaya itaanza kuchangia Sh 150,000 kwa mwaka.

Akizungumza wakati wa kikao kazi cha  wahariri wa vyombo vya habari jijijni Dar es Salaam hivi karibuni, Mchengerwa amesema katika kipindi chake cha kuongoza wizara hiyo hatakubali kuona mifumo na taratibu zilizopo zinachezewa na  kundi la watu wachache.

“Kipindi changu cha kuongoza wizara hii sitakubali kuona watu wanachezea Mfuko wa Bima ya Afya kwa namna yoyote ile, serikali imejipanga vizuri kuhudumia wananchi kwa sababu afya ndiyo msingi wa kila kitu.

“Afya ni ngome ya kwanza ya ulinzi wa taifa, uhai na umoja  ambao unaleta ukombozi ambao si wa maneno bali vitendo, ukipuuza afya unachezea usalama wa taifa, tumedhamiria  kuleta mapinduzi makubwa  sekata ya afya kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa na maoni yake katika eneo hili,” amesema.

Amesema kabla ya serikali kuzindua mfumo wa afya kwa wote, lazima  izindue ufahamu, kabla hatujatangaza hatua lazima tuunganishe moyo wa taifa, ni vema tukumbushane tukio hili halijatokea hewani tu, haya ni matokeo na ahadi za Rais Samia.

“Hizi  ni ahadi za siku 100 akiwa madarakani, si kauli za majukwaani, ni dira ya utekelezaji, ndiyo maana kila hatua tunayochukua sasa, bila kusawazisha uelewa na mwendo tunachofanya hapa ni sehemu ya kuyageuza maelekezo ya Rais kuwa matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

“Kwa msingi huo, tunatekeleza kwa ukamilifu, kwa wakati na kwa viwango vinavyolingana na matarajio ya wananchi wetu, si kwa sababu tu ni wajibu wa serikali, bali hicho ndicho kipimo cha uongozi wa kweli, na kazi yetu sisi wasaidizi wake ni moja, kuweka mazingira bora ya huduma, kujenga na kushusha gharama za wananchi katika afya,” amesema.

Amesema kazi kubwa ni kuwatia moyo watendaji na kuwajengea ubunifu, ambapo kila eneo la mtoa huduma za afya nchini zimfuate mwananchi na kumlinda kwa utu na kumuongeza imani yake kwa taifa lake.

“Hapa ndiyo tunakutana na ukweli wa ukombozi, taifa haliongozwi kwa maneno pekee, bali huongozwa kwa nidhamu ya mifumo, nidhamu ya kazi kwenye afya si kazi ya utawala tu, ni suala la usalama wa taifa, kwa sababu uzembe katika afya hausababishi tu ucheleweshaji, unaweza kuzalisha vifo, taharuki na kuyumbisha imani ya wananchi kwa taifa lao.

“Hospitali ikifanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa, taifa linakuwa thabiti, zikilegea, taifa linateteleka, mgonjwa asiyehudumiwa kwa heshima ni raia anayepoteza imani, siku zote imani ya raia ni mtaji kwa usalama wa taifa letu.

“Serikali inaendelea kuwekeza katika kiwango kikubwa cha huduma za ubingwa na ubobezi, ikiwamo ugonjwa wa saratani, upandikizaji wa figo, moyo na huduma zingine za kibingwa, ndiyo maana tunataka mgonjwa au wagonjwa wasiokuwa na uwezo wapate huduma za afya bila kikwazo cha fedha pale wanapohitaji. Huu ni ujumbe wa ukombozi wa kisiasa, siku zote taifa linalowekeza kwenye matibabu bingwa na ubobezi linaamua maisha ya raia wake, hayataamuliwa nje ya mfumo,” amesema.

Amesema wagonjwa wasio na uwezo wanapaswa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha, kuanzia  sasa kwa sababu matibabu bingwa si anasa, bali ni hadhi ya taifa kumkinga na kumjengea uwezo sambamba na wajibu wa dola yenye utu.

“Kama mnakumbuka Januari 23, mwaka huu, kwa mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote nilitangaza kuanza rasmi kutumika kwa kitita  nafuu cha afya kwa gharama ya Sh 150,000 kwa kaya ya watu sita kwa mwaka ili kuwapunguzia wananchi gharama,” amesema.

Anasema  mwananchi akijunga na bima hiyo kutamsaidia kupata huduma kwa wakati, badala ya kwenda kuuza mali, hivyo hapaswi kukatishwa tamaa wala kuchelewa kupata matibabu kwa sababu ya gharama.

“Tumedhamiria, lengo letu kubwa ni kila Mtanzania popote alipo bila kubagua, kuhakikisha anapata huduma bora kwa wakati na kwa heshima inayostahili katika hospitali zetu.

“Afya kwa wote ni daraja la usawa, usawa ndio daraja la umoja, tumeamua kutekeleza jambo hili kwa moyo thabiti  na nia njema kwa wananchi na taifa  letu. Kwa kufanya hivi haina mbadala na inamhusu kila mmoja, tumeamua kwa dhati tumshirikishe kila mtu bila kuacha yeyote nyuma, hiki ni  kipimo cha utu  wa taifa.

“Siku zote taifa linaposema hakuna atakayebaki nyuma  linatangaza mshikamano kwa vitendo, bila uwajibikaji mfumo hugeuka nadharia, unakuwa mzuri kwenye karatasi, dhaifu kwenye uhalisia, bila uamuzi sahihi kwa wakati, afya haiwezi kusubiri, na uzembe wa muda wakati mwingine huwa gharama kubwa ya uhai,” amesema.

Amesema ili kuhakikisha elimu inamfikia kila mtu, watatumia mbinu shirikishi zinazoendana na hali halisi ya maisha ya sasa, zikilenga makundi ya kimkakati kama wakulima, wafugaji, wamachinga, baba na mamalishe, wachimbaji wadogo, bodaboda na wasanii kote nchini.

“Tutatumia uongozi wa Serikali za Mitaa, tutaingiza ajenda ya bima ya afya kwa wote kwenye mikutano na shughuli za wananchi za kila siku, wataalamu  na viongozi wetu watatumia vyombo vya habari vya aina  na ngazi zote kutoa elimu, dhana na ufafanuzi  wa kisheria,” amesema.

Amesema njia nyingine ni kuwafuata wananchi kokote waliko kwa lugha ya makabila yao na maisha yao, kwa sababu elimu ikishuka chini kwa wananchi wakaelewa uelewa hupanda juu kwa taifa.

Kwa upande wa maofisa habari wa wizara hiyo, amewataka wao na wataalamu wengine kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mikakati na miongozo vinafika kwa walengwa na kueleweka.

“Nawaagiza maofisa habari wa wizara yangu kuzuia hatari ya kitaifa ya taarifa potofu, habari, maelezo na elimu vitoke kwa wakati, penye ukimya, uvumi hukua, uvumi ukikua umoja hupungua.

“Nimepata taarifa ya malalamiko wakati mwingine wataalamu wa afya wanapoalikwa kutoa elimu kwenye vipindi hawafiki, ilhali vipindi hivyo hutolewa bure, bila malipo yoyote, hili halikubaliki,” amesema.

Gharama za saratani

Kuhusu gharama za matibabu ya saratani, Waziri Mchengerwa amesema Tanzania imeandika historia  eneo hilo baada ya kuzindua matumizi ya mashine maalumu ya kuchunguza na kutibu ugonjwa huo, PET  CT Scan, katika  Hospitali ya Tiba ya Saratani (Ocean Road).

Amesema uzinduzi huo utaokoa mamilioni ya fedha za Watanzania ambao walilazimika kwenda nchini India kupata matibabu, huku akisisitiza kuwa gharama za matibabu kwa Watanzania ni Sh milioni 1.2, wakati wagonjwa wa nje gharama zimeshushwa  hadi Sh milioni 2.4 na Sh milioni 3.

“Tunataka kwenye utalii wa tiba, ndiyo maana wenzangu Ocean Road, Benjamin Mkapa, Muhimbili na wengine tumejiandaa.

“Naomba niwataarifu Watanzania, wenzetu wa Malawi wamethibitishia wagonjwa wao wote kuanzia sasa rufaa zao itakuwa ni Tanzania, lazima tuwe ‘proud’, wakati mwingine tunajificha ficha hatutaki kuzungumzia mafanikio, sijui tunaficha nini, tumepiga hatua kubwa.

“Tunataka kuangusha mbuyu katika moja ya mataifa makubwa ya Afrika, tunataka kushinda katika sekta ya afya, si majirani zetu, kiwango chetu ni kikubwa. Nataka niwaambie wazi kabisa, ndiyo maana wakisikia habari njema hizi wananuna, sisi tunapenda wanune huku tunawaona.

“Gharama ya tiba na wenzetu Malawi wamekubali kuleta wagonjwa wote nchini kwetu, tunajiandaa vizuri kutoa huduma za kimataifa, hadi sasa tumearifiwa na Waziri wa Afya wa Malawi kuna wagonjwa 1,900 walipaswa kupelekwa India kutibiwa, wote wanakuja Tanzania. Nimemuomba Rais pindi wakikamilisha taratibu zote tutatumia usafiri  kuwafuata, maana watalipia, nitakwenda kuwapokea, sitatuma mtu, hili ni kama adhimisho la kuonyesha wanatibiwa hapa nchini.

“Tunayo mataifa mengi kama Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanapata tiba hapa hapa Ocean Road, tutawawekea utaratibu mzuri wa namna ya kuwatambua. Nisisitize, wenzangu kila  anayekuja hospitalini ni vema tukamtambua kwa kitambulisho chake cha taifa ili serikali isipoteze mapato,” amesema.

Amesema Tanzania imejipanga vizuri kutoa huduma hiyo  tofauti na mataifa jirani ambayo yalianzisha mpango kama huo lakini umeishia kughubikwa na matatizo mengi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa amewasihi waandishi wa habari nchini kuandika habari za afya zinazohusu sekta ya afya ili kusaidia kubaini mianya inayofanywa na watumishi wanaovunja maadili ya kazi zao.

“Nawaomba sana mkawe mabalozi wazuri wa kuandika habari za uchunguzi ambazo zitatusaidia sisi kufuatilia katika mifumo kama kuna ujanja ujanja unaofanywa na watumishi wetu na kuchukua hatua mara moja…kwa kutambua umuhimu wenu, nilimuagiza  katibu mkuu kuleta mifumo yote kwangu ikiwamo ya usjaili,” amesema.

Mashine

Akiwa  amedhamiria kuboresha sekta hiyo, Waziri Mchengerwa amempa siku saba Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Seif Shekalaghe, kuhakikisha anamkabidhi ripoti kutoka kwa waganga wakuu wa mikoa juu ya mashine zinazotakiwa kutoa huduma lakini hazifanyi kazi.


“Nimempa siku saba Katibu Mkuu kuniletea ripoti  ya kila mganga mkuu wa mkoa  ambaye mkoani mwake  ana mashine zinazopaswa kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi lakini hazifanyi kazi, ikibainika kuna uzembe kila mmoja atachukuliwa hatua, tumedhamiria kuwapatia wananchi huduma za afya bora na kwa wakati,” amesema.