Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,Songea

MKUU wa Utumishi (CP) wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Meja Jenerali Paul Simuli amewapongeza walimu wa Shule ya Sekondari ya Ruhuwiko pamoja na bodi ya shule hiyo kwa kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa sayansi kwa miaka miwili mfululizo 2020/ 2021 Jambo ambalo linailetea sifa kubwa shule hiyo ambayo inamilikiwa na jeshi la wananchi.

Meja jenerali Simuli ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 30 ya wahitimu 92 wa kidato cha nne wa shule ya Sekondari hiyo ambayo ipo kidato cha Kwanza hadi cha Sita na ni kati ya Shule 10 zinazomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania .

Meja Jenerali huyo amesema kuwa amesikiliza risala ya wahitimu hao pamoja na taarifa ya shule ambayo imesomwa na mkuu wa shule hiyo Luteni Kanali Benedictor Bahame kuwa shule hiyo imejiwekea malengo ya kufanya vizuri hasa katika kuongeza ufaulu ambao kila mwaka umekuwa ukiongezeka na kuiweka kuwa moja ya zinazofanya vizuri kwenye taaluma hapa Nchini ,hivyo walimu wanatakiwa kuendelea kukazana kuwafundisha wanafunzi ili kufikia malengo ya ufaulu mzuri zaidi ikiwemo masomo ya Sayansi ili kuendana na malengo ya Serikali.

Mkuu wa shule ya sekondari ya Ruhuwiko Luteni kanali Benedictor Bahame akitoa taarifa ya shule ya sekondari ya Ruhuwiko mbele ya mgeni rasmi hayupo pichani kwenye mahafari ya kidato cha nne yaliyofanyika juzi kwenye viwanja vya shule hiyo

Mkuu huyo amefafanua kuwa kumekuwepo na changamoto kwa baadhi ya watu ambao hawana nia njema wamekuwa wakiwatia hofu watoto (Wanafunzi) juu ya masomo ya Sayansi kuwa ni magumu jambo ambalo siyo kweli na lisiposimamiwa ipasavyo kwa kuondoa dhana hiyo potovu Taifa litakosa wataalamu wa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za uanzishwaji wa viwanda.

Hata hivyo mkuu huyo amewapongeza Walimu wa shule hiyo pamoja na mkuu wao kwa kuongeza ufaulu pamoja na kuwafundisha wanafunzi hao katika nyanja nzima ya nidhamu ambayo Wazazi na Walezi wameishuhudia wenyewe kwenye mahafali hayo.

Pia akizungumzia changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi hasa wakijeshi amesema kuwa litafanyiwa kazi huku akimpa agizo mkuu wa shule hiyo kuwa wawapo kwenye vikao vyao wawatafute walimu wa masomo hayo ambao ni raia wanaoendana na umri stahiki kisha wapatiwe mafunzo ya kijeshi ili wasinyang’anywe na taasisi zingine.

Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Luteni Kanali Benedictor Bahame awali wakati akitoa taarifa ya shule mbele mgeni rasmi huyo amesema wamekuwa wakifanya vizuri kwenye taaluma kiasi cha uongozi wa ngazi ya mkoa Ruvuma kutoa na Tamisemi kutoa pongezi za vyeti.

Meja jenerali CP PaulL Simuli akihutubia wanafunzi wa kidato cha nne, wazazi na walezi , walimu pamoja na bodi ya shule ya sekondari ya Ruhuwiko iliyopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma

Mkuu Bahame amesema kuwa licha ya kuwepo kwa Sekondari hiyo lakini bado Jeshi hilo limekuwa na Shule ya Msingi ambayo huanza na awali na baadhi yao wamekuwa wakiendelea na masomo ya Sekondari hiyo wakitokea kwenye shule ya Msingi iliopo kwenye Jeshi hilo.

Bahame amekizungumzia kwa wanafunzi wanaohitimu amesema kuwa Walimu wamewaanda vizuri na kuwa mwaka huu ufaulu utaongezeka zaidi tofauti na misimu mingine kwenye kidato cha nne na sita.

Naye mjumbe wa bodi ya Shule hiyo Yusuph Mwikoki amewataka Wazazi na Walezi kuwajibika kwenye majukumu yao hasa ya kulipa karo (Ada)ili kufanikisha kupunguza baadhi ya changamoto ambazo zingeweza kutatuliwa kwa haraka.

By Jamhuri