LICHA YA KUJITENGENEZEA REKODI NA KUTESA DUNIANI:

WIKI tatu zilizopita, mshambuliaji anayeaminika kuwa ndiye bora zaidi duniani hivi sasa, Lionel Messi, alivunja rekodi ya kuifungia mabao mengi zaidi timu yake ya Barcelona ya Hispania tangu ilipoundwa.

Alimtungua kipa mara tatu katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), hivyo akaifanya Barcelona itoke kifua mbele kwa mabao 5-3 dhidi ya Granada FC, timu iliyokuwa ikishika nafasi ya 16 kati ya 20 zinazosaka ubingwa wa kandanda wa nchi hiyo msimu huu.

Messi alivunja rekodi hiyo ya mabao 232 iliyowekwa miaka 60 iliyopita na mshambuliaji hatari wa timu hiyo enzi hizo, Cesar Rodriquez, baada ya kufikisha mabao 234 kutokana na mechi 314 alizoichezea tangu mwaka 2004.

Mbali na hiyo, Messi pia alijiongezea sifa nyingine duniani mwanzoni mwa wiki iliyopita. Aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikisha mabao 54 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa ni kinda wa miaka 24 tu.

Katika msimu huu pekee hadi sasa, mwanasoka huyo bora wa dunia kwa mwaka wa tatu mfululizo ameziona nyavu za timu pinzani mara 63 katika mechi 50 alizocheza, na kati ya hizo, mabao 36 ameyafunga kutokana na La Liga huku mengine 13 akiyafunga kupitia michuano tofauti ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Amefunga pia “hat trick” 18 akiwa na Barcelona, zile ambazo sita kati ya hizo amezifunga katika msimu huu pekee na kufikia rekodi iliyowekwa na winga wa kulia wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo msimu uliopita, yule ambaye ndiye hasimu wake mkubwa kwa kutikisa katika La Liga.

Katika kikosi cha Barcelona, Messi ndiye anayetegemewa uwanjani kwa mechi zote za ligi na kimataifa hasa anapocheza na miamba ya kandanda kama Xavi Alonso, Cesc Fabregas, Andres Iniesta, Xavi Hernandez na Alexis Sanchez, ile ambayo humlisha mipira ya uhakika kutoka kila kona na kumwacha akiwaadhiri makipa milangoni.

Hao ndiyo wanaomtengenezea nafasi za kupachika mabao, hivyo inawezekana bila kuwapo kwao huenda si lolote wala chochote katika kufamania nyavu.

Ukweli huo unathibitika pale anapochezea kikosi cha timu ya taifa ya Argentina akiwa na watu kama Carlos Tevez, Javier Pastore, Angel Di Maria na Sergio Aguero na kutofanya anachopaswa aifanyie nchi yake hiyo – kuiletea ushindi na makombe ya kimataifa.

Ameichezea Argentina katika michuano mbalimbali – mikubwa kuliko yote ikiwa ni Kombe la Dunia – lakini ameshindwa kuwakuna mashabiki wa nchi hiyo ya Amerika Kusini.

Ndiyo maana ukienda nchini humo, Messi hapapatikiwi sana kama anavyozungumzwa na mamilioni ya mashabiki wengine wa kandanda duniani, hatua inayowaacha wanasoka wa zamani kama Diego Maradona, Jorge Valdano, Gabriel Bastituta na wengineo wakiendelea kuwa kwenye chati zaidi.

Mbali na mambo mengine, Messi pia hajawahi kuisaidia nchi yake kutwaa Kombe la Soka la Dunia, hatua iliyoibua malumbano makali endapo kiwango chake hivi sasa kiko juu zaidi kuliko alichokionyesha Maradona au Pele.

Kikubwa kinachompunguzia sifa ni kushindwa kwake kuisaidia Argentina kutwaa Kombe la Dunia kama walivyofanya wenzake, hivyo kuonekana kuwa mchezaji wa kawaida sawa na wengine.

Kutoka mbali Hispania na Argentina kwa pamoja, mshambuliaji mahiri wa timu ya Azam FC hapa nchini, John Boko ‘Adebayo’ ambaye anaongoza kwa upachikaji mabao katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, msimu huu, naye ana kitu kinachofanana na Messi.

Hadi kufikia sasa, Boko amefunga mabao 16 akiwa anafuatiwa kwa pamoja na mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Kenneth Asamoah na Emmanuel Okwi wa Simba, walioziona nyavu mara 10 kila mmoja.

Lakini kama alivyo Messi, Boko aliyelazimika kuikimbia timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) mwishoni mwa mwezi uliopita kwa kuwa si lolote wala chochote anapoichezea, kiasi cha kuwakera mashabiki na kuanza kumzomea, hatua iliyosababisha ajiuzulu kuichezea Stars.

Mathalani, mshambuliaji huyo wa kati hakuifungia Stars bao katika mechi ya kusaka tiketi ya kwenda kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mwaka 2013, zitakazofanyika nchini Afrika Kusini.

Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, iliikutanisha Stars na timu ya taifa ya Msumbiji (Mambaz) na kutoka sare ya bao 1-1, mechi ambayo Boko aliendelea kuwa ‘kimeo’ na kusababisha mashabiki wawe wakimzomea na kumtaka kocha Jan Poulsen amtoe nje ya dimba.

Siku tano kabla ya hapo, Stars pia ilitoka suluhu uwanjani na timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika uwanja uleule. Lakini aliporejea katika timu yake ya Azam FC siku chache baadaye, mshambuliaji huyo aliifungia mabao mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Yanga.

Katika ushindi mwingine wa timu hiyo ilioupata wiki moja iliyopita, Boko ndiye aliyetoa pasi iliyozaa bao la kwanza lililofungwa na Mrisho Ngassa walipoichapa JKT Ruvu mabao 4-1, kisha akaipachikia bao la pili na la 16 kwake msimu huu.

Kama alivyo Messi anapoichezea Argentina, siku zote Boko hakuwa chochote alipokuwa na Taifa Stars, huku akifanya vizuri anapokuwa na Azam na kuwachanganya mashabiki wa soka nchini.

Ingawa ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao akiwa na timu yake ya Azam na kuvunja rekodi ya ligi hiyo katika historia yake huku ikiwa bado inaendelea, lakini kama Messi naye pia hajawahi kuisaidia Taifa Stars kutwaa kombe lolote.

Hakuwahi kufanya hivyo kwa kuifungia mabao mwenyewe, kutoa pasi zilizotumbukizwa wavuni, kuzisumbua ngome za wapinzani wake au kuwapa fursa washambuliaji wenzake kufunga kwa urahisi.

Ameshindwa kuisaidia Taifa Stars kama walivyofanya washambuliaji wenzake akina Peter Tino, Zamoyoni Mogella, Abdallah Burhan, Abdallah Kibadeni, Kitwana Manara, Justine Simfukwe, Omar Hussein Sultani na kadhalika.

Ndiyo maana alipotangaza kuachana nayo hivi karibuni akidai amechoka kuzomewa, mtu pekee aliyejitokeza hadharani kumzungumzia ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela.

Wengi waliiona hatua hiyo kuwa ilichelewa na ndiyo sababu hawakushangaa wala kusikitika ila kunyamaza. Wanajiuliza kwa nini alipokuwa katika kikosi cha Stars aliishia kukimbia ovyo uwanjani, lakini katika mechi zote anazoichezea klabu yake ya Azam hatoki bila ya kumtungua kipa, jambo linalofanywa pia na Messi akiwa na Barcelona huku akishindwa kuisaidia Argentina?

Hata hivyo, uwezo huo wa kupachika mabao wakiwa na timu zao za Azam FC na Barcelona unaelezwa kuwa hukosekana kutokana na kusimama na wachezaji tofauti uwanjani.

Wakati Messi akiwa na kina Xavi Alonso, Cesc Fabregas, Andres Iniesta, Xavi Hernandez au Alexis Sanchez anapokuwa na Barcelona na kunolewa na kocha Pep Gurdiola; pale anapoichezea Argentina huwa na wachezaji kama Carlos Tevez, Javier Pastore, Angel Di Maria, Sergio Aguero na kadhalika.

Aidha, Boko anapokuwa na Azam FC hushirikiana na kina Kipre Tchetche, Abdi Kassim, Abdulhalim Humoud, Gaudence Mwaikimba, Salum Aboubakar na wengineo; lakini katika kikosi cha Stars alikuwa akicheza na Nizar Khalfan, Henry Joseph, Thomas Ulimwengu, Nurdin Bakari, Mwinyi Kazimoto na kadhalika, kule ambako pia alikutana na kocha tofauti na John Stewart.

Hivyo ndivyo Lionel Messi anayezichezea Barcelona na Argentina anavyofanana kwa kiasi kikubwa na John Boko wa Azam FC aliyejiuzulu kuichezea Tanzania.

By Jamhuri