Waraka wa wanafunzi elimu ya juu nchini (1)

Ufuatao ni waraka wa wanafunzi wa elimu ya juu nchini kwa Serikali, kuhusu migomo na maandamano ya mara kwa mara hapa nchini. Umeandikwa na jopo la viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu na wameupeleka serikalini. Wanatoa ushauri maridhawa wa namna ya kukomesha migomo kwa kuboresha sekta ya elimu, hasa kwa kuwapa fursa wanafunzi wote bila ubaguzi. Waraka huu ni mrefu na JAMHURI itauchapisha wote kuanzia leo. Endelea…

Tunapenda kuchukua fulsa hii kwanza kuomba msamaha na kuwataka radhi wazazi wetu mliotutuma kwenda kutafuta elimu vyuo vikuu hapa nchini, kutokana na vurugu, migomo na maandamano ya mara kwa mara.

Mambo hayo mmekuwa mmekuwa mkiyasikia au mkiyaona kupitia vyombo vya habari yakitokea katika vyuo mbalimbali hapa nchini.

Pia tunaomba radhi kutoka mioyoni mwetu kwa walimu wetu (lecturers) kwa adha inayowakuta inapotokea migomo na maandamano.

Pia tunawaomba msamaha viongozi wetu wa dini ambao kwa namna moja ama nyingine, wamekuwa wakitulea kiroho na kimaadili. Lakini tutakuwa hatujawatendea haki Watanzania ambao kodi zao ndizo zinazogharamia elimu yetu hapa chini.

Bila shaka walitarajia kutuona tukisoma kwa bidii na kufaulu vuzuri, ili tutakaporudi katika jamii zetu tutumie elimu tuliyoipata kuwakomboa Watanzania wenzetu, ambao hadi sasa wanalia na kuangamia na vita kubwa ya Ujinga, Umaskini, Maradhi na Ufisadi, lakini wameendelea kushuhudia migomo na maandamano ya mara kwa mara yasiyo na kikomo.

Baada ya kutafakari kwa kina kama wasomi, tukaona kama hatutakaa chini na kufanya utafiti (research) wa vyanzo na sababu zinazotufanya tuwe na migomo, tuandamane na kufanya vurugu za mara kwa mara vyuoni.

Hatutaeleweka na tutaonekana kweli sisi ni wahuni, au tunatumiwa na watu ama wanasiasa wakati hizi ni tuhuma ambazo hazina ukweli hata chembe ndani yake.

Lakini tunapenda kuwataarifu viongozi wetu, wazazi na Watanzania kwa jumla, kwamba matatizo haya yanatokana na vitendo vichafu vya baadhi ya watumishi pamoja na sera mbovu za kikandamizaji, kibaguzi, manyanyaso na uonevu uliovuka mipaka kwa wanafunzi wa elimu ya juu (vyuo vikuu).

Na hatutaeleweka kwa walimu wetu waliojitolea kwa uzalendo wao wa hali ya juu, kutufundisha japo masilahi yao ni madogo ukilinganisha na kazi kubwa wanayoifanya.

Pia kama tungekaa kimya, viongozi wetu wa dini ambao ni walezi wetu wa kiroho na maadili wasingetuelewa. Vilevile hatutaeleweka zaidi kwa Watanzania ambao wanatozwa kodi kwa ajira ya kugharamia elimu yetu ya juu, ili tusome kwa bidii ili turudi kulitumikia taifa.

Tumefanya utafiti huu wa migomo, vurugu na maandamano ya mara kwa mara, ili tutoe taarifa ya upande wa pili wa wanafunzi, kwani kumekuwa na desturi au utamaduni wa vyuo kutoa taarifa zisizokuwa na ukweli kwa wananchi (umma), kwa kuwasingizia wanafunzi kwamba wanatumiwa na viongozi wa siasa kufanya fujo, vurugu na migomo matatizo haya yanapojitokeza.

Taarifa hizi zisizokuwa na ukweli zimekuwa zikitolewa na baadhi ya watawala wa vyuo, ili kukwepa kutekeleza madai yetu ya msingi kwa kisingizio hiki kisicho na ukweli ndani yake, kama ilivyonekana katika gazeti la Mtanzania toleo namba na 5842 la Jumapili Januari 15, 2012.

Kuna makala yenye kichwa cha habari kilichoandikwa kwa herufi kubwa na kusomeka: Vurugu UDSM: Uongozi wa chuo wadai waliofukuzwa ni wanasiasa.

Habari kama hiyo ilichapishwa katika gazeti la Uhuru ilisomeka, “Vurugu za: Chama cha … cashukiwa kuwa nyuma ya mgomo’. Gazeti la Mzalendo la Januari 15, 2012 lilikuwa na makala yenye maudhui kama hayo.

Kwa bahati mbaya, kwa upande wa wanafunzi hatukupata nafasi ya kukanusha madai hayo kwa ushahidi wa wazi kwa wazazi, walimu, viongozi wetu wa dini na Watanzania waliolipa kodi zinazotusomesha, wakaamini madai yaliyotolewa na Serikali na utawala wa chuo kuwa ni sahihi.

Wakatuhukumu na kuwafukuza chuo wenzetu kwa kutuhusisha kutumiwa na vyama vya siasa, kitendo ambacho si kweli. Walifanya hivyo ili kukwepa na kupinga hoja na madai yetu ya msingi kwa majibu mepesi eti tumetumwa, ni ajabu kweli!

Namna hii siasa zinavyoingizwa katika chuo, matokeo yake chuo kinakuwa sehemu ya kisiasa, jambo ambalo si sahihi. Chuo ni taasisi inayojitegemea, hivyo inapaswa kuendesha mambo yake bila kuingiliwa na taasisi nyingine.

Hali hii ikiachwa iendelee kama Serikali haitatekeleza mapendekezo yetu ambayo ni njia sahihi ya kupunguza vurugu, migomo na maandamano, vyuo vikuu nchini kama siyo kumaliza kabisa, tutaomba wazazi wetu, walimu wetu na Watanzania walipa kodi mtuelewe kwa uamuzi mgumu tutakaochukua kama itakavyoonekana inafaa.

Lakini vyuo vikuu vitapoteza sifa yake ya ndani na nje ya nchi. Vitabaki ni vyuo vya migogoro ya migomo, vurugu na maandamano miaka nenda rudi.

Kufukuza wanafunzi si mwarobaini wa tatizo kwani maandamano, vurugu, migomo itaendelea kuwapo endapo madai na mahitaji ya wanafunzi hayatatekezwa.

Yapo madhara makubwa ambayo yanatokana na migomo vyuoni, yakiwamo ya kuharibiwa kwa rasilimali za chuo, kuharibu ratiba za masomo, Serikali kuingia hasara na gharama za ziada chuo kinapofungwa kwa mgomo, kwani bajeti ya chuo inakuwa ilishapitishwa, na gharama za kupeleka polisi na magari ya maji ya kuwasha na mabomu ya machozi zinakuwa mzigo.

Kibaya zaidi ni kwa wanafunzi kufukuzwa na kusimamishwa masomo, ambao wamegharamiwa na kodi za Watanzania wakitarajiwa kuhitimu na kurejesha mikopo na kulitumikia taifa letu.

Tunaomba wazazi, walimu, viongozi wetu wa dini na Watanzania walipa kodi, kwa pamoja mtumie fursa hii kuishauri Serikali kutekeleza mapendekezo yetu, ili kuinusuru sekta mama ya elimu nchini isiyumbe na kuporomoka kwa kasi ya ajabu.

Ni matumaini yetu kila kundi litatumia nafasi yake kuishauri Serikali kupokea mapendekezo yetu.

Ili binadamu aweze kuzikabili changamoto za maisha na kujikomboa katika lindi la umasikini, lazima awe na elimu. Elimu ndiyo msingi wa kujitambua, kuyatawala na kuyatumia mazingira anamoishi binadamu ili kuboresha maisha yake na kujiletea maendeleo ya haraka.

Ni wazi kuwa elimu ndiyo ukombozi wa binadamu kuiona kesho iliyo bora zaidi na kuogelea katika bahari ya utandawazi, ambayo inamtaka kila mmoja aogelee kwa namna awezavyo.

Kwa kutambua ukweli huo, Serikali ya Tanzania imetoa fursa kwa wadau wa elimu kuwekeza katika sekta hiyo, ili kujenga taifa la watu wenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kuzalisha.

Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA) pamoja na Sera ya Elimu na Mafunzo, vyote vinaeleza umuhimu wa elimu ili kuiwezesha nchi kusonga mbele.

Watanzania na wazazi kwa ujumla wanatarajia kuona watoto wao wanapata maarifa na uwezo, ili wachangie juhudi za Watanzania na wazazi wao kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Wanafunzi wenye maarifa na ujuzi huwa na uwezo wa kufanya mambo mengi mapya kwa usahihi na kuwaongoza wenzao. Katika maendeleo ya ukweli katika jamii tunamoishi, matendo ya wasomi, kazi zao, majukumu yao na shughuli wanazofanya zinapaswa kudhihirisha matunda ya elimu waliyonayo.

Zao muhimu la elimu kwa mtoto ni kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri kwa makini. Uwezo huu ndiyo unaohitajika sana katika jamii ya leo. Mtu mwenye uwezo wa kufikiri ndiye mwenye nguvu ya kuibua dhana mpya na kutafuta njia mbadala za kutatua matatizo.

Watu walioibua teknolojia tulizonazo waliongozwa na upeo wa kufikiri ndipo wakaibuka na dhana mpya. Tendo la kufikiri lipo ndani ya akili na utashi wa mtu. Bila kufikiri matokeo ya juhudi za mtu mara nyingi huwa anguko au hasara.

Serikali pamoja na wadau wa elimu nchini, wana mchango mkubwa wa kuibua taifa la wasomi na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, MKUKUTA na Sera ya Elimu na Mafunzo ambavyo vyote vinaeleza umuhimu wa elimu ili kuiwezesha nchi kusonga mbele.

Kukua kwa uchumi pamoja na mambo mengine hutegemea uwekezaji hasa wenye manufaa kama elimu, ili kupata wataalamu ambao ndiyo watakaoinua uchumi wetu. Kimsingi, uchumi hauwezi kukua bila wasomi. Nchi lazima iandae rasilimali watu wanaohitajika ili kuinua uchumi wa nchi yetu na kusaidia familia zao masikini.

Rais wa Kwanza wa Tanganyika (Tanzania Bara) aliwahi kusema maneno yafuatayo katika hotuba zake kwa wananchi kwamba: “Hakuna Serikali yoyote duniani inayowawekea wananchi wake hela mfukoni, bali “the only best way to enrich a poor people is to educate their children” yaani njia pekee ya kuwasaidia wananchi masikini ni Serikali kuwasomeshea watoto wao.

Kwa hili alikusudia kwamba ukimsomesha mtoto wa maskini, atakapopata hiyo elimu ataitumia kuinua familia yake kiuchumi na taifa kwa jumla. Ndiyo maana baada ya kupata Uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alitambua maadui watatu- Maradhi, Umaskini na Ujinga.

Lakini ili ukabiliane na maadui hawa, lazima uanze na adui ‘ujinga’ kwa kutoa elimu bora kwa wananchi ili waondoe umasikini na maradhi. Lakini tumeshuhudia Serikali kwa sasa inavyosuasua katika sekta hii muhimu ya elimu nchini.

Katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 9 kifungu kidogo cha (i), inasema hivi: “Matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umasikini, ujinga na maradhi.”

Kama tulivyosema, baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, na baadaye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Mwalimu Nyerere alitangaza vita kwa maadui watatu – Ujinga, Maradhi na Umasikini.

Mwalimu alihakikisha anafanikiwa katika mapambano hayo. Alianza kuweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukazia elimu ili kufuta ujinga, kupatikana madaktari wa kupambana na adui maradhi na wataalamu wa uchumi wa kupambana na adui umasikini.

Fikra hii ya Mwalimu ilidumu hadi kufikia maziko ya Azimio la Arusha na kuanzishwa Azimio la Zanzibar Februari 1991 lililoamua kufuata mfumo wa kibepari uliokusudia kumilikisha rasilimali ya Tanzania kwa wachache.

Baada ya hapo, maadui hawa waliwavamia Watanzania. Ujinga ulianza kuongezeka (idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika iliongezeka), maradhi yakaongezeka – vifo kwa mama na mtoto; uchumi ukadorora, umasikini ukaongezeka, shilingi ya Tanzania ikashuka thamani siku hadi siku huku mfumuko wa bei ya bidhaa ukiwaumiza wananchi wa kipato cha chini.

Hilo ndilo Azimio la Zanzibar.

Itaendelea