Alasiri ya Aprili 12, 1984 wakati huo nikiishi Kurasini Highway, nilivuka barabara kwenda Kurasini Shimo la Udongo kuchukua picha zangu za passport kwenye studio moja.

Jina la hiyo studio silikumbuki, maana miaka 35 ni mingi, lakini nakumbuka ilikuwa karibu na duka maarufu la ndugu mmoja aliyeitwa King Nose, jirani na Mti Mpana.

Nilipovuka barabara na kuyakaribia maduka ya eneo hilo, nilishitushwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wamesimama kwa wingi kando nje ya maduka – wakisikiliza taarifa iliyoonekana si ya kawaida. Hapa ikumbukwe kuwa njia pekee kuu za mawasiliano kwa wakati huo zilikuwa magazeti, redio na barua. Hapakuwa na televisheni wala mitandao ya kijamii tunayoishuhudia katika ulimwengu wa leo.

Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ikawa inapiga wimbo wa taifa. Kwa kawaida wimbo wa taifa ukipigwa kwa miaka ile kila mtu alisimama na kukaa mkao wa kupokea jambo lisilo la kawaida. Ni wimbo ulioheshimika mno.

Baada ya ule wimbo ikasikika sauti ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akisema: “Ndugu wananchi, leo saa saba mchana, ndugu yetu na kijana wetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Edward Moringe Sokoine, alipokuwa akisafiri kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake ilipata ajali. Amefariki dunia!”

Bila shaka hii ndiyo hotuba fupi kuliko zote zilizowahi kutolewa na Mwalimu Nyerere wakati wote wa uongozi wake.

Maneno hayo ya Mwalimu yaliwagusa watu wengi. Hapo nilipokuwa watu walianza kuangua kilio. Wananchi wengi walilia kweli kweli. Tuliambiwa hali ilikuwa hivyo kwa nchi nzima. Ulikuwa ni msiba mkubwa kwa taifa baada ya ule wa Sheikh Abeid Amani Karume mwaka 1972.

Mwili wa Sokoine ulisafirishwa hadi Dar es Salaam na kupelekwa moja kwa moja Ikulu. Mwalimu hakuvumilia. Yeye na Mama Maria walimwaga machozi kwa uchungu mkubwa.

Miaka 35 baada ya kifo cha Edward Moringe Sokoine, alama ya uongozi wake bado ipo. Alipendwa mno na wanyonge kwa sababu alikuwa mtetezi wao.

Kuna wakati nilizungumza na mzee Joseph Butiku, aliyekuwa msaidizi wa Mwalimu. Butiku anaeleza tabia za kazi za Sokoine kwa namna ambayo si rahisi kuamini.

Kwa mfano, anasema Sokoine alipokuwa na jambo, aliliandaa na kwenda ofisini kwa Mwalimu mapema asubuhi. Hapo alimsubiri Mwalimu aingie ofisini, na yeye akiwa na faili lake mkononi alimfuata Mwalimu kumweleza nini alichoamini kilikuwa kinapaswa kufanywa kwa masilahi ya nchi.

Japo watu wanafahamu kuwa Mwalimu alikuwa mtu mwenye msimamo kwenye mambo aliyoyaamini, Sokoine anaelezwa kuwa alikuwa zaidi!

Sokione alikuwa wa kwanza kuingia na wa mwisho kutoka ofisini. Alisafiri huku na huko nchini kote kuhimiza shughuli za maendeleo. Alichukia dhuluma na aina zote za unyonyaji kwa mtu mmoja mmoja hadi katika ngazi ya taifa. Alianzisha na kufanikisha vita ya uhujumu uchumi. Matajiri walioficha fedha walizitupa wenyewe mitaani, mabondeni na pwani. Hakuwa na mzaha hata kidogo.

Alikuwa mwana mageuzi. Alisaidia sana kumbadili Mwalimu hata akaanza kukubaliana na ujenzi wa sekta binafsi. Aliamini serikali pekee isingeweza kutoa huduma za kijamii kwa umma wote. Sokoine anakumbukwa kwa kuhimiza kuwapo kwa maduka ya watu binafsi; na usafiri – hasa usafiri wa daladala katika Jiji la Dar es Salaam na baadaye katika miji mingine.

Tofauti na viongozi wengi wa leo, Sokoine hakuwa kiongozi wa kumwonea mtu.

Kazi alizofanya za kupambana na wahujumu uchumi ndizo zilizowaaminisha baadhi ya watu kuwa huenda kifo chake kilipangwa, lakini Mwalimu alijitokeza hadharani na kusema mwanamapinduzi huyo mzalendo alikuwa amekufa kifo cha ajali ya kawaida. Hata hivyo, hadi leo wapo wanaoamini kuwa kifo chake kilikuwa na “mkono wa watu”.

Tunapokuwa kwenye wiki ya kumbukizi ya kifo cha mzalendo huyu, hatuna budi kuyarejea yote mema aliyoyafanya kwa ajili ya manufaa na ustawi wa nchi yetu.

Tunapaswa kuwa na kina Sokoine wengi, lakini hawa hawatapatikana kama nchi itaendelea kukosa ‘jando’ na ‘unyago’ – kuwaandaa viongozi wa baadaye wa taifa letu.

Pale mkoani Morogoro ambako kulitokea ajali iliyogharimu uhai wake, panapaswa patengenezwe kwa namna inayoendana na hadhi yake. Kwa hali ilivyo sasa ni kama mahameni.

Viongozi wengi wa sasa, hasa vijana, wana kila sababu ya kusikiliza hotuba na kusoma maandishi ya Sokoine ili kuchota mengi kutoka kwenye hazina ya mzalendo huyu. Mungu ampuzishe kwa amani.

Please follow and like us:
Pin Share