Kuna jambo ambalo limezungumziwa bungeni na kunifanya nihisi furaha iliyopitiliza. Jambo hilo ni kwamba wanandugu ndio wanaochangia kwa kiasi kikubwa kosa la watu kuwabaka hata dada zao na wakati mwingine binti zao, pia kuwatelekeza watoto wanaotokana na unyama huo wa hatari!

Itakuwa ni jamii ya aina gani tuliyomo tunapoyaacha majanga ya aina hiyo yaendelee kutamalaki ndani yake! Tulizoea kusema haya ni mambo ya kinyama, lakini ieleweke wanyama wanafanya mambo ya uadilifu kuliko binadamu. Mfano, wanyama hawajawahi kufanya mambo yaliyo kinyume cha maumbile kama vile kulawiti, kuharibu mimba makusudi na kadhalika.

Kosa hilo la kuulinda uovu wa aina hiyo linaendelea kukua na kuzidi kukomaa ndani ya jamii yetu kutokana na wanadugu kuliona na kulificha kinyemela  ili kuwatunzia siri wahusika.

Kwa mantiki hiyo, naona wanyama ndio wangekuwa wanadai kutofananishwa na binadamu, kutokana na sisi binadamu kushindwa kuyatunza maadili yetu!

Hivi kweli upo umuhimu wa kuitunza siri ya mtu kumbaka mwanae au dada yake? Mtu anafanya mapenzi na dada yake au binti yake, tena wakati mwingine kwa nguvu, mnaamua kunyamaza eti kwa kutunza siri, kweli hayo ni maadili!  “Bhose manzi ga nyanza’, kama alivyosema Mwalimu Julius Nyerere kuhusu mtoa rushwa na mpokea rushwa?

Eti kulinda siri, hizo ni siri gani za kishetani? Hata kama muathirika si mtu wa ndani ya familia moja, kwa maana ya binti wala dada, haifai kuachwa hivi hivi kwa madai ya kumtunzia siri mhusika. Ina maana hata mnyama mkali, tuseme simba au chui anaweza kuingia mtaani na kuanza kuwatafuna watu lakini watu wa eneo husika wakanyamaza ili kumtunzia siri!

Ieleweke kwamba  mtu anayemlala binti yake au dada yake hana tofauti hata kidogo na simba au chui aliyeingia mtaani kufanya vurumai. Tungekuwa waadilifu waliokamilika, mtu wa hivyo anapaswa apigwe risasi anapoonekana bila hata  kusubiri polisi.

Mfano yupo mama mmoja anayesimulia alivyobakwa na  mwanamume mmoja katili sana kijinsia. Anasema mwanamume huyo alimtuma ndugu yake wa kike akamuite mama huyo ambaye walikuwa marafiki na yule aliyetumwa.

Aliyetumwa alimshawishi huyo rafiki yake waende kumtembelea kaka yake, walipofika kwa mwanamume huyo wageni hao wakapewa mvinyo, baadaye aliyetumwa akaanza kukonyezana na mwenyeji wao, kisha akajifanya anaitwa nje, akatoka nje na kutokomea akiwaacha wawili hao, kaka yake na rafiki yake.

Anaongeza kwamba ndiyo ilikuwa siku ya kwanza yeye kunywa mvinyo, alijisikia anaishiwa nguvu bila kujua kuwa mvinyo ulikuwa unalewesha.

Kilichofuatia mwanamume akamrukia huyo mgeni mithili ya simba anayemrukia pundamilia na kumuingilia kinguvu, kwa vile mama huyo alikuwa anafanyiwa tendo hilo kwa mara ya kwanza, ikabidi damu nyingi imtoke, mara baada ya tendo mwanamume akamfungia ndani mama huyo na kwenda kuita mabinti wa kumsaidia.

Kumbe wakati wa ubakaji huo mama huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa bado bikira, alipata mimba. Alipopimwa na kujulikana kuwa ana mimba, mwanamume aliyehusika akataka waitoe mimba hiyo lakini mama huyo akakataa. Baadaye akajifungua mtoto wa kike.

Wakati huo ilikuwa mwaka 1988, miaka 31 iliyopita. Binti aliyezaliwa kwa sasa ana miaka 30 na tayari binti huyo ana watoto watano. Lakini anashangaa baba yake hajawahi kumpeleka kwao hata walau kumtambulisha kama mmoja wa watoto wake!

Hivi kutokana na muda uliopita kuwa mrefu, baada ya tendo,  ni sahihi kwamba binti huyo hapaswi kupaelewa nyumbani kwao? Au mama aliyebakwa kutopaswa kusema lolote kuhusiana na kitendo hicho cha kinyama? Muda unahalalisha kitendo kama hicho cha kinyama kiwe safi na kitakatifu? Wanasheria wa Haki za Kinamama na Watoto wanasemaje kuhusu suala hilo?

Kwa kiasi kikubwa jambo hilo limetunzwa na wanadugu, wanaona itakuwa aibu kubwa kulisema, wapo wanaodai kuwa binti aliyezaliwa kutokana na ukware wa baba yake ni bora apotelee huko kusikojulikana na wanandugu wanaona anayejaribu kukumbushia jambo hilo ndiye adui anayepaswa kuangamizwa!

Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema kuwa ikibidi ataanza kutoa orodha ya wabunge wenye kashfa za aina hiyo. Nadhani asiwasahau watu kama huyu mwanamume katika kuitendea haki jamii nzima.

Mama mhusika yupo na anaweza kutoa maelezo yote ikibidi, isije kuonekana kuwa haya ni maneno ya kusadikika. Pia binti aliyepatikana kufuatia unyama huo yupo.

[email protected]

0654 031 701 / 0784 989 512

Please follow and like us:
Pin Share