Mwanadamu ana uwezo wa kufikiri na kuamua kutenda jambo zuri au baya. Anaweza kujifanyia haya binafsi, kuwafanyia wanadamu wenzake na viumbe vyote vilivyomo katika ulimwengu huu, kwa nia tu ya kuridhisha nafsi yake. Na hapa ndipo yanapoanzia maelewano na mifarakano baina ya wanadamu.

Uwezo alionao mwanadamu huyu unampa kiburi kutii au kutotii jambo, kukiuka kanuni na taratibu alizojiwekea na zile alizoandaliwa na kukabidhiwa na Mwenyezi Mungu ambazo ndizo zenye nguvu zaidi na amali njema kuliko za kwake. Hata hivyo bado ana majigambo na majivuno kwa kutumia uwezo huu kwa viumbe vingine.

Mwanadamu anazo fikra mbili. Fikra nzuri na fikra mbaya. Fikra nzuri inatengeneza na fikra mbaya inaangamiza. Anapozitumia fikra hizi, ukweli anajitengenezea tabia. Tabia ni hali ya mazoea ya kufanya jambo fulani. Nazungumzia desturi, mazoea na mwenendo.

Maelezo hayo yanatufahamisha msingi wa tabia ni fikra, na mazoea ni matunda ya tabia ya mwanadamu. Kwa hiyo matendo mazuri au mabaya asili yake ni fikra za mwanadamu jinsi anavyozitoa na anavyoziwasilisha kwa wanadamu wenzake.

Pili, jinsi fikra hizi zinavyopokewa na zinavyotekelezwa kwa mapana yake.

Shauku au tamaa ya kufanya kazi, kuzembea jambo, kupata kitu, kumiliki mali, kushika madaraka, kufanya fujo au uasi, kujeruhi au kuua ni baadhi ya matendo yatokanayo na fikra unazozitengeneza akilini mwako. Busara inahitajika katika kuchagua fikra ipi ni njema na yenye manufaa: na ipi si njema kwa mwanadamu.

Leo, mwanadamu kwa kujiamini ni kiumbe mwenye uwezo wa kufikiri na kufasili fikra zake katika matendo mbalimbali, anajikuta akibadili, akiboresha na akiharibu mazingira yake na bado akijisifu ni kiumbe bora na mfalme wa ulimwengu. Ama! Hakika yeye si mfalme wa ulimwengu. Mwenye ufalme huo ni Mwenyezi Mungu peke yake.

Hata kama haamini na kukataa kuwapo kwa Mwenyezi Mungu, naye mwanadamu ndiye mwenye uwezo wa kubadili mazingira ya eneo au kitu, kutokana na uwezo wake, huku akiamini fikra zake ndizo chanzo, basi, ni hekima akatambua asili ya fikra.

Samahani. Sitaki kuzungumzia ‘UDHANIFU na UYAKINIFU’ si  mahali pake. Itoshe kutamka kwamba mwanadamu ana kiburi na si mfalme wa ulimwengu. Lakini ikumbukwe na kuzingatiwa mwanadamu ni kiumbe chenye akili na uwezo mkubwa kufikiri na kutenda. Ana silika. Viumbe vingine havina nafsi ya kujitambua.

Bado sina uhakika ni uwezo au kiburi ama vyote viwili ndivyo vinavyompa jeuri kusema na kutenda mambo bulibuli au shaghalabaghala. Katika kufanya hivi mwanadamu amefuzu kuweka ulimwengu katika makundi matatu. Makundi ambayo kila moja linamtazama mwenzake kwa hadhari kubwa.

Kundi tulivu na salama. Hili ni kundi makini. Kundi la pili ni la unyang’anyi na vita. Ni kundi dogo kuliko la kwanza lakini linatetemesha na linasumbua wanadamu. Kundi la tatu ni la shaka na wasiwasi. Hili ni kundi la wastani. Lina vuruga mikakati, linajenga hoja ya nguvu na lina vuruga vikao, mijadala na mazungumzo ya kundi tulivu na salama.

Angalia yanayotokea katika nchi mbalimbali huko Ulaya, Asia  Latini Amerika na Afrika. Chungulia ndani ya vikao vya serikali, taasisi ( mabunge) na vyama  vya siasa na kwenye vyombo vya utekelezaji wa haki, na vya usimamizi wa usalama wa wanadamu.

Mwanadamu anatumia fikra zake kuyumbisha na kugonganisha mihimili ya dola. Serikali, Bunge na Mahakama. Anapitisha fikra katika mitandao mbalimbali kwenye mkonga wa  mawasiliano. Nina shaka iwapo vyombo vya habari vitanusurika kutokana na tabia ya mwanadamu.

Nashauri na kuomba vyombo vya habari visije kutumbukia kwenye mtego wa panya. Natambua vyombo vya habari si mitambo, kalamu na karatasi. Hizi ni zana za kufanyia kazi. Vyombo vya habari ni wanadamu waliomo ndani ya vyombo hivi. Fikra nzuri ndiyo mwongozo, dira na maono ya usalama, haki, usawa na umoja wa taifa au nchi.

Please follow and like us:
Pin Share