Naanza na salamu kama ilivyo kawaida yangu, naamini huo ni moja ya uzalendo ambao tumekuwa nao kama watoto wa Tanganyika mpaka ikawa Tanzania huru. Salamu inakufanya umtambue mzalendo mwenzako na kumtambua kama yuko salama na uko mikono salama kama mmekutana barabarani.

Nakumbuka enzi hizo tukihisi tu kama si mwenzetu kwa hatua ya salamu tu, tunaanza kwa kukuomba barua ya mwenyekiti wa TANU wa kijiji ulichotoka.

Kwa uzalendo zaidi tukipata barua husika na kujiridhisha kuwa wewe ni mzalendo mwenzetu, utapata mlo, maji ya kunywa na kuoga, utapata malazi na ulinzi wa kutosha hadi utakapoondoka. Enzi hizo tulikuwa na mashamba ya ushirika hivyo hata wazalendo wenzetu wageni kama walikuwa na muda mwingi wa kukaa kijijini kwetu, basi walishiriki kikamilifu katika zoezi la kilimo au upaliliaji au uvunaji wa shamba la ushirika wa kijiji.

Nimekumbuka haya leo hasa kutokana na hali ilivyo sasa hivi, kwamba ni vigumu kumtambua mzalendo mwenzio, iwe kwa salamu au maisha yake. Hii ndiyo Tanzania ambayo ningependa niizungumzie leo kwa umri wangu kiasi cha kuomba kama Tanzania ni basi la abiria, naomba nishushwe, maana kasi yake inakinzana na uwezo wangu wa kuifikiria safari yenyewe.

Tangu tupate uhuru, najua kwamba huu ni mwongo wa sita, yaani miaka sitini hivi, kizazi kile cha kabla ya uhuru wengi wetu wametangulia mbele ya haki, tumepata bahati watu wachache sana kuendelea kuona kasi ya maisha ambayo hatukuwahi kufikiria enzi zile za ujana wetu kwamba kuna siku nchi itakwenda kasi kuliko sisi.

Nchi hii imepata uhuru ikiwa na watu wachache sana na bajeti yetu ya kwanza kama hujui, basi ni sawasawa na fedha anazotembea nazo mtu mmoja kwenye mfuko wa suruali leo hii, ni bajeti ambayo ilikuwa na mambo mengi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa shule na zahanati, ujenzi wa viwanda vikubwa na vile vidogo, maarufu SIDO.

Sitaki kukumbuka tulikotoka, naona kizunguzungu kabisa, kwamba leo mtu anaweza kutoka kaskazini hadi kusini mwa nchi kwa siku moja, kwamba leo unaweza kupiga simu moja kwa moja kwa mhusika bila kupitia Posta, kwamba leo unachagua aina ya usafiri wa kwenda mahali na si kwamba unapangiwa? Kwamba leo demokrasia imefika mahali tunaweza kubishana kwa hoja tofauti na zamani ambapo fikra za mwenyekiti zilikuwa ndiyo hatima ya kila jambo. Jamani kwa kweli naomba nishuke. Huu mwendo siuwezi.

Najua kwamba nataka kuwa wa zamani lakini ukweli utabaki pale pale kwamba mambo mengi yanayokwenda haraka kiasi hiki yanafanya tushindwe kujua lipi ni jambo bora kwa jamii yetu na lipi ni baya, watu na maisha wote wanazongana kiasi cha kufanya jambo gumu kuwa jambo rahisi, jambo la utekelezaji linakuwa siasa uchwara na jambo la kijinga linapewa nafasi zaidi kuliko jambo la maana.

Niliwahi kuandika hapa kwamba iwapo hatutakuwa makini, nachelea kuona mambo ya maana kuwa ya kijinga, wapo walionikataza kwa maana ya kunitukana juu ya kuonekana mzee na nimepitwa na wakati katika kutoa mawazo yangu, lakini bado nitasimama na imani yangu kwamba sasa tunahitaji zaidi marejeo ya zamani kuliko tunavyohitaji mambo mapya ya kileo.

Katika hili nahisi umuhimu wa kujali mavazi yetu ya zamani na heshima zake, katika hili nawaona mabingwa na wawakilishi wa kweli wa enzi zetu, katika hili nawaona watumishi waliotukuka wa enzi hizo za zamani ambazo wengi wetu tunazifubaza kama hazina maana, nauona utamaduni na desturi yetu enzi hizo na mwisho nauona uzalendo wa kweli pasi na huu wa kizazi kipya.

Inawezekana kweli ndiyo maendeleo lakini napata taabu kila ninapopitia njia ya mkato katika maendeleo hayo, sioni maendeleo ya kugawa kazi za sanaa kama sehemu ya ajira rasmi na hasa kwa mtu mwenye nguvu zake, nachelea kuona siasa ni kazi badala ya kuwa siasa ni kilimo kwa maana ya azimio letu la Musoma.

Nadhani tunatakiwa kujitafakari tunaruka wapi ili twende wapi na kwamba hatima yake itakuwa ipi, kuna siku nchi hii tutakuwa na maendeleo na kuuza bidhaa kama filamu, vichekesho, siasa, nyimbo, usanii na kdhalika badala ya bidhaa na mazao.

Si kweli kwamba nchi yetu ina uhaba wa kutafuta rasilimali zingine kwa kuwa hatuna ardhi, uongozi na watu.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

Please follow and like us:
Pin Share