Kicheko cha maji Kitongoji cha Oldonyoogol

 

Maji ni miongoni mwa kero kubwa zinazowakabili maelfu ya wananchi wilayani Ngorongoro.

Kwa kutambua kuwa wananchi wa eneo hili ni wafugaji, mahitaji ya maji ni ya kiwango cha juu mno. Jiografia ya Ngorongoro imefanya upatikanaji wa huduma hiyo kuwa mgumu.

Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), kwa kutambua kuwa ina dhima ya kutoa huduma kwa wananchi wanaoishi ndani na nje ya eneo linalozunguka Mamlaka, imekuwa ikitumia kila mbinu ya kisayansi kuhakikisha kuwa maji yanapatikana kwa ajili ya wananchi na mifugo yao.

Japo mpango wa maji umekuwa endelevu, hata hivyo kwa siku za karibuni kazi hiyo imepamba moto. Chanzo cha kasi hiyo ni kutokana na maagizo ya serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupiga marufuku uingizaji wa mifugo ndani ya eneo la kreta ambako kuna maji baridi yanayofaa kwa matumizi ya binadamu, wanyama na mifugo.

Uamuzi wa serikali unalenga kuiokoa kreta hiyo iliyokuwa imeanza kupoteza uhalisia wake kutokana na makundi ya maelfu ya mifugo kuingizwa huko kwa ajili ya malisho na maji.

Kutokana na uamuzi huo, NCAA sasa inachimba mabwawa na visima katika vijiji mbalimbali wilayani Ngorongoro.

Miongoni mwa wanufaika wa mpango huu ni Kitongoji cha Oldonyoogol kilichoko Kijiji cha Meshil, Kata ya Olbalbal, Tarafa ya Ngorongoro. Kitongoji hiki kina kaya 390.

NCAA walianza kuchimba kisima katika eneo hili katika mwaka wa fedha wa 2016/2017; na hatimaye maji yalipatikana Septemba 10, 2019.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Oldonyoogol, Seiyai ole Seyeda, anasema: “Hakika tumefurahi sana. Maji ni baridi sana, yanafaa kwa matumizi ya binadamu na wanyama wa kufuga na wa porini.

“Tunafurahi kwa sababu sasa kina mama wanaondokana na mateso ya kuamka usiku na kutembea umbali mrefu sana kwenda kusaka maji. Walitembea hadi kilometa 20 kusaka maji kwa kutumia punda, shida ilikuwa kubwa sana. Ndoa ziliingia shida.”

Wananchi katika kitongoji hicho walitembea umbali huo mrefu kwenda kupata maji katika eneo la Olng’arwa.

“Hata huko Olng’arwa maji hayakupatikana kama haya, badala yake tulikuwa tunachimba kuanzia hapo hadi Lemuta. Maji yalikuwa ya kusubiri, sasa kwa hiki kisima wananchi wa kule wanaweza nao kuja huku kupata maji safi na salama,” anasema Seyeda.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa NCAA, Bashiru Nchira, ambaye amekuwa akizunguka vijijini kote kusimamia miradi ya kijamii, anasema uchimbaji hadi ufungaji pampu kwenye kisima hicho umegharimu Sh milioni 92. Hata hivyo, kazi anasema bado ni kubwa.

“Huu ni mwanzo tu maana kunatakiwa kujengwe matangi ya kuhifadhia maji, ujenzi wa vibanio kwa ajili ya kunywesha mifugo, uwekaji umeme wa solar na kadhalika. Hadi kazi zote hizo zikamilike zitatumika Sh zaidi ya milioni 500. Huu ni mradi mkubwa,” anasema.

Kwa mujibu wa Nchira, kukamilika kwa mradi huu kutawanufaisha wananchi katika vijiji vya Naspolion, Endulen, Ngorongoro, Ngoile, Olba, Piyaya, Oloirobi na Enokanoka.

“Hapa walikuwa wakifuga mbuzi na kondoo, hawakufuga ng’ombe kwa sababu ya ukosefu wa maji, sasa kwa ujio wa maji mifugo yao itakuwa salama,” anasema Nchira.

Msimamizi Mkuu wa ujenzi wa kisima hicho, Mhandisi Hemed Hussein, anasema: “Urefu wa kisima hiki kwenda chini ni mita 106 [zaidi ya uwanja wa mpira]. Kisima kina uwezo wa kutoa wastani wa lita 7,900 za maji kwa saa. Haya ni maji mengi.

“Kwa bahati nzuri maji ni baridi, hayana chumvi na kwa kweli ni mengi sana.”

Nchira anasema mradi wa maji katika Kitongoji cha Oldonyoogol utakuwa na faida endapo wananchi wataulinda na kuuepusha na aina zote za hujuma.

“Mradi huu umegharimu fedha nyingi, faida zake ni kubwa kwa wananchi, kwa mifugo na hata kwa wanyamapori, maana kuna wakati – ukame unapokuwa mkali zaidi – maji haya yanaweza kutumika kuwaokoa wanyamapori.

“Kumekuwapo matukio kwa jamii nyingine kuhujumu miradi ya aina hii. Tunazungumza na viongozi wa vijiji na wa mila kuhakikisha mradi huu na mingine inayojengwa kwa fedha nyingi sana za umma itunzwe ili ilete faida iliyokusudiwa. Matumaini yetu ni kuona wananchi hawarudi tena kwenye mateso ya kukosa maji, lakini hilo litawezekana endapo watakuwa walinzi wa mradi,” anasema.

Mapema mwaka huu, NCAA ilizindua mradi wa maji wa Sh milioni 231. Mradi huo una malambo mawili na kisima. Kila lambo moja lina uwezo wa kunyweshea ng’ombe  60 kwa wakati mmoja.

Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk. Freddy Manongi, anasema ni jukumu la mamlaka kuboresha maisha ya wananchi, akiamini kuwa uwepo wa mradi huo na mingine ya aina hiyo inapunguza kero ya wafugaji ya utafutaji maji.

Mradi huo pia utapunguza malalamiko yaliyokuwa yanatolewa na watalii wanaozuru ndani ya kreta ambao walikuta mifugo badala ya wanyamapori.

By Jamhuri