Biashara

 

Visa na mikasa ya wajasiriamali kukopa na baadaye kujikuta wakishindwa kurejesha mikopo yao ni vingi sana mahali pote, si tu Tanzania bali duniani kote.
Mikopo imekuwa chanzo cha baadhi ya wajasiriamali na wafanyabiashara kudhalilika, kurudi nyuma kimaendeleo na hata kukimbia maeneo yao. Hata hivyo, huo ni upande mmoja wa mikopo na tena ulio mdogo sana; upo upande wa pili ulio mkubwa, ambao ni faida za mikopo kwa wajasiriamali.
Jambo kubwa la kufahamu ni kwamba mikopo ni sehemu ya biashara. Huwezi kuanzisha biashara pasipo kukopa na huwezi kukua sana kibiashara pasipo mikopo. Biashara zote duniani zilianzishwa kwa mikopo na zinaendelea kuwa na mikopo.
Mtu anaweza kuniuliza, “Sanga, mimi nilianzisha biashara kutokana na fedha zangu za mfukoni, unawezaje kusema nilianzisha kwa mkopo?” jibu ni rahisi. Ukweli ni kwamba kibiashara tunasema kuwa biashara ni ‘mtu’ anayejitegemea; hivyo ukichukua fedha yako kutoka mfukoni na kupeleka katika biashara basi huko ni kuwa umeikopesha biashara.


Tunachokiangalia hapa kwa leo ni mambo matatu; kwa nini ukope, unajipangaje kukopa na unafanya nini kuhakikisha kwamba marejesho ya mkopo yanakuacha ukiwa umeinuka zaidi kibiashara na siyo kudidimia? Hii ni kwa sababu pasipo kuwa makini ni rahisi sana mkopo kugeuka jehanamu badala ya kuwa ngazi ya kuelekea kwenye mafanikio.


Sababu kubwa ya kukopa ni kule kuwa na uhitaji wa mtaji kutokana na kuwa na fedha chache katika mzunguko wako. Hitaji hili huja inapotokea unataka kupanuka ama ikiwa unaona idadi ya wateja ni kubwa ukilinganisha na usambazaji wa bidhaa unaoufanya katika soko.
Hii mikopo ipo ya aina nyingi na inapatikana kutoka taasisi mbalimbali za kifedha — ndogo na kubwa. Kwa kadiri ya malengo ya taasisi husika, kila taasisi huwa na masharti na taratibu zake katika utoaji wa mikopo kwa wahusika. Vile vile kuna taasisi nyingine ambazo siyo za kifedha lakini zinatoa mikopo kwa ajili ya wajasiriamali. Hizi zinahusisha mifuko mbalimbali, programu mbalimbali.


Unapokwenda kukopa ni lazima ujipange vilivyo kuhakikisha kwamba mkopo unaouchukua unaleta tija kwa biashara yako. Usipokuwa makini au ikiwa utakurupuka kuchukua mkopo, unaweza kujikuta unakwama kurejesha mkopo au kama ukifanikiwa kurejesha utakuta hakuna faida yoyote uliyozalisha katika biashara yako. Wajasiriamali wengi huwa wana msemo wao kuwa unakuwa ulikuwa unaifanyia benki. Kabla ya kwenda kukopa ni vema sana ukafanya tathmini ya kina sana kuhusu mwenendo wa biashara yako.
 Kama unamiliki duka usiridhike na ule wingi wa bidhaa zilizopo stoo ama katika mashelfu bali unatakiwa upige hesabu kamilifu kubaini kiwango halisi cha faida unayoipata ama uliyowahi kuipata katika mwenendo wa biashara zako. Usisahau kuwa kuna mtaji na kuna faida; kinachohitajika katika tathmini ya kupatiwa mkopo ni ile faida unayoingiza; kwa maana hutalipa mkopo kwa mtaji bali kwa kutumia faida.


Tunaposema suala la kupiga faida na kufanya tathmini ya mahesabu kwa biashara yako, wajasiriamali wengi huwa hawataki kufanya suala hili. Nawakumbuka wajasiriamali wawili walionifuata; ambao benki walikotaka kuchukua mkopo waliwaeleza kuwa wapeleke michanganuo ya kibiashara.
Wote wawili niliwaeleza gharama ya kuandaa michanganuo hiyo. Mmoja akaniambia hawezi kutoa fedha hiyo kwa sababu ni nyingi mno. Mwingine akakubali kulipa gharama hiyo lakini akanieleza kuwa hitaji lake ni mkopo mkubwa ambao hauendani na mauzo yake, hivyo akataka “tupike” taarifa. Nilimweleza hatari ya kufanya hivyo, akaghairi.


Haya ni matatizo makubwa yaliyopo kwa wajasiriamali wengi; mosi wengi wao ni wabahili wa kutumia gharama kulipia huduma za kitaalamu kwa biashara zao. Hili yawezekana ni tatizo la ule utamaduni wa kuendesha biashara zetu kienyeji.
 Hata hivyo, lazima tuelewe kuwa katika zama hizi ili ufanikiwe huna budi kuendesha biashara kisasa na kwa akili za kisasa. Pili ni kwamba wengi wanapokutana na maafisa wa benki kutathmini mienendo ya biashara zao huwa wanakuwa waongo.
 Ili kupata mkopo mkubwa mtu anataja mauzo makubwa kiasi kwamba anaishawishi benki kumpa fedha nyingi kupita uwezo wake. Kimsingi nia na melengo ya wajasiriamali wengi wanapokwenda kutaka mikopo huwa ni nzuri kwa namna mbili. Moja ni kutaka kupanua ile biashara. Pili ni kutaka kupata fedha kupitia biashara hiyo lakini fedha inayochukuliwa inakwenda kufanya mambo ama biashara nyingine.


Vinginevyo uwe na biashara ama vyanzo vingine vya mapato vinavyotiririka kwako na uvielekeze katika kulipa mkopo wako; kinyume na hapo mkopo uliochukuliwa kwa kutofanya tathmini nzuri ya mwenendo wa biashara ni lazima utakushinda tu. Pia ukichukua mkopo kwa mgongo wa biashara moja na kuupeleka kwingine, omba Mungu mambo yasigome, vinginevyo utajikuta unayumba na kuyumbisha mwenendo wako katika biashara.
Kikwazo kikubwa cha kupatiwa mikopo kwa wajasiriamali wengi huwa kinaonekana ni kukosekana kwa dhamana ambazo huwa ni rasilimali zisizohamishika, kama nyumba, mashamba, viwanja na nyingine. Wengi hudhani kuwa kuwa na dhamana hizi ndio mwarobaini wa kupatiwa mikopo.
Hata hivyo, kwa taratibu za benki nyingi, dhamana ya mali isiyohamishika ni kigezo cha mwisho kabisa kwa mtu kupewa mkopo. Jambo la kwanza wanaangalia, je, una biashara? La pili wanaangalia nidhamu yako katika masuala ya fedha.


Kwenye eneo hili la nidhamu ndipo wataangalia mzunguko wa fedha zako benki wakamini kuwa kitendo cha kuwa na utamaduni wa kuweka, kununua na kulipa kupitia benki kunaonesha unathamini thamani ya fedha na unazingatia utunzaji mzuri wa fedha. Kitu cha tatu wataangalia aina ya biashara yako na mwenendo wake.
Cha nne watataka kujiridhisha, je, ni kweli unahaja ya kukopa? Na kama una haja ya kukopa, je, ni kweli unahitaji kiasi ulichokiomba? Watafanya tathmini kuona ikiwa wakuongezee ama wakupunguzie kiasi ulichoomba. Katika tathmini hii inayofanywa na benki kuna maelezo watayapata wao wenyewe.


Hata hivyo, sehemu kubwa ya maelezo watayahitaji kutoka kwako kisha wao watatumia utaalamu wao kufikia uamuzi utakaokusaidia. Kinachozivutia benki kukupa mkopo ni ustawi wa biashara pamoja na matazamio ya kukua kwa biashara yako hapo mbeleni
Kutoa taarifa za uongo kwa wataalamu wa benki ni sawa na kujidanganya kwa sababu uamuzi utakaofikia utakuwa ni msalaba kwako. Unaweza kutoa maelezo yasiyo sahihi na ukajikuta umepatiwa mkopo mkubwa kuliko uwezo wako ama ukapewa mkopo mdogo kuliko unaohitajika kukusaidia.
Kimsingi natambua kuwa katika zama hizi zilizojaa watu wasio waaminifu, pia kuna maofisa na wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za fedha ambao wanaweza kushirikiana na mjasiriamali kufanya ‘ujanja ujanja’ wa kupatikana mkopo pasipo kuzingatia taratibu njema zilizopo kwenye taasisi za fedha.


Ni kweli kwamba pasipo tathmini yoyote mjasiriamali anaweza kupeleka hati tu ya rasilimali isiyohamishika na akapatiwa mkopo ‘fasta fasta’. Mambo kama haya yamewagharimu wajasiriamali wengi na kujikuta mikopo ikiwashinda. Hata hivyo simaanishi kuwa wote wanaochukua mikopo kwa staili hizi hushindwa kurejesha mikopo, la hasha! Isipokuwa mjasiriamali huna sababu ya kujiweka kwenye mstari mwekundu katika biashara yako.
Semina zangu mikoani zinaendelea. Wiki iliyopita nilifanya semina ya siku tatu mjini Iringa iliyohudhuriwa na watu mbalimbali na niliwasilisha mada tatu; kusimamia ulichonacho, mtazamo katika biashara na namna ya kuibuka na wazo bora la biashara. Ni semina iliyowagusa wengi.

5931 Total Views 4 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!