Na Alex Kazenga, JamhuriMedia, Morogoro

Hifadhi ya Taifa ya Safu za Milima ya Udzungwa ipo kwenye hatua za awali za ujenzi wa njia ndefu ya utalii ipitayo juu ya miti maarufu ‘canopy walk away’ itakayosababisha ongezeko la watalii wa ndani na nje ya nchi; JAMHURI linaripoti.

Mbali na ujenzi wa njia, pia ndani ya msitu uliosheheni miti ya kila aina ikiwamo, minene, miembamba, mifupi na mirefu, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linapanga kwa siku za mbeleni liweka kituo cha watalii kufanya tafakuri ‘meditation’ kwa ajili ya kutafuta amani na furaha ya moyo.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa hifadhi hiyo, Abel Peter akizungumizia mradi wa kujenga njia inayopita juu ya miti alisema itakuwa na urefu wa mita 1000. ambapo ikikamilika itakuwa ya kwanza kwa urefu barani Afrika ikizipita zilizojengwa Rwanda, Ghana na Nigeria.

Nyani wanaopatikana katika Hifadhi yaUdzungwa

“Litakuwa zao jipya la utalii ndani ya hifadhi yetu, njia hii itavuta watalii wa nje na ndani waje kuitembelea Udzungwa. Wakifika watajionea vivutio vya kipekee kama nyani aina mbega wa Iringa na goraga wa Sanje,” anasema Peter huku akiongeza kuwa nyani hao hawapatikani kwingine duniani isipokuwa katika hifadhi ya Taifa ya Safu za Milima ya Udzungwa tu.

Hifadhi ya Milima ya Udzungwa inapatikana katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kwenye safu za milima ya tao la mashariki,ambazo zimeanzia kusini mwa Kenya katika eneo la Taveta na zimeishia Makambako Iringa katika eneo la Ihefu.

Akizungumzia miradi ya utalii na uhifadhi katika milima ya Udzungwa, Peter anasema ni pamoja na ujenzi wa kambi ya kisasa ya watalii maarufu ‘Chui Camp’ na ujenzi wa kituo cha maabara maalumu itakayotumika kufanya tafiti za wadudu wanaopatikana katika milima hiyo.

“Tumepata fedha kutoka benki ya dunia, sisi kama Uduzungwa pia tuna mradi wa kuendeleza utalii kusini mwa Tanzania. Huu mradi wa njia za kupita juu ya miti mwaka huu wa fedha tunategemea ikamilike.

“Mradi haujafikia hatua nzuri ya kuonekana, lakini mkandarasi yuko eneo la kazi anatekeleza kazi ya kusimika nguzo. Lakini pia, tunafanya mafunzo ya kuwazowelesha mbega wa Sanje kuwa karibu ya binadamu ili mradi ukikamilike kasi ya utalii iongezeke,” anasema Peter.

Hata hivyo, anasema watu wanaizungumzia Udzungwa kwa taswira ya maporomoko ya Sanje tu lakini wanasahau kuwa ndiyo hifadhi pekee inayoongoza kwa kuwa na wadudu pamoja na wanyama wa kipekee.

Kwa mujibu wa maelezo yake kuna tafiti zimefanyika hivi karibuni katika hifadhi hiyo ambapo watafiti wamemgundua jongoo wa kipekee ambaye kwa sasa wamempa jina la Udzungwa.

Kware wanaopatikana katika hifadhi hiyo

“Maabara maalumu itakayojengwa itatusaidia kupima na kutambua vinasaba vya wadudu waliopo kwenye hifadhi hii. Mpaka sasa kuna ugunduzi na utambuzi unaendelea kufanyika,” anasema Peter.

Hifadhi pekee iliyopo kwenye safu za milima ya Udzungwa ni Hifadhi ya Udzungwa tu na sehemu zilizosalia ni misitu ya asili kama ulivyo msitu wa Amani uliopo Muheza mkoani Tanga.

Misitu ya asili katika eneo la Kilombero ipo tisa na kwamba kwa upande mkubwa inapatikana katika eneo la Iringa katika wilaya za kilolo na Mfindi huku kwa mkoa wa Morogoro ikipatikana katika wilaya ya Kilombero.

“Hifadhi yetu ni mashuhuli kwa utalii wa kutembea hifadhiNI. Zipo njia kadhaa; njia za kutembea kwenda kwenye maporomoko ya sanje, hii ni njia maarufu inayotumiwa na watalii kwenda kuona maporomoko ya maji.

“Kule juu kwenye maporomoko tuna kambi ambayo tumeiweka kwa ajili ya watalii kukaa na kuona wanyama wanaotembea usiku.

“Zipo kambi nyingine chini ya milima ambazo watalii wanaotaka kuweka kambi kwenye eneo la hifadhi watapata nafasi ya kuona hata wanyama,” anasema Peter huku akiongeza Udzungwa inafikika kwa njia ya barabara na reli ya Tazara.

Mikakati mingine ya kuboresha hifadhi hiyo anasema ni pamoja na kuimarisha njia za utalii ili zipitike vizuri huku ikitaja uwepo wa njia ndefu katika hifadhi hiyo imbayo mtalii anaweza kuitumia kutembea ndani ya hifadhini kwa siku sita.

Njia hiyo inatokea upande wa magharibi mwa hifadhi na kuishia upande wa mashariki na kwamba mtalii akiitumia anaona wanyama kama simba, nyati na tembo.

Maporomoko ya Sanje

Njia hiyo anasema wanalenga kuiwekea mkazo ili ipate wageni akidai kuwa inaunganisha hifadhi ya Udzungwa na msitu wa asili wa Kilombero ‘Kilombero nature reserve’.

“Mradi wa ‘regrow’ limeufadhili ujenzi wa kambi ya kisasa ya Chui, kwa watalii wanaotembelea kambi hiyo wataweza kuingia ndani ya hifadhi na kupanda juu ya kilele kirefu cha milima cha Lomelo Peak chenye urefu wa mita 2548.

“Wakati mtu anaenda kwenye hicho kilele kuna vitu vizuri vingi vya kuvutia, ataona bonde la Kilombero, mapango ya kiasili ambayo watu walikuwa wanatumia kwenye shughuli za kimira.

“Tukiweza vizuri kwenye hayo maeneo, tutafanya watalii wakae muda mrefu. Kilombero nature reserve kuna mnyama anaitwa Kipunjii, huyu yupo kwenye misitu ya Rungwe. Hii ni aina ya nyani wanaovutia. Pia kule utamuona ndege anayeitwa Kware wa udzungwa ambaye anapatikana hapa tu kote duniani,” anasema Peter.

Kwa upande mwingine anamsifia Balozi wa Poland nchini akidai amekuwa mtalii wa mara kwa mara wa hifadhi ya Udzungwa.

Anasema balozi huyo amewahi kuleta watu maarufu katiuka hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na kutengeneza filamu inayoonyesha vivutio vilivyoko kwenye hifadhi hiyo.

“Kwa kipindi chote ambacho amewahi kutembelea hifadhi yetu amekuwa akija hapa kwa njia ya reli akitoea Dar es Salaam.

“Balozi akija hoifadhini anatumia treni ya Tazara na mara nyingi haji peke yake,” anasema Peter.

Anasisitiza Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi kuitembelea hifadhi ya Udzungwa kuona vitu vya kipekee visivyopatikana kwingine isipokuwa katika hifadhi hiyo akiwamo ndege aliyepewa jina la chozi mbawa nyekundu.

Kivutio cha Maporomoko ya maji

Gift Mafulu ni moja wa wanufaika wa mradi wa ‘regrow’ aliyepata mafunzo ya kuongoza watalii katika hifadhi ya safu za Milima ya Udzungwa.

Si mwajiliwa wa TANAPA katika hifadhi ya Udzungwa, lakini shirika hilo linamuwezesha kujipatia kipato kwa kuwaongoza watalii wanaopanda milima kwenda kwenye maporomo hasa ya Sanje.

“Maporomoko ya Sanje yapo ya aina mbili; marefu zaidi na mafupi. Marefu zaidi yana urefu wa mita 170 na haya yanapita kwenye njia yake , mengine ya pili yapo kwenye njia ya maji ambayo imetengeneza maporomoko yenye urefu unaotofautiana. Ya kwanza yana urefu wa mita 70 ambayo yapo kileleni kabisa mwa milima hii,” anasema Mafulu

Na kuongeza kuwa maporomoko mengine yenye urefu wa mita 30 yanapatikana kwenye njia ya maporomoko ya awali yenye urefu wa mita 70.

“Njia inayoelekea kwenye maporomoko yenye urefu wa mita 170 ndiyo inapendwa na wageni wengi kwasababu yalipo panafikika kwa urahisi, watu wanapiga picha na kuogelea,” anasema Mafulu.

Maji yanayoporomoko kwenye mwamba wenye urefu wa mita 170 kwa chini limejitokeza bwawa la asili ambalo watu hulitumia kuogelea na TANAPA imetengeneza sehemu ya kusimama ili kupata picha ya maporomoko hayo.

Baadhi ya maajabu yaliyopo kwenye maporomoko hayo ni pamoja na uasili wa maporomoko hayo kutengeneza taswira yenye mfanano wa ramani ya Afrika suala ambalo huwavutia na kuwastaajabisha wageni wengi.

DC, Mbunge wa Kilombero wanena

Mkuu wa wilaya ya Kilomero, Dastan Kyobya anasema suala la utalii ndani ya wilaya ya Kilombero ni ‘package’ kwa sababu kuna vitu vingi vinapatikana katika wilaya hiyo. Anavitaja kuwa ni pamoja na uwepo wa Hifadhi ya Nyerere ambapo lango la kuingilia katika hifadhi hiyo limewekwa Msolwa.

Pia, anasema ndani ya wilaya ya Kilombero wana pori tengefu la Ilumwa ambalo hutumiwa na watafiti kufanya tafiti hasa za mimea na wanyama.

Mbali na hilo, pia, anasema wanapori la akiba la Kilombero lenye wanyama aina ya sheshe na mito yenye samaki aina zaidi ya 200.

“Watu waje kutalii ndani ya wilaya yetu, Rais Samia amehakikisha mambo yanakuwa mazuri, barabara tayari tunayo, umeme tayari, kwanini watu wasije?

“Mtu yoyote anaweza kufanya get away ya kutoka Dar es Salaam kuja Udzungwa, kwenda kuona Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Watu wanaweza kuja kwa timu, kwa familia ama kwa mmoja mmoja, kwa urahisi zaidi,” anasema DC Kyoba.

Kwa upande mwingine anasema mgeni yoyote anaweza kufika katika wilaya ya Kilombero kwa njia ya ndege huku akivitaja viwanja vya ndege vilivyoko kwenye wilaya hiyo kuwa vitatu; kimoja akisema kipo kwenye kiwanda cha sukari cha Kilombero, kingine Ifakara na kingine kipo ndani ya hifadhi ya Mwalimu Nyerere.

“Sisi Kilombero tunaongoza kwa kilimo cha miwa Tanzania na Afrika mashariki hakuna anayezalisha sukari kutuzidi, sema kwa sasa mvua zimeathiri uzalishaji, tunaongoza pia kwa kilimo cha mpunga, hii nayo ni fursa ya uwekezaji na utalii,” anasema Kyoba.

Anawakaribisha wanafunzi pia kuja kutalii na kujifunza katika hifadhi ya safu za Milima ya Udzungwa.

Kwa upande wa Mbunge wa jimbo la Kilombero, Abubakar Asenga, anasema bonde la Kilomboro ni eneo muhimu kwa sababu maji yanayoingia kwenye bwawa la maji la Mwalimu Nyerere.

“Asilimia 46 ya maji yanayoenda bwawa la Mwalimu Nyerere yanatoka kwenye hifadhi ya Milima ya Udzungwa. Juzi wamekuja wabunge wenzangu wakaridhika na hili eneo, wakashangaa kukuta hali ya hewa ya tofauti.

“Nawaambia wabunge wenzangu waje kupumzika na familia zao, tuko tayari kuwapokea,” anasema Asenga.

By Jamhuri