Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

Serikali imeshaidhininisha kiasi cha shilingi Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Kiloka linaounganisha kijiji cha Kiloka na vijiji jirani ambalo lilisombwa na maji ya mvua zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka huu nchini.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa miindombinu ya barabara na madaraja inayosimamiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Morogoro.

Picha mbalimbali zinazoonesha daraja la Kiloka lililopo wilaya ya Morogoro ambalo limeathiriwa na mvua za Elnino zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka huu nchi nzima ambapo serikali imeidhinisha kiasi cha shilingi milioni 250 ambazo zitaenda kurejesha mawasiliano kwenye vijiji jirani. Daraja hilo lenye urefu wa mita 12 litajengwa na kuwekewa kingo za mto pamoja na kukarabati tuta la barabara.

Mhandisi Mativila amesema serikali imetoa fedha hizo kuweza kurejesha mawasiliano katika vijiji hivyo ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma za kijamii pamoja na zile za kiuchumi.

“Serikali imejikita kwenye ukarabati wa miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua za Elnino,hivyo fedha hizi zitaenda kurejesha mawasiliano kwa kujenga daraja hili la Kiloka na vijiji vya jirani”.

Hata hivyo Mhandisi Mativila aliitaka TARURA kuendelea kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo ili kuwawezesha wananchi kuweza kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama ilivyokuwa awali.

Naye, Meneja wa TARURA wilaya ya Morogoro Mhandisi Mohamed Muanda amesema wanaishukuru serikali kwa kuwapati fedha hizo ambazo zitaenda kurejesha mawasilino ya vijiji vya jirani kupitia daraja la Kiloka.

Amesema fedha hizo zitaenda kujenga daraja hilo lenye urefu wa mita 12 na kuliwekea kingo za mto pamoja na ukarabati wa tuta la barabara