Na Muhidin Amri, JamhuriMedia, Songwe

ZAIDI ya watu 6,000 wa vijiji vya Ilasilo na Kongatete Halmashauri ya wilaya Songwe mkoani Songwe, wanatarajia kuondokana na changamoto ya huduma ya maji safi na salama.

Ni baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa), kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha mradi wa maji wa Galula-Kangatete wenye thamani ya Sh.milioni 344.
Hayo yalisemwa na kaimu meneja wa Ruwasa wilayani humo Ponsiano Kailole,wakati akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Ruwasa wilaya ya Songwe.

Alisema,mradi huo ni miongoni mwa miradi ilinayoendelea kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na mara utakapokamilika utaleta tija kubwa kwa wananchi na kutimiza adhima ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Alisema mradi ulisanifiwa kuhudumia vijiji vitatu, kati ya vijiji hivyo viwili vilikuwa na mradi wa maji wa zamani kwa kutumia chanzo kingine ambacho kiliharibika,na wakaamua kujenga mradi mpya kwa ajili ya kijiji kimoja ambacho hakikuwa na maji na kurudisha huduma hiyo kwenye vijiji viwili.


Kailole alisema,ujenzi wa mradi huo unaendelea na umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi ambapo alitaja kazi zilizotokelezwa ni kujenga tenki la lita 100,000,vituo vya kuchotea maji 8 kati ya hivyo 5 vinatoa huduma na kujenga mtandao wa maji urefu wa kilomita 21.

Aidha alisema,mkandarasi ameshalipwa Sh.milioni 130 na yuko katika hatua za mwisho kukamilisha kazi ambazo ni kufunga bomba ya chuma kwenye maeneo yenye makolongo makubwa.

Katika hatua nyingine Kailole alisema,wamekamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Kaloleni- Iseche uliopo kijiji cha Iseche kata ya Mwambani kwa gharama ya Sh.milioni 310.

Alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi machi na kukamilika mwezi Septemba 2023 na umehusisha ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 100,000,vituo 3 vya kuchotea maji na mtandao wa bomba kilomita 9.1.

Kwa mujibu wa Kailole,mradi wa Iseche ndiyo mradi pekee katika wilaya ya Songwe ambao wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuingiza maji majumbani na kulipia gharama za matumizi ya maji ambapo kwa muda wa wiki mbili tangu ulipoanza kutoa huduma zaidi ya watu 100 wameingiza maji majumbani.

Diwani wa kata ya Mwambani Noha Sharif alisema,kijiji cha Iseche ndiyo cha mawisho katika kata hiyo kupata mradi wa maji ya bomba na ameishukuru serikali kutoa fedha ili kutekeleza mradi huo.

Alisema,kabla ya mradi huo wananchi wa kijiji cha Iseche walikwenda hadi mto Songwe umbali wa kilomita 4 kila siku kuchota maji kwa ajili ya matumizi yao hivyo kuathiri ushiriki wa kazi za maendeleo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Iseche Gaudence Nusuhela alisema,tangu kijiji hicho kilipoanzishwa mwaka 1974 hakikuwa na huduma ya maji ya bomba,badala yake wananchi walitegemea chanzo pekee cha mto Songwe.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kangatete wilayani Songwe wakicheza ngoma ya asili na kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Songwe mkoani Songwe Mhandisi Ponsiano Kailole kulia baada ya kushuhudia maji ya bomba  kwa mara ya kwanza tangu Uhuru.

Diwani wa kata ya Mwambani Halmashauri ya wilaya Songwe mkoani Songwe Noha Sharif,akizungmza na baadahi ya wananchi wa kijiji cha Iseche kuhusiana na umuhimu wa kutunza miradi ya maji na kulinda vyanzo ili miradi inayotekelezwa iweze kudumu kwa muda mrefu.
Diwani wa kata ya Mwambani Halmashauri ya wilaya Songwe mkoani Songwe Noha Sharif,akizungmza na baadahi ya wananchi wa kijiji cha Iseche kuhusiana na umuhimu wa kutunza miradi ya maji na kulinda vyanzo ili miradi inayotekelezwa iweze kudumu kwa muda mrefu.

By Jamhuri