Ripoti ya CAG yathibitisha madai aliyotoa mwaka jana

DAR ES SALAAM

Na Alex Kazenga

Wiki iliyopita iligubikwa na taarifa za kutoweka kwa mmoja wa mawakili wa Mahakama Kuu, Peter Madeleka, ikidaiwa kuwa ‘ametekwa’ na watu wasiojulikana.

Inadaiwa kuwa Madeleka, kachero wa zamani wa Jeshi la Polisi, alichukuliwa kwa ajili ya mahojiano na maofisa wa serikali nje ya Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mchana wa Jumanne ya Aprili 19, mwaka huu.

Na sasa taarifa rasmi zinasema kwamba Madeleka anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, na kwamba jana angeachiwa kwa dhamana, taarifa zinazozima tafrani iliyoibuka kwenye mitandao ya kijamii ambako watu wamekuwa wakidai kuwa ametekwa nyara.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, kelele hizo zimesababisha dhamana ya kuachiwa huru iliyokuwa wazi baada ya mahojiano kusitishwa kwa muda.

Taarifa hiyo inasema kukamatwa kwa Madeleka kunatokana na kosa la kukaidi wito wa polisi.

“Tulimwita aje kutoa maelezo ya tuhuma alizosambaza kwenye mitandao ya kijamii, akimtuhumu mmoja wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji kwamba anataka kumuua,” inasema taarifa hiyo.

Inadaiwa kuwa siku moja kabla ya kukamatwa kwake, alipewa wito na akakumbushwa kwa kupigiwa simu, lakini hakwenda.

“Medeleka hakutekwa. Ila alichukuliwa kwenda kutoa maelezo ya mambo aliyokuwa amepanga kuyasema kwenye mitandao ya kijamii,” imesema taarifa ya polisi.

Siku chache kabla ya kukamatwa, Madeleka alikuwa ameahidi kufanya kongamano katika Hoteli ya Serena kuueleza umma kuhusu sakata la ‘viza’ feki na hasara ambayo wahusika wanalisababishia taifa.

Polisi wanasema kukamatwa kwa Madeleka kulifanyika hadharani, na kwamba wakati huo alikuwa na wenzake watatu ambao ndio waliotoa taarifa, kwa kuwa walifahamishwa kwamba anapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), Dar es Salaam, ambapo baadaye alihamishiwa ilipokuwa Wizara ya Mambo ya Ndani na makao makuu ya zamani ya polisi.

Polisi wanasema akiwa mikononi mwao walimpa haki zote, ikiwa ni pamoja na kumruhusu kuwasiliana na mwanasheria pamoja na familia yake.

Taarifa za polisi zinakinzana na zile zilizotolewa wiki iliyopita na Wakili Paul Kisabo, aliyefika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na baadaye wizarani, akisema kuwa aliambiwa hakuna taarifa za kukamatwa mteja wake.

“Awali nilielezwa kuwa yupo mikononi mwa polisi, na kwamba yupo salama. Hawakuniambia sababu za kumkamata,” anasema Kisabo.

Anasema baada ya mawasiliano ya ziada na maofisa kadhaa, aliambiwa kwamba Madeleka amekamatwa kwa makosa ya uharifu wa kimtandao ‘cybercrime’, lakini baadaye maofisa hao wakamweleza kuwa taarifa walizompa si za kweli, kwa kuwa wamechanganya majina.

Miongoni mwa makosa yanayodaiwa kufanywa na Madeleka ni kuwatuhumu maofisa wa Idara ya Uhamiaji kuwa wanapanga njama za kumuua.

Madeleka na Ripoti ya CAG

Wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akitoa ripoti mapema mwezi huu, pamoja na mambo mengine, ameorodhesha mambo kadhaa yanayohusu Idara ya Uhamiaji, ikiwamo upotevu wa mabilioni ya fedha.

Kwa mara ya kwanza madai hayo yaliandikwa na Gazeti la JAMHURI Mei mwaka jana baada ya kuzungumza na Madeleka.

Hii hapa habari iliyochapwa mwaka jana chini ya kichwa cha habari: ‘‘VISA’ FEKI… Siri imefichuka’…

Ufujaji mkubwa wa fedha umeripotiwa kufanyika ndani ya Idara ya Uhamiaji nchini, ukihusisha mtandao mpana wa kimasilahi uliojichotea fedha kwa kutoa vibali feki vya kuingia nchini na vile vya kuishi au kufanya kazi nchini, JAMHURI limedokezwa.

Uhamiaji ni miongoni mwa idara nyeti zenye dhamana ya kusimamia na kuimarisha ulinzi wa taifa, lakini sasa baadhi ya maofisa wasio waaminifu wanadaiwa kujihusisha na vitendo haramu, kinyume cha maadili ya kazi zao.

“Kazi ya idara yetu pia ni kukusanya ‘maduhuli’ ya serikali. Lakini sasa kuna mabosi wetu wameamua kuweka rehani usalama wa nchi yetu kwa makusudi kabisa,” anasema mmoja wa maofisa ‘waadilifu’ wa Uhamiaji akiomba hifadhi ya jina lake.

Anasema kuna wizi wa mabilioni ya fedha umefanyika kati ya mwaka 2015 hadi 2020 unaofanikishwa kwa kughushi vibali vya wageni kuishi (resident permits) na vya kuingia nchini (visas).

Wiki iliyopita, Wakili wa Mahakama Kuu, Peter Madeleka, aliliambia JAMHURI kuhusu kuwapo kwa mtandao huo, akidai kuwa unaongozwa na kuratibiwa na baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa Idara ya Uhamiaji.

“Mwaka 2019 nilihusishwa katika mtandao huo (wa visa feki) na kushikiliwa katika Gereza la Mahabusu la Segerea na baadaye Kisongo, Arusha kwa mwaka mmoja na miezi saba. Baadaye nikaachiwa kwa kukosekana ushahidi.

“Lakini mtandao wenyewe haukuguswa na umeendelea kuwapo. Wanalindana,” anasema Madeleka akidai kuwa ukwasi wa hali ya juu walionao baadhi ya maofisa wa Uhamiaji ni kielelezo tosha cha ubadhirifu wanaoufanya serikalini.

Kauli yake inathibitishwa na mtoa habari wetu ndani ya idara, anayedai kuwafahamu fika wote wanaohusika.

Kazi hufanywa kwa usiri wa hali ya juu

Ofisa huyo anasema fedha maalumu hutengwa kwa ajili ya kuchapisha vibali hivyo feki katika utaratibu usio rasmi.

Inakadiriwa kuwa visa feki 500 zimekuwa zikitolewa kwa wageni nchini kila mwezi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita; nyingi zikiingizwa kutoka Afrika Kusini kupitia Nairobi na Namanga.

Hata hivyo, JAMHURI linafahamu kwamba vipo vibali vingine viliingia kwa njia ya barabara katika mpaka wa Tunduma.

“Kwa kuwa kuna watu walikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Agosti 2019 wakiwa na visa feki zenye thamani ya Sh bilioni 1.4; maana yake ni kwamba hata uwanja huo nao hutumika kama njia ya kuingiza magendo hayo,” anasema Madeleka ambaye katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi naye alihusishwa.

“Vibali hivyo vikishaingia nchini husambazwa kwa maofisa wafawidhi wa vituo vinavyoingiza wageni kwa wingi kama JNIA, KIA, Namanga na Tunduma,” anasema mtoa habari wetu.

Mipaka mingine ni ya Kasumulu (Kyela), Horohoro (Tanga) na Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na kutumika kama visa halali ingawa hazimo kwenye mfumo rasmi unaotambulika na kuingiza fedha serikalini, badala yake mapato yanayotokana na visa hizo huingia kwenye mifuko ya watu binafsi.

Hata mgawo pia ni siri

“Kuna maofisa waadilifu mipakani walijikuta wakipokea fedha wala hawajui zilikotoka, kwa kuwa hawakuwamo kwenye mtandao. Lakini utakataaje fedha?

“Hata kama ni muadilifu, kwamba huwezi kukubali kutoa vibali feki lakini kumbe vimeshapita kwenye mikono yako bila kufahamu, ukipewa fedha na mtu unayemuamini, unapokea na kushukuru tu,” anasema ofisa huyo ambaye pia amewahi kukaa katika mpaka wa Namanga nyakati hizo za hujuma.

Anasema vibali feki viliingizwa katika kila shifti na kiongozi wa ‘wanamtandao’ kwenye shifti husika alitakiwa kupeleka ripoti ya mapato hayo ‘haramu’ kwa viongozi wao.

“Mgawo ulikuwa ukifanyika kila mwisho wa wiki, ukitofautiana kwa vyeo, nyadhifa na kuaminika kwa wahusika. Usiri huo ndio ulifanya maofisa wengine kupata fedha bila kuelewa wapi zimetoka,” anasema.

Anasema yeyote aliyehisiwa kuvujisha siri ya mtandao huo au hata kuonyesha dalili za kupambana nao au kuupinga, ama alifukuzwa kazi au kupelekwe kwenye vituo ‘dume’ visivyo na fedha.

“Kuna wengine wamebambikiwa kesi za uhujumu uchumi kwa kuwa kinyume cha mtandao,” anasema na kuwataja watu hao (majina tunayo) na kituo chao cha kazi.

Kwa upande wa vibali vya ukaazi, tofauti na visa, hivi vilisambazwa kwenye mikoa kama Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza, Arusha, Pwani, Mtwara na Mbeya, inayoaminika kuwa na wageni wengi wanaofanya kazi.

Katika mikoa hiyo kulikuwapo mwanamtandao walau mmoja mwenye jukumu la kupokea maombi ya hati za ukaazi na kuziingiza katika mfumo wa kughushi.

“Walikuwa wamejipanga vizuri sana. Walikuwa na kompyuta mpakato zenye ‘soft copy’ kwa ajili ya kuingizia taarifa za wateja. Karatasi zao ni kama zile za serikali kabisa! Huwezi kutofautisha kama si mtaalamu,” anasema.

Kila kazi iliyofanyika ililindwa ipasavyo na kwa muda wote hakuna taasisi ya dola kama Polisi au TAKUKURU walioshituka.

Wazungu wa unga nao wanufaika

Chanzo kingine cha mapato haramu kwa wanamtandao ndani ya Idara ya Uhamiaji kilikuwa ni utoaji wa vibali vya ukaazi kwa raia wa kigeni, hasa wa mataifa ya Afrika Magharibi.

“Hawa hawakuwa wakiishi wala kufanya kazi Tanzania. Walikuwa wakitoa fedha nyingi ili watengenezewe vibali vya ukaazi vya Tanzania, kisha wanakwenda kuomba visa za Asia na Amerika Kusini ambako ndiko maeneo yao ya biashara ya dawa za kulevya.

“Hali hii ilisababisha Tanzania kuchafuka kimataifa kwa kuonekana kinara wa biashara za dawa za kulevya,” anasema.

Katika kuulinda mtandao huo, wakuu wa Idara ya Uhamiaji wanadaiwa kuwaonea wafanyakazi wa ngazi za chini walioonekana kwenda kinyume nao.

“Zaidi ya wafanyakazi 120 wamesimamishwa au kufukuzwa kazi kwa uonevu tu. Wengi miongoni mwao ni wale waliokuwa hawakubaliani na yanayoendelea ndani ya idara au wale wasiokuwa na wakubwa wa kuwabeba,” anasema.

Inadaiwa kuwa wafanyakazi waliofukuzwa hawapewi nafasi ya kujitetea, na wapo ambao hadi sasa hawajalipwa mafao yao.

“Yaani kuna madudu mengi sana ndani ya idara, huwezi kuamini, watu wanafukuzwa na kutelekezwa vituoni bila kupewa stahiki zao,” anasema ofisa Uhamiaji huyo.

Anawataja maofisa wawili wa juu kama vinara wa mtandao wa wizi na uonevu akisema: “Afadhali Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) ameligundua hilo na kufanya mabadiliko ndani ya idara.

“Huenda mambo yatakuwa mazuri sasa na uonevu utakwisha. Kwa nini unamhamisha mtu kituo cha kazi bila kumlipa chochote? Watu wanahamishwa hadi mara tatu bila malipo! Hii si sahihi.”

 Ofisa huyo anamuomba Rais aunde tume maalumu ya kupitia upya taarifa za maofisa na askari wa Uhamiaji waliofukuzwa kazi ili haki ibainike na kutendeka.

Uhamiaji wazungumza

JAMHURI limemtafuta mmoja wa makamishna wa Uhamiaji anayetajwa kuwamo kwenye mtandao huo huku pia akidaiwa kufanya vitendo vya uonevu kwa maofisa wa chini; na sasa ameondolewa kwenye nafasi aliyokuwa nayo ili kujua uhalisia wa tuhuma dhidi yake.

“Sidhani kama ni kweli, kwa kuwa kwa nafasi niliyokuwa nayo sihusiki kabisa na vibali kama hivyo. Wapo makamishna wanaohusika, labda wao ndio uwaulize,” anasema ofisa huyo akikana lawama na shutuma zote zilizoelekezwa dhidi yake.

Anasema ni kweli ameondolewa kwenye nafasi aliyokuwa nayo awali, lakini ni utaratibu wa kawaida wa kikazi na kwamba: “Kwa sasa ninasubiri kupangiwa kazi nyingine.”

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, ameliomba JAMHURI kufika ofisini kwake jijini Dodoma kujadiliana kwa kina kuhusu masuala yote yanayolalamikiwa.

690 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons