Leo nimeamua kusitisha makala ya Raila Odinga na urais wa Kenya ili nami kidogo nishiriki kujadili na kuichambua miaka mitatu ya Rais John Magufuli.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli iingie madarakani, yametokea mambo mazuri kadhaa. Binafsi nitajikita katika machache, ambayo yote yanaangukia katika ujenzi wa miundombinu.

Naanza na umeme. Umeme ndio msingi wa maendeleo kwa taifa lolote. Wakati sisi hapa tukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 1,500 kwa sasa, naomba kusimulia safari yetu ya maendeleo inavyohitaji umeme. Takwimu za kidunia zinaonyesha kuwa dunia inatumia umeme wastani wa megawati bilioni 25. China peke yake inatumia bilioni 5.6.

China inafuatiwa na Marekani inayotumia umeme megawati bilioni 4.6, ambayo nayo inafuatiwa na Jumuiya ya Ulaya inayotumia megawati bilioni 3.2, huku Urusi ikishika nafasi ya nne kwa kutumia megawati bilioni 1.0, ikifuatiwa kwa karibu na India inayotumia megawati bilioni 0.98. Kwetu hapa Afrika nchi inayoongoza ni Afrika Kusini inayotumia megawati 234,000.

Sitanii, nimejaribu kuangalia nchi zote zilizoendelea, nchi yenye maendeleo ya kati inayotumia megawati kidogo sana ni megawati 15,000. Hapa Tanzania tunapozungumza megawati 1,500 ni uwezo wa kuzalisha, lakini uzalishaji halisi unaweza kukuta unaishia megawati 1,000 tu. Ni kwa mantiki hiyo, ikiwa nchi yetu inataka maendeleo ya kweli, ni lazima imuunge mkono Rais Magufuli katika mpango wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge.

Umeme wa Stiegler’s Gorge ujenzi wake ukikamilika tutapata megawati 2,100. Kiasi hiki kinatuelekeza huko katika maendeleo. Naomba kutoa mfano hai. Mwekezaji wa mradi wa kuchimba madini ya nikel, pale Kabanga – Ngara, Kagera, mwaka 2006 alikuwa anataka umeme wa megawati 800 ili aweze kuanzisha uchimbaji katika mgodi huo.

Sitanii, viwanda vinavyozalisha faida vinatumia umeme mkubwa. Kwa mfano kiwanda cha kuchakata aluminum cha Australia (Australia Aluminum Smelter) kinatumia wastani wa megawati 800. Kiwanda cha kutengeneza magari kinatumia angalau megawati 95. Kiwanda cha ndege kama Bombardier kinatumia umeme wa megawati karibu 150.

Kwa msingi huo, katika eneo hili la umeme wa Stiegler’s Gorge tukiunganisha na huo wa gesi, basi tufahamu kuwa huo ndio mkondo sahihi wa kuelekea kwenye maendeleo.

Eneo jingine ni ununuzi wa ndege. Kwa sasa utalii unachangia asilimia 17.5 ya uchumi wa taifa letu. Hii ina maana nchi yetu ikiwa na usafiri wa ndege wa uhakika, tutaweza kusafirisha watalii kutoka kona nyingi za dunia. Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, mwaka 2017 nchi yetu ilipata watalii milioni 1.3. Tukipata watalii milioni 10 kwa vivutio tulivyonavyo, umaskini tunauaga. Ndege ndizo za kutufikisha huko.

Suala la reli nalo ni ukombozi wa uchumi. Tanzania haiwezi kuendelea kwa utaratibu wa kusafirisha mzigo mkubwa kwa malori. Reli inapunguza gharama za usafirishaji. Nchi yetu ikifika mahala ikapata uwezekano wa kusafirisha angalau tani 5,000 kwa wakati mmoja kwa kutumia reli badala ya malori, unakuwa umeondoa malori 156 kwa wakati mmoja. Kwa mantiki hiyo, ujenzi wa reli ni suala la msingi mno katika kukuza uchumi.

Hata hivyo, wakati hayo yote mazuri yakiendelea, Rais Magufuli naomba kukushauri kiungwana ujaribu kuiangalia historia. Historia ni mwalimu mzuri mno. Ukiona kesi za uchochezi zimeongezeka, si vema kulichukulia jambo hili kuwa ni la kawaida. Inapotokea kundi fulani likadai haki, baadhi ya watu huliita kundi hilo la kichochezi. Idadi ya kesi walizonazo wapinzani nchini mwetu zinaanza kuwakumbusha watu harakati za uhuru ambapo kina Mwalimu Julius Nyerere walifunguliwa kesi za uchochezi.

Kwa kasi ya maendeleo inayofanya serikali yako, iwapo usingeruhusu doa la kupeleka kila mpinzani mahakamani na raia wanaowaza tofauti na falsafa yako, ungejenga maendeleo kwa kasi kubwa ajabu. Kimsingi yote waliyokuwa wanalalamikia wapinzani ndiyo unayotenda, sasa najiuliza, kwa nini usuguane nao? Tafadhali jenga miundombinu, lakini ruhusu uhuru wa mawazo. Mawili haya yanakwenda sambamba.

1871 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons