MizengoWaziri Mkuu  mstaafu, Mizengo Pinda anaumwa.

JAMHURI limeambiwa kuwa Pinda ni mgonjwa kwa kipindi cha wiki mbili sasa, hali iliyomfanya asionekane hadharani.

Si upande wa Serikali, wala familia yake waliokuwa tayari kueleza maradhi yanayomsumbua mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, watu walio karibu naye wamethibitisha kuwa siha yake si nzuri. Taarifa zilizopatikana mwishoni mwa wiki zilisema mipango ilikuwa ikifanywa ili akapatiwe matibabu nje ya nchi.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane, Pinda, ameshindwa kuhudhuria sherehe na matukio makubwa ya kitaifa.

Alishindwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Waziri Mkuu wa Awamu ya Tano, Majaliwa Kassim, zilizofanyika Novemba 20, katika Ikulu Ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma.

Pinda alishindwa pia kuhudhuria sherehe za uzinduzi rasmi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliofanywa na Rais John Magufuli.

“Mheshimiwa Pinda ni mgonjwa kwa muda sasa, taarifa zake za kuugua zilitolewa mapema wiki ya pili ya mwezi huu, kisha aliondoka kwenda kijijini kwake Kibaoni (Katavi).

“Kwa sasa yupo shambani kwake Zuzu, Dodoma ambako anaendelea kujiuguza,” kimesema chanzo chetu.

Viongozi kadhaa wamekuwa wakienda nyumbani kwake kumjulia hali. Miongoni mwao ni Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alimjulia hali Novemba 21.

“Amedhoofu, lakini si kuwa yuko taabani, anaongea vizuri,” kimesema chanzo chetu.

Gazeti la JAMHURI limezungumza na Msemaji wa Serikali, Assah Mwambene, kuhusu afya ya Pinda, na akasema hakuwa na taarifa za kina kuhusu afya ya Waziri Mkuu mstaafu.

Kwa muda wote aliokuwa Waziri Mkuu, Pinda, hakuwa na historia ya kuugua, na hata kutibiwa nje ya nchi.

Kutoonekana kwake kwenye shughuli hizo za kitaifa kumeibua sintofahamu miongoni mwa wanasiasa na wananchi kadhaa.

Kwenye hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge, Rais Magufuli, aligusia suala la afya za Watanzania na kusema: “Tutaimarisha na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza utaalamu katika nyanja za afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi; kwa kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu.

“Lengo la kufanya hivyo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma mahsusi hapa hapa nchini na hivyo kutolazimika kupeleka watu wetu kutibiwa nchi za nje.”

Pinda alikuwa miongoni kwa wana CCM waliojitokeza kuwania kuteuliwa na chama hicho ili waweze kukiwakilisha kwenye uchaguzi wa rais.

Hata hivyo, jina lake lilikuwa miongoni mwa majina yaliyokatwa katika hatua za awali kabisa, likiwa pamoja na la Makamu wa Rais Mohamed Gharib Bilal.

Watu walio karibu na Pinda, wanasema tangu wakati hu, Pinda, kama ilivyo kwa Bilal, amekuwa mtu asiye na furaha.

Wanasema uchungu anaupata pale anapojiuliza sababu za msingi za yeye kama Kiongozi Mkuu wa shughuli za Serikali za kila siku, kushindwa kuingia kwenye “tano bora”, lakini wanasiasa wachanga kama January Makamba, wakifanikiwa kupenya.

“Tukio hilo lilimpa mzee msongo wa mawazo kwa sababu hakuamini kilichotokea. Tangu wakati huo amekuwa mwenye mawazo,” kimesema chanzo chetu.

Pamoja na Pinda, mwanasiasa mwingine mkongwe, Spika mstaafu Samuel Sitta, naye hakuweza kujitokeza kwenye uapishwaji Waziri Mkuu Majaliwa na pia wakati wa hotuba ya uzinduzi ya Rais Magufuli, bungeni.

Inadaiwa kwamba kutoonekana kwake kumetokana na hasira za kukatwa jina lake kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta uwakilishi wa kiti cha uspika.

Sitta, alikuwa miongoni mwa majina ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyokatwa kwenye ngazi ya Kamati Kuu ya chama hicho.

Sitta, ambaye hadi mwezi huu alikuwa Waziri wa Uchukuzi, amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu ndani ya CCM.

Alikuwa Spika wa Bunge la Tisa mwaka 2005-2010. Alipotaka kuwania nafasi hiyo mwaka 2010, alienguliwa kwa kigezo cha “zamu ya wanawake” kilichowekwa na CCM. Sharti hilo lilikuwa gumu kwake kulitekeleza, na kwa hiyo akajikuta hana namna, isipokuwa kuukosa uspika. Anne Makinda, ndiye alishinda nafasi hiyo.

Maspika wastaafu, Makinda, na Pius Msekwa, walidhuria sherehe hizo.

Kwa upande wa mawaziri wakuu wastaafu, Jaji Joseph Warioba, na Samuel Malecela walihudhuria Chamwino na baadaye bungeni. Salim Ahmed Salim na Cleopa Msuya, hawakuwapo.

Wengine wawili, Edward Lowassa, na Frederick Sumaye, kama ilivyotarajiwa, hawakuhudhuria. Lowassa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ilhali Sumaye akiwa amejivua uanachama wa CCM bila kutangaza rasmi chama kingine cha siasa alichojiunga nacho. Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wanasiasa hao wawili walishiriki kampeni hizo na kutoa upinzani mkali kwa CCM.

4821 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!