kanuniUjasiri wa Rais John Magufuli, wa kueleza madhara ya safari za nje kwa uchumi wa nchi, umemwongezea umaarufu miongoni mwa wananchi.

Miongoni mwa wasafiri wakuu nje ya nchi alikuwa mtangulizi wake, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, anayetajwa kuwa ndiye kiongozi wa nchi katika Afrika aliyesafiri nje ya nchi kuliko marais wengine.

Wakati fulani aliweza kuishi Marekani kwa wiki tatu, akiwa kwenye matamasha na shughuli nyingine za kawaida, huku akitajwa kuwa na msafara wenye watu wengi mno.

Akifungua rasmi Bunge wiki iliyopita, Rais Magufuli, alizungumzia safari za watumishi wa umma nje ya nchi na kusema wapo waliosafiri kwenda nje ya nchi mara nyingi zaidi kuliko walivyoenda vijijini kuwajulia hali mama zao.

Rais Mstaafu akiwa ameshika tama, Rais Magufuli alitaja eneo la safari kuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo Serikali yake itayasimamia kwa lengo la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali.

Wananchi wengi wamepongeza ujasiri huo wa Rais Magufuli, na wamekuwa na imani kuwa kama amethubutu kulisema jambo hilo zito linalomgusa moja kwa moja mtangulizi wake, tena akiwa mbele yake, hiyo ni dalili kuwa kuna mabadiliko makubwa yanakuja.

“Tutazidhibiti safari za nje na badala yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye mikutano ya aina hiyo. Na pale inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi kusafiri tutahakikisa kwamba haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana umuhimu wala shughuli za kufanya katika safari hizo,” alisema.

Rais Magufuli aliongeza: Katika kusisitiza hili napenda niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015.

“Jumla ya shilingi bilioni 356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:

•Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi bilioni 183.160;

•Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia shilingi bilioni 68.612;

•Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia shilingi bilioni 104.552;

Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani, n.k.

“Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami, tujiulize zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? Nyumba za walimu ngapi? Madawati mangapi? n.k. Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.”

 Wananchi waliohojiwa na JAMHURI mara baada ya hotuba, wamependekeza Rais Magufuli, aongezewe ulinzi kwa kuwa genge la walioanza kumchukia, ingawa ni dogo, linajipanga kuhakikisha hafanikiwi.

“Mheshimiwa (Rais Magufuli) amenifanya nione kama Nyerere yuko hai. Hotuba ya aina hii tulikosa kuisikia kwa mika mingi. Tunashukuru Rais ameanza kutuonyesha nuru ya Tanzania mpya,” amesema John Mang’ondi, mkazi wa Dodoma.

Hotuba yote ya Rais Magufuli, ya uzinduzi wa Bunge tumeichapisha katika Uk.14 wa toleo hili.

 

Kikwete ‘muumini’ wa safari za nje

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Rais Kikwete, alilaani na kushangazwa na watu wanaomshangaa kwa kusafiri mara kwa mara kwenda nje ya nchi na kusema safari hizo zina maana kubwa.

Akasema kama safari hizo zisingekuwapo, Watanzania walio wengi wangekufa kwa njaa.

Katika mkutano wake wilayani Urambo, alisema safari hizo zina maana kubwa si kwake tu, bali ni kwa Watanzania walio wengi.

Alisema kuwa safari hizo zinamwezesha kwenda kuomba misaada kwa wahisani na kunufaisha nchi kama nchi; na si yeye kama watu wanavyombeza na kumshangaa.

Alijitetea kwa kusema kuwa: “Mimi ninapokwenda nje nakwenda kwa malengo, sijiendei tu -naomba mtambue, lazima niende huko nikutane na watu mbalimbali watakaoweza kusaidia nchi yetu.”

Akaongeza kijembe kwa kusema: “Siwezi kukaa Ikulu tu kuangalia uzuri wa mke wangu Salma.”

Akahoji kwa kusema: “Hivi kama nisingeenda Marekani kuongea na rafiki yangu Bush (Rais George Bush) tungewezaje kusaidia kudhibiti malaria? Nilipokwenda kule nikakutana na rafiki yangu akaniambia nitamaliza tatizo la malaria kwako na kweli akatununulia vyandarua vyenye thamani ya dola milioni 78.” alisema.

Akawataka Watanzania wanaolalamikia safari zake watambue kuwa yeye anakwenda kuitengeneza nchi na kukutana na wahisani na mara nyingi safari zinakuwa za kiserikali.

 

Kauli ya Rais Magufuli yaiumbua Wizara

 Septemba 17, mwaka huu, Serikali, kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilitoa taarifa ikikanusha madai yaliyotolewa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ya kwamba Rais Kikwete alikuwa ametumia Sh trilioni 4 kwa kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake kwa safari za nje.

“Tangu Rais Jakaya Mrisho Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, kiasi kikubwa kabisa cha bajeti kuwahi kutengwa kwa ajili ya safari za Viongozi Wakuu yaani Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ni shilingi bilioni 50 ambazo zilitengwa kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015 kwa ajili ya Idara ya Itifaki.

“Kwa miaka mingine yote wastani umekuwa ni kati ya shilingi bilioni tano hadi 25 kulingana na mahitaji ya idara hiyo.

“Ifahamike kuwa kiasi hicho cha shilingi bilioni 50 ni bajeti nzima ya Idara ya Itifaki, ambapo kuna fungu maalum kwa ajili ya ziara za viongozi. Fungu hilo linagharamia makundi makuu matano kama ifuatavyo:

“1. Kundi la Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;

“2. Kundi la Makamu wa Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;

“3. Kundi la Waziri Mkuu wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;

4. Kundi la Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nje ya nchi wanapotembelea Tanzania; na

“5. Kundi la Wajumbe Maalum wanaokuja nchini kuleta taarifa muhimu kwa Rais.

 “Makundi yote haya hugaramiwa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ndani ya bajeti ya Idara ya Itifaki kifungu cha Ziara za Viongozi.

“Aidha, uandaaji wa bajeti ya Wizara chini ya Idara ya Sera na Mipango unahusisha wadau wengine nje ya Wizara kama vile Kamati ya Bunge ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hupitishwa kila mwaka na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tunapenda kuwaatahadharisha wananchi juu ya watu wanaotoa taarifa za uongo kwa madhumuni ya kujenga chuki dhidi ya Serikali. Ikumbukwe kuwa ziara za viongozi zinazoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje zina mafanikio makubwa kwa nchi na Watanzania kwa ujumla.

“Wizara inaandaa taarifa ya ndefu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara, changamoto na mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambayo itatolewa kwa umma kwa lengo la kutoa elimu zaidi,” ilisema taarifa hiyo.

 

Ukweli wa mambo

Hata hivyo, uhalisia wa mambo umeelezwa kuwa tofauti kabisa na hadaa hizo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Watu walio karibu wanasema fedha ambazo zimekuwa zikitumiwa na Rais Mstaafu Kikwete wakati wa uongozi wake ni nyingi mno, kiasi kwamba baadhi ya walionufaika nazo walikuwa hawajui wala hawahoji mishahara yao.

Imekuwa ikikisiwa kuwa safari moja ya kawaida ya kiongozi huyo iligharimu hadi Sh bilioni 2. Kundi kubwa la wasaidizi wake lilisafiri kwa kutumia daraja la kwanza na kulala katika hoteli zenye hadhi ya nyota tano au nne.

Muda mfupi baada ya kung’atuka, kumeripotiwa kuwapo hali mbaya ya fedha katika Hazina; huku deni la Taifa likifikia Sh zaidi ya trilioni 40. Deni hilo limeongezeka kwa zaidi ya asilimia 200 likilinganishwa na alilolikuta mwaka 2005.

Habari za uhakika kutoka ndani ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) zinasema mipango imeanza ya kuhakikisha wanakusanya taarifa za fedha zilizotumiwa na Rais Mstaafu Kikwete, na hata zilizohifadhiwa nje ya nchi.

Ukawa wamepanga kuanza mpango huo wakati wa Mkutano wa Pili wa Bunge utakaoanza Januari 26, mwaka huu mjinni Dodoma.

“Kwanza tunataka atangaze mali alizonazo kwa sasa. Kama aliweza kufanya hivyo alipoingia madarakani, ana wajibu wa kuwambia Watanzania kiasi alichochuma na namna alivyokipata,” amesema mmoja wa wabunge wa Ukawa.

By Jamhuri