Jaji aamua kuipitia hukumu ya ‘kiaina’ Moshi

Kashfa inayomkabili Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Kilimanjaro, Joachim Tinganga, ya kutoa hukumu yenye utata kisheria kwa mshitakiwa aliyepatikaa na hatia ya kukutwa na mali ya wizi, imefikishwa hatua za juu za uongozi wa Mahakama.

Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imeitisha jalada la kesi hiyo ya jinai ambayo hakimu huyo alimtoza mshitakiwa faini badala ya kumhukumu  kifungo kisichopungua miaka mitatu jela kama sheria inavyoelekeza.

Sakata hilo ambalo limeibua gumzo katika tasnia ya sheria, lilitokea wiki mbili zilizopita mjini Moshi baada ya Hakimu Tiganga akishirikiana na Wakili wa Serikali Kassim Nassir, kufanya “mipango” ya pamoja ya kumtoza mshitakiwa huyo faini badala ya kifungo jela.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kabla ya kuitishwa kwa jalada hilo Alhamisi iliyopita, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Benard Mpepo, alimwita Hakimu Tiganga na kumhoji kuhusu uamuzi wake huo. Baadaye aliitisha rasmi jalada hilo ili liweze kupitiwa na Mahakama Kuu.

Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake, Mpepo alisema kwa kutumia kifungu namba 30(1) (a) cha Sheria ya Mahakimu kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, Mahakama Kuu imeitisha jalada hilo ili kulipitia na kujiridhisha uhalali wa hukumu hiyo.

“Sheria hiyo inatupa mamlaka kuitisha jalada lolote la kesi iliyo Mahakama za chini yake ili kulipitia kujiridhisha na mwenendo wake, uhalali wa kisheria na usahihi; kwa hiyo jalada hili nitampelekea Jaji ili alipitie na baada ya hapo atatoa mwongozo,” alisema Mpepo.

Chini ya Sheria hiyo, Jaji Mfawidhi anayo mamlaka ya kisheria ya kuagiza kufanyiwa marejeo kwa hukumu yoyote iliyotolewa Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi au Mahakama ya Mwanzo ambayo kesi hiyo ilisikilizwa au inaendelea kusikilizwa.

 

 SAKATA LILIVYOKUWA

Mahakama ya Mosho, kupitia kwa Hakimu Tiganga inadaiwa kupindisha sheria na kumtoza mshitakiwa wa kukutwa na mali ya wizi faini ya Sh 800,000 badala ya kifungo kisichozidi miaka mitatu kama sheria inavyoelekeza.

 Mshitakiwa huyo, Devis Kavishe, alikamatwa na gari lililoibwa nchini Kenya mwaka 2012 aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Shirika la Misaada la Kimataifa la Japan (JICA) lenye namba KS653D.

 Gari hilo lilikamatwa nyumbani kwa mshitakiwa huyo eneo la Majengo mjini Moshi huku likiwa na namba za usajili T816AWN za gari lililokuwa la kampuni ya Northern Engineering ya jijini Arusha.

 Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Oktoba 20, mwaka huu, bila mshitakiwa kuwapo kortini baada ya kuruka dhamana, lakini akajisalimisha Novemba 3 na ikafanyika “mipango” ili akiri kosa na kupigwa faini.

Hata hivyo, kosa hilo linaloangukia chini ya kifungu 312 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, halina adhabu ya faini; isipokuwa kifungo jela.

 Katika hukumu yake aliyoitoa Novemba 3, mwaka huu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa Kilimanjaro, Joachim Tiganga, alimhukumu kulipa faidi ya Sh 800,000 badala ya kifungo gerezani.

Kifungu hicho kinasomeka: “If found guilty of the offence; with which he is charged and be liable, on conviction, to imprisonment for a term not exceeding three years”.

Kwa tafsiri isiyo rasmi kifungu hicho kinaamanisha: “Kama atapatikana na hatia katika kosa analoshitakiwa nalo, atatumikia kifungo kisichozidi miaka mitatu gerezani”.

 Tiganga alipoulizwa na JAMHURI sababu za kutoa adhabu ya faini badala ya kifungo, alimtaka mwandishi asitazame sheria inasemaje, bali yeye afuate tu hukumu aliyoitoa ya faini ya Sh 800,000.

 Wakili wa Serikali Kanda ya Moshi, Kasim Nasir, alipoulizwa ilikuwaje mshitakiwa hakukamatwa kama amri ya Oktoba 20 iliyotolewa na Mahakama, alijitetea kuwa walimuonea huruma.

 

“Unajua tulimuonea tu huruma tuliona atakaa muda mrefu gerezani kwa sababu angefutiwa dhamana kwa hiyo nikamsaidia kumpeleka kwa Hakimu ili apigwe faini mambo yaishe,” alisema wakili huyo.

 Alipoulizwa imekuwaje mshitakiwa akatozwa faini badala ya kifungo, wakili huyo alimrejesha mwandishi kwenye kifungu cha 29 cha kanuni ya adhabu kuwa kinampa hakimu uwezo huo.

 Kifungu hicho kinahusika tu pale ambako shitaka analoshitakiwa nalo mshitakiwa lina mwanya wa faini, lakini kiwango cha faini hakikuelezwa na Mahakama lakini si kwa kosa lenye adhabu ya kifungo.

 Baadhi ya wanasheria waliozungumza na JAMHURI wameshtushwa na hukumu hiyo wakisema kisheria kosa la kupatikana na mali ya wizi ama inayodhaniwa haikupatikana kihalali huwa halina faini.

Wanasheria hao wameiomba mamlaka ya juu kuitisha jalada hilo na kupitia upya mwenendo wa kesi hiyo hadi kutolewa kwa hukumu hiyo kwa kile walichosema kinatia doa Mahakama.

Awali, mshitakiwa huyo aliruka dhamana ambako wakili Nassir aliiomba Mahakama kutoa hati ya kumkamata (arrest warrant), na kesi hiyo isikilizwe bila ya kuwapo, ombi ambalo lilikubaliwa.

Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashitaka waliotoa ushahidi wao ni ofisa kutoka kampuni ya JICA nchini Kenya, Ahmed Hassan Sirat ambaye ndiye gari hilo liliibwa nyumbani kwake.

Mashahidi wengine ni aliyekuwa Mwanasheria wa kampuni ya Northern Engineering, Regold Nkya na Meneja Masoko wa Kampuni ya uwakala wa Bima ya Ndandu ya jijini Arusha, Frank Mtui.

Mwingine aliyetoa ushahidi wake ni mfanyabiashara wa vyuma chakavu, Thobias Senya ambaye anadaiwa alilinua gari la Northern Engineering lililopata ajali baada ya kuuzwa na Bima.

Akitoa ushahidi wake, Mtui alidai kuwa gari ambalo namba zake zimebandikwa katika gari hilo la Kenya, ililipwa stahiki zote na kampuni ya bima ya MGEN baada ya kupata ajali mwaka 2011

Alidai kuwa gari hilo liliharibika vibaya lilipopata ajali Loliondo na tathimini ya wataalamu wa magari ilionesha gharama za kulitengeneza zingezidi gharama za kununua gari jipya.

Alidai makahamani hapo kuwa baada ya taratibu zote kukamilika, kampuni ya Northern Engineering ililipwa zaidi ya Sh milioni 20 na kudai yeye aliuziwa gari hilo kama chuma chakavu kwa Sh milioni 5.

Shahidi huyo alieleza Mahakama kuwa baada ya kulinunua gari hilo naye aliliuza kwa mfanyabiashara wa vyuma chakavu ambaye alikuwa shahidi wa nne katika kesi hiyo.

Kwa upande wake, mfanyabiashara huyo alilikana gari lililoletwa mbele ya Mahakama na kudai kuwa si lile alilouziwa kama chuma chakavu.

Aliiambia Mahakama kuwa gari lililopata ajali lilikuwa la rangi ya kijani huku shahidi wa nne, Thobias Senya ambaye ni mfanyabaishara wa vyuma chakavu akidai kuwa gari aliloliona mahakamani hapo si lile alilouziwa kama chuma chakavu.