Mpita Njia, maarufu kwa ufupisho wa MN, kwa wiki nzima iliyopita amesikia mijadala mingi katika mitaa kadhaa aliyopita wakati wa shughuli zake za kawaida za kila siku.

Mijadala hii ilihusu Azimio la Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Bunge limeazimia kutokufanya kazi na msomi huyo mwenye dhamana ya kikatiba ya kukagua hesabu za serikali na taasisi zake kwa niaba ya wananchi. Katika sakata hilo itakumbukwa kuwa siku chache baada ya kutoa azimio hilo, kuliibuka utata mwingine uliohitaji ufafanuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwamba kilichoazimiwa hasa na Bunge ni kutokufanya kazi na Profesa Assad tu, lakini Bunge litaendelea kufanya kazi na Ofisi ya CAG.

Katika mitaa na vijiwe alivyopita MN, mijadala ya suala hili kwa ujumla wake ilikuwa mizito na mikubwa. Katika kijiwe kimojawapo mjini Tunduru, MN alimsikia mchangiaji mmoja wa mjadala huo akihoji: “Unawezaje kudai kwamba nyama hii ni haramu kwako, lakini ukiwa uko tayari kutumia mchuzi wake?”

Mwingine tena katika hali ya hamaki akamjibu mwenzake huyo: “Usilete mambo ya nyama na mchuzi katika masuala muhimu ya kitaifa kama haya.” Akaendelea: “Huoni kwamba hapa kuna mgogoro wa kikatiba ambao kwa mapana yake hauna uhusiano na utekelezaji wa ilani ya chama tawala, CCM?” Akawahoji zaidi wenzake: “Kwani katika hili sakata masilahi ya wananchi yako kwa kiwango gani?”

Hapo mjadala ukanoga zaidi na MN akabaki kimya kusikiliza. Naam! Bwana mmoja akadakia mjadala ili kuuendeleza kutoka pale alipoishia mwenzake.

Akasema: “Nadhani katika sakata hili hakuna masilahi ya wananchi.” Mwingine akataka ufafanuzi, na haraka sana akajibiwa: “Unachotakiwa kukielewa ni kwamba masilahi ya wananchi yanapatikana kwenye ripoti za CAG, angalau kwa kujulishwa matumizi ya fedha zao yako salama kwa kiasi gani, kwa hiyo yeyote atakayekuwa anafanikisha mchakato huo wa wananchi kujulishwa mambo yao hayo kimsingi huyo ndiye anayelinda masilahi yao, pia na utekelezaji mzuri wa ilani ya uchaguzi ya chama tawala.”

Hapo, MN alikubaliana na baadhi ya hoja za ‘wananzengo’ hao kutoka kusini mwa taifa hili, kwamba malumbano baina ya taasisi moja na kiongozi fulani wa taasisi nyingine si kipaumbele cha wananchi katika vita dhidi ya umaskini. Vilevile masuala ya kuwekeana maazimio ya kususa si jambo lenye ustawi mzuri katika taifa.

Kwamba Watanzania hawana muda wa kutumbukizwa katika mijadala ya uhalali wa kauli za viongozi, bali wanachohitaji zaidi ni kushirikishwa katika utatuzi wa matatizo yao ili hatimaye taifa lisonge mbele kwa kasi inayohitajika katika maendeleo.

Please follow and like us:
Pin Share