Na Julius Konala,JamhuriMedia,Songea

Katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha majengo ya shule hapa Nchini,mkurugenzi wa kampuni ya ukandarasi ya GAJOVU Joseph Ngonyani(WAYA)amechangia mifuko 20 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya shilingi 300,000 kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule ya msingi Makambi iliyopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kwa lengo la kuthibiti wizi.

Ngonyani alitoa msaada huo jana baada ya kusomewa taarifa fupi ya mafanikio na changamoto zinazoikabili shule hiyo na mmoja wa wahitimu wa darasa la saba Julieth Kinunda katika mahafali ya shule ya msingi Makambi ya mjini humo.

Amesema kuwa katika kuguswa na changamoto hiyo pia atatoa gari ya kampuni yake bure kwa ajili ya kubebea matilio ya ujenzi wa uzio huo pindi shughuli hiyo itakapoanza.

Mkurugenzi wa kampuni inayojishughulisha na ukandarasi ya GAJOVU ya mjini Songea mkoani Ruvuma Joseph Ngonyani(WAYA)katikati akimkabidhi cheti cha kuhitimu Elimu ya msingi John Mwamkinga wa shule ya msingi Makambi kwenye mahafali ya darasa la saba ya shule hiyo mjini humo

Akizungumza katika mahafali hayo Ngonyani amewataka wahitimu hao wa darasa la saba kutobweteka na elimu waliyoipata na badala yake wajiendeleze hadi kufikia ngazi ya chuo kikuu.

Aidha amewataka wazazi na walezi wa wahitimu hao ambao wanatarajia kufanya mitihani yao ya kumalizia elimu ya msingi Oktoba 5 hadi 6 mwaka huu kuwalea vijana wao katika maadili mema ili waweze kujiepusha na utumiaji wa madawa ya kulevya,udungaji sindano na utumiaji wa mihadarati pindi wanaposubiria matokeo yao ya mtihani.

Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo Faustine Mbena akiongea katika mahafali hayo amempongeza mgeni rasmi huyo kwa mchango wake huo na kwamba amewataka wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kuchangia shughuli za maendeleo ya shule badala ya kusubiria viongozi na wageni rasmi wanaoalikwa kwenye mahafali.

Mkurugenzi wa kampuni ya ukandarasi ya GAJOVU ya mjini Songea mkoani Ruvuma Joseph Ngonyani (WAYA) katikati mwenye miwani akimkabidhi cheti cha kuhitimu Elimu ya msingi mwanafunzi Sharifa Komba wa shule ya msingi Makambi iliyopo mjini humo kwenye mahafali ya darasa la saba ya shule hiyo.

Awali akisoma taarifa ya shule kwa niaba ya wahitimu wenzake Julieth Kinunda alisema kuwa shule yao inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa madawati,uchakavu wa miundombinu ya nyaya za umeme,uchakavu wa choo cha walimu pamoja na ukosefu wa uzio wa shule ambao utasaidia kuthibiti wizi na uhalibifu wa miundombinu ya shule.

By Jamhuri