Mkanganyiko rangi za mapaa Dodoma

Uamuzi wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dodoma wa kutofautisha kwa rangi mapaa ya nyumba kwenye kata zote 41 umepokewa na wananchi kwa mitazamo tofauti. Uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha robo ya pili ya mwaka, Januari, mwaka huu na utekelezaji wake ulipaswa uanze Machi, mwaka huu. Baadhi ya wananchi wanalalamikia ukubwa wa gharama zinazowakabili ili kubadili rangi kulingana na maelekezo ya Baraza la Madiwani. Tangazo la uamuzi huo linaagiza aina ya rangi na maeneo zikakopaswa kutumiwa. Rangi ya kahawia – maroon chocolate: Madukani, Uhuru, Majengo, Hazina, Kilimani, Viwandani, Makole, Kiwanja cha Ndege, Dodoma Makulu, Kikuyu Kusini, Kikuyu Kaskazini, Tambukareli, Nzuguni, Chamwino, Chang’ombe na Nkuhungu. Nyekundu mpauko – karoti: Iyumbu, Ntyuka, Mkonze na Kizota. Rangi ya kijani mpauko: Kikombo, Mpunguzi, Zuzu, Mbalawala, Chihanga, Mnadani, Msalato, Miyuji na Ipagala. Kijani iliyoiva: Hombolo Bwawani, Ipala, Ihumwa, Matumbulu, Chigongwe na Makutupora. Bluu mpauko – bahari: Mtumba, Chahwa, Ng’hong’hona, Mbabala, Nala na Hombolo Makulu. Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, anasema atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumza suala hilo pindi utekelezaji ukianza. Baadhi ya madiwani na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, wanasema lengo la uamuzi huo kuwa ni kuboresha na kupendezesha mandhari
ya Dodoma.

Diwani wa Kata ya Viwandani, Jafar Mwayemba (CCM), ambaye amewahi kuwa Meya wa Dodoma (ilipokuwa manispaa), haungi mkono uamuzi huo wa kupaka rangi mapaa kulingana na maeneo. “Itamaanisha ukienda Nkuhungu utakutana na rangi inayotofautiana na Viwandani, huu ni ubaguzi sana,” amekaririwa akisema. Anapendekeza mpango huo upate ushauri wa kitaalamu ili kufahamu rangi zinazoruhusiwa hasa jirani na uwanja wa ndege ili usafiri wa anga usiathiriwe. Anasema kaya zenye kipato kidogo hazitamudu kupaka rangi mabati kulingana na vigezo vilivyowekwa. Diwani wa Hombolo Kisiwani, Asedi Ndajilo (CCM) anasema wanaendelea kuelimisha wananchi na mwitiko ni mzuri kwani baadhi yao wameanza kutekeleza maagizo hayo. “Suala la uwezo mdogo wa uchumi kwa baadhi ya kaya tulilijadili na tulidhamiria kwenda nao taratibu kwa muda mrefu na ndiyo maana nguvu tumezielekeza kwenye majengo ya taasisi na mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali pamoja na majengo yote mapya,” anasema. Mkazi wa Area ‘A’, Zuleiya Mvungi, anasema uamuzi uliochukuliwa na Baraza la Madiwani haukuzingatia hali halisi ya maisha ya wananchi wengi.

“Wengi watashindwa kubadili bati au kwa wale walioezeka kwa bati zisizo za rangi watashindwa kuzipaka rangi kwa kuwa gharama ni kubwa,” anasema. Anasema ametumia Sh. 1,046,000 kupaka rangi paa la nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala, sebule, jiko, choo na bafu. JAMHURI limezungumza na baadhi ya mafundi wa ujenzi waliosema gharama za kupaka rangi paa kwa nyumba ya kawaida ni wastani wa Sh. 700,000 kwa rangi ya mafuta na Sh.
600,000 kwa rangi za maji. Mkazi wa Nzuguni ‘C’ Alex Kazoba, pamoja na kutaja gharama kuwa changamoto ya kutekeleza uamuzi huo, anasema kwa kuwa ni uamuzi wa mamlaka halali, utekelezaji hauna hiari. “Wanaojenga nyumba kwa ajili ya kuishi wengi kipato chao ni cha kawaida, kuwaingiza kwenye gharama za kubadili rangi za paa ni mtihani mzito kwao, nashauri utatatibu huu ungezingatiwa na wanaojenga sasa – na siyo waliokwisha kujenga,” anasema Kazoba. Mkazi wa Nzuguni ‘B’, Yoweri Kagashani, amefurahia uamuzi huo kwamba utabadili mwonekano wa jiji na kurahisisha utambuzi wa maeneo. “Hakuna jambo zuri lisilo na gharama, hapa kinachotakiwa ni kuweka utaratibu utakaowezesha utekelezwaji wa agizo hili, nashauri wanaotakiwa kubadili rangi za paa wapewe muda wa kutosha usiopungua miaka mitano,” anasema. Kunambi amenukuliwa na kituo cha televisheni cha Star Tv akisema jiji linakusudia kutunga sheria ndogo ya utekelezaji wa uamuzi huo ili kila kata itambuliwe kwa rangi yake.

“Tatizo ni watu kutosoma sheria, hakuna jambo jipya katika uamuzi uliofanywa, kwa kuwa Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya Mwaka 2007 inatoa uwezo kwa mamlaka kuamua hata kimo cha majengo kwenye eneo lake,” anasema.

Wakili wa Kujitegemea, Karoli Mluge, anakosoa uamuzi wa jiji, akisema una athari nyingine mbali na kipato cha wananchi. Anasema hata sheria inayotoa mamlaka kudhibiti kimo na ubora wa majengo, inalenga kuhakikisha usalama na kwamba rangi za mapaa ya nyumba si suala la usalama. Anatoa mfano kuwa mamlaka inaweza kuzuia majengo marefu jirani na uwanja wa ndege ili kuepusha ajali.
Anasema si kawaida kwa mamlaka kuchagulia watu rangi, kwani binadamu ana sifa za ziada zinazomtofautisha na wanyama wengine..

Kwa sababu hizo, anasema kila mwanadamu hutofautiana na mwenzake katika kuchagua vitu kama mazingira na mwonekano wa mandhari kulingana na utashi, utayari; vitu ambavyo hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Anasema si jambo la ajabu kwa mtu hata kuacha kazi kutokana na kutakiwa kuishi mahala ambako rangi ya paa la nyumba anayotakiwa kuishi ni tofauti na anayoipenda, na kwamba hata ununuzi wa viwanja Dodoma kuna watu watakaoacha kununua maeneo wanayopenda kutokana na kufungwa na aina fulani ya rangi wasizopenda. Ametoa mfano wa mtu anayetaka kujenga eneo la uelekeo wa Dar es Salaam na hapendi rangi ya kahawia, huku rangi anayoipenda ikitakiwa kuwa kwenye uelekeo wa Arusha asikopenda.

“Haitakuwa ajabu mtu huyo kuacha kununua na kujenga au kuishi Dodoma, hilo likitokea itamaanisha mamlaka husika imemnyima haki ya usawa – uhuru wa kuishi anakotaka.

“Tuchukulie mfano wa shabiki kindakindaki wa timu ya Simba, atakuwa ameathiriwa na utashi wa rangi, bila shaka ni mpenzi wa rangi nyekundu. Leo akiambiwa akaishi eneo ambalo paa lake ni rangi ya njano haitashangaza kusikia ameacha kazi ilimradi asiishi eneo hilo,” anasema Mluge.

Anasema kama lengo la uamuzi huo ni kupendezesha mandhari ya jiji, anayependezeshewa mandhari hayo ni nani? Kwa gharama za nani, na ili iweje? Je, jamii husika ina uwezo wa kiuchumi kugharimia utekelezaji huo? “Maswali hayo yote yatahitaji kujibiwa na watakaotunga sheria hiyo,” anasema Mluge